Thursday, May 14, 2015

Wananchi wenye sifa ya kupiga kura Mkalama washauriwa kujiandikisha

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mkalama mkoa wa Singida,James John Mkwenga,akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao cha baraza la madiwani  kilichofanyika katika kijiji cha Nduguti.Kushoto ni Makamu Mwenyekiti Asma Seif na kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Mkalama,Cusbert Mwinuka.
Mkuu wa wilaya ya Mkalama mkoani Singida, Edward Ole Lenga, akizungumza mbele ya kikao cha kawaida cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Mkalama. Ele Lenga alitumia nafasi hiyo kuagiza madiwani na viongozi kuongeza juhudi kuhamasisha wananchi kuisoma na kuielewa vizuri Katiba iliyopendekezwa.

Makamu Mwenyekiti wa halmashauri ya Mkalama, Asma Seif,atoa taarifa yake mbele ya kikao cha kawaida cha madiwani kilichofanyika kijijini Nduguti.
Baadhi ya madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Mkalama mkoani Singida,waliohudhuria kikao cha kawaida cha baraza la madiwani kilichofanyika katika kijiji cha Nduguti.

MWENYEKITI wa halmashauri ya wilaya ya Mkalama mkoani Singida, James John Mkwega,amewataka watumishi wa umma kujiepusha na mihemko ya kisiasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, kwa madai kwamba shughuli za kisiasa hazipo kwenye mikataba yao ya ajira.

James ambaye ni Diwani (CCM) kata ya Gumanga,ametoa tahadhari hiyo juzi wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao cha baraza la madiwani cha kawaida kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo kijijini Nduguti.

Alisema uzoefu unaonyesha wazi kwamba katika miaka ya hivi karibuni, baadhi ya watumishi wa umma wamekuwa wakijiingiza kwenye masuala ya kisiasa hasa vipindi vya chaguzi mbalimbali kinyume na mikataba yao ya kazi.

“Kujiunga huko kumekuwa kukichangia kuvuruga chaguzi na hasa matokeo ya kura mbalimbali na kuleta madhara mengi yasiyokuwa na sababu zo zote. Mtumishi yeyote anayetaka kuingia kwenye siasa,ni vema akafuata sheria,kanuni na taratibu husika ili kuepuka kuwatumikia mabwana wawili kwa wakati moja”,alisema Mkwenga.

Katika hatua nyingine,mwenyekiti huyo ambaye ni mwnjilisti mstaafu wa KKKT Gumanga,alitumia nafasi hiyo kuwasihi wananchi wenye sifa ya kupiga kura kuwa wahakikishe wanajiandikisha kwenye daftari  la wapiga kura bila kukosa.

“Mkazi yeyote wa wilaya ya Mkalama mwenye sifa ya kupiga kura,wakati ukifika wa kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura,asikose kujiandikisha ili muda utakapofika waweze kutumia haki yao ya kidemokrasia katika kufanya maamuzi sahihi ya kuchagua viongozi bora”,alifafanua.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mkalama, Edward Ole Lenga, amewataka madiwani na viongozi kuongeza juhudin katika kuwahamasisha wananchi kusoma na kuielewa kwa kina katiba iliyopendekezwa,ili kuwajengea uwezo wa kutoa maamuzi yao wakati wa kupiga kura.

Aidha, amewataka wananchi wawe makini na baadhi ya watu/viongozi ambao wanaeneza upotoshaji kwa lengo la kukwamisha/kuvuruga mchakato wa katiba iliyopenekezwa.


“Sisi watumishi wa serikali,tafadhali sana,naomba tuendelee kufanya kazi ambazo tumeajiriwa kuzifanya,mambo ya siasa tuwaachie wenyewe wanasiasa.hatukuletwa hapa wilaya ya Mkalama kuja kuwachagulia  Wanyiramba viongozi, hapana hilo sio jukumu letu”,alisisitiza Ole Lenga.

No comments:

Post a Comment