Sunday, June 28, 2015

Sungusungu watuhumiwa kuua vijana watatu

Kamanda wa Jeshi la polisi mkoani Singida, ACP Thobias Sedoyeka akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

VIJANA watatu wakulima na wakazi wa kijiji cha Udimaa wilayani Manyoni mkoani Singida,wamefariki dunia baada ya kupewa kipigo kikali na askari Sungusungu na wananchi wenye hasira kali, kwa tuhuma ya kuvamia duka la mfanyabiashara Robert Francis (23) na kisha kumpora shilingi 1,500,000 taslimu.

Vijana hao ni Mosi Emmanuel (31), Mbasha Mhembano (27) na Mosi Mashauri (31) na wamefariki dunia wakati wakipatiwa matibabu katika hospitali ya wilaya ya Manyoni.

Kamanda wa Jeshi la polisi mkoani Singida, ACP Thobias Sedoyeka, alisema tukio hilo limetokea juni 17 mwaka huu saa nane usiku huko katika kijiji cha Udimaa  wilaya ya Manyoni.

Alisema mfanyabiashara Robert siku ya tukio alivamiwa na vijana hao wanaodhaniwa kuwa ni
majambazi huku wakiwa na silaha za jadi aina ya visu na fimbo na kuporwa fedha hizo.

“Katika purukushani hizo, mlalamikaji aliweza kufanikiwa kuwatambua kwa sura na majina yao kwa vile wote walikuwa wakiishi kijiji kimoja cha Udimaa pamoja na mfanyabiashara Robert”,alifafanua.

Akifafanua zaidi alisema kuwa siku iliyofuta  ya juni 17 mwaka huu, mlalamikaji akiwa na majirani zake na baadhi ya sungusungu wa kijiji cha Udimaa, waliweza kufuatilia nyayo za watuhumiwa na kufanikiwa kuwakamata wakiwa wamejificha katika kijiji cha jirani cha Uhelela wilaya ya Bahi mkoani Dodoma.

“Baada ya kuwakamata,waliwapa kipigo kikali kilichosababisha wapate majeraha makubwa mwilini na walifariki dunia wakati wakiendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Manyoni”,alisema.

Kamanda Sedoyeka alisema jeshi la polisi linaendelea kuwasaka watu waliohusika na mauaji hayo ili waweze kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma ya mauaji ya vijana hao.


“Jeshi la polisi tunarudia kuwakumbusha wananchi kuwa waache tabia ya kujichukulia sheria mkononi bali watuhumiwa wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria, ili sheria ichukue mkondo wake”, alisema Sedoyeka.

No comments:

Post a Comment