Tuesday, May 19, 2015

Wanawake wahimizwa kusaidia makundi yenye mahitaji maalumu.

Mwanyekiti wa Umoja wa Wanawake watumishi kanisa la Pentekoste (UWW) mjini Singida, Lessi Jared (kushoto) akimkabidhi vifaa tiba Kaimu mganga mfawidhi hospital ya mkoa ya mjini Singida, Dk.Daniel Tarimo.Vifaa tiba  hivyo vingi vikiwa kwa matumizi ya chumba cha upasuaji imedaiwa kuwa gharama yake ni mamilioni ya shilingi, vimetolewa na shirika lisilo la kiserikali la waumini wanawake kanisa Pentekoste nchini Denmark-Heart to Heart.
Mganga Kaimu mganga mfawidhi hospitali ya mkoa mjini Singida, Dk.Daniel Tarimo (wa tano kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na wanachama wa Umoja wa Wanawake watumishi FPCT Singida mjini na baadhi wa viongozi wa kanisa hilo, muda mfupi baada ya kukabidhi vifaa tiba.

Askofu wa kanisa la Pentekoste (FPCT) Singida,  Paulo Samweli (wa kwanza kulia) akizungumza na  mganga mkuu mkoa wa Singida wa kwanza kushoto muda mfupi kabla wanachama wa Umoja wa wanawake watumishi, hawajakabidhi msaada wa vifaa tiba.Katikati ni mchungaji wa FPCT, Boniface Ntandu.

WAUMINI wanawake wa madhehebu mbalimbali wa Mkoani Singida, wamehimizwa kuwa mstari wa mbele katika kusaidia kwa hali na mali makundi ya watu yenye mahitaji maalum, ili kuyapunguzia makali ya maisha.

Pamoja na kuyasaidia kupunguza makali ya maisha, misaada hiyo pia itayajengea imani makundi hayo yaendelee kuamini kwamba na wao, ni sehemu ya jamii ya mkoa wa Singida.

Hayo yamesemwa juzi na mwenyekiti wa kikundi cha  umoja wa wanawake watumish (UWW) wa kanisa la Pentekosti (FPCT) Singida mjini, Lessi Jared, wakati akizungumza kwenye hafla kukabidhi msaada wa vifaa tiba mbalimbali kwa uongozi wa hospitali ya mkoa wa mjini hapa.

Alifafanua, alisema makundi hayo  yenye mahitaji maalum yakiachwa bila kupewa misaada, yatafika mahali yatajenga imani kwamba wao sio sehemu ya jamii ya Singida.

”Sisi akina mama wa kanisa la Pentekoste hapa mjini, kwa muda mrefu tumekuwa tukichangishana wenyewe kwa wenyewe kwa ajili ya  kusaidia wanawake walioko kwenye mahabusu ya magereza, na wajawazito walioko hospitalini na watoto wadogo.Tumejifunza kwamba wenzetu wa makundi hayo, wanayo mahitaji ya msingi mengi na wengi hawana uwezo wa kuyamudu”,alifafanua zaidi mwenyekiti huyo.

Kuhusu msaada wa vifaa tiba hivyo, Lessi alisema msaada huo  wamepewa  na kikundi rafiki cha wanawake waumini wa kanisa Pentekoste nchini Denmark cha Heart to Heart .

“Vifaa hivi vya tiba, ingawa  kwa sasa bado thamani yake hatujaijua, lakini ni vya thamani kubwa kutokana na ubora wake. Vingi ni kwa ajili ya matumizi  ya chumba cha upasuaji katika hospitali hii ya Mkoa”,alisema mwenyekiti huyo.

Lessi alitumia nafasi hiyo kumshukru askofu Paulo Samweli kwa juhudi zake binafsi zilizowezesha kikundi chao kupata msaada huo kutoka marafiki wa shirika la Heart to Heart cha nchini Denmark.

Kwa upande kaimu mganga mfawidhi hospitali ya mkoa Dr. Daniel Tarimo, aliwashukuru wanakikundi hao kwa msaada huo mkubwa, na ametoa fursa hiyo kuwaomba wanawake waumini wa madhehebu mengine ya dini kuiga kitendo hicho, ili hospitali hiyo iendelee kutoa huduma inayokidhi mahitaji.


“Nina imani kwamba wakazi wa Mkoa wa Singida wakiwa na afya bora, watajiletea maendeleo yao na y a mkoa bila matatizo. Sio hivyo tu, bali watakuwa na uwezo mzuri wa kutoa sadaka makanisani na misikitini. Kwa  hiyo kusaidia vifaa tiba hospitali ya mkoa, ni kuiunga mkono serikali kupitia sekta yake ya afya katika kutoa huduma bora”,alisema Dk.Tarimo.

No comments:

Post a Comment