Wednesday, June 3, 2015

Wakazi wa manispaa ya Singida walalamikia uongozi kushindwa kuzoa taka ngumu.

Baadhi ya maghuba yaliyopo katika Manispaa ya Singida yakiwa yamefurika taka ngumu kwa muda mrefu sasa kama ambavyo Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Bwana Joseph Mchina alivyokiri katika maelezo yake kushindwa kuzoa kutokana na magari ya kuzolea taka kuchelewa kufika.
WAKAZI wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida wameulalakia uongozi wa Manispaa hiyo kwa kushindwa kuzoa taka kwenye maghuba ya kukusanyia taka ngumu zinazokusanywa na wananchi wa mji wa Singida,licha ya wananchi hao kutozwa ushuru wa shilingi elfu tano kwa kila mwezi kwa ajili ya uzoaji wa taka hizo ngumu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao,Abdallah Daudi Kibiriti,Mwandoghwe Gwao na Avi Mohamedi walifafanua kuwa uongozi wa Manispaa hiyo,akiwemo mkurugenzi kwa kushirikiana na madiwani waliokabidhiwa dhamana ya kusimamia maendeleo kwenye maeneo yao,lakini maslahi zaidi yamewekwa katika kulipana posho za vikao na safari za mara kwa mara za mkurugenzi huyo.

Walifafanua wananchi hao kwamba kutokana na kuwepo kwa hali hiyo,ni wakati wowote ule
magonjwa ya milipuko yanaweza kutokea kutokana na kukithiri kwa uchafu kupita kiasi katika maghuba yote yaliyopo kwenye Manispaa hiyo,huku maafisa afya wakiwa wamekaa kimya wakiangalia mafuriko hayo,na kibaya zaidi kufuatilia fedha kwa ajili ya ushuru wa kukusanya taka.

“Kila kaya inalipa shilingi elfu tano kila mwezi halafu madampo hayo hayazolewi kwa wakati husika,kule mtaani ukipita inabidi utafute kuli abebe mataka ayalete hapa,sasa yule kuli analipwa na halmashauri wamekula hela sasa haya nani abebe mataka haya”alifafanua Abdallah mmojawananchi hao.

“Haya leo yamejaa mpaka hivi tunayaona yamefurika sasa sisi kama wananchi tunataka tusaidiwe nini,maradhi hapa ya milipuko wakati wowote yanaweza yakatokea,twende huku shimo letu la maji machafu limejaa,watu wakileta kule wanakuja gari la Halmashauri lipo,linazoa tu vyoo vya watu,haya hapa siyo maji machafu kwa nini hawaji kuzoa hapa?”alihoji mwananchi huyo kwa masikitiko.

Hata hivyo Kibiriti alisisitiza kwamba ni wakati muafaka kwa viongozi wa Manaispaa kutopuuzia uchafu mpaka uwe umefurika kwa kujifanya hawauoni,na kuelekeza nguvu zao kwenye safari,hususani za mkurugenzi wa Manispaa hiyo.

Kwa upande wake Mkazi mwingine wa Manispaa hiyo,Avi Mohamedi akiongea kwa masikitiko sana alisema dampo hilo lililopo katika soko kuu la mjini hapa,linahatarisha maisha ya wafanyabiashara wake kwani imekuwa ni adha kubwa kwa akina mama lishe wanaouza vyakula sokoni hapa.

Mkazi mwingine wa mjini Singida,Mwandoghwe Gwau kwa upande wake alisema hali hiyo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na mkurugenzi wa Manispaa hiyo kwa kushirikiana na madiwani waliochaguliwa kuwawakilisha wananchi kuweka mbele zaidi maslahi yao kwenye rushwa.

“Na rushwa ni adui wa haki na wananchi hawawezi kupata haki ya kutengenezewa usafi wa hapa pasi kuwa vyombo vya dola kutokuwa wazi kutokana na kupokea rushwa kutoka kwa wazabuni wa kuzoa taka katika Manispaa hiyo.

Alipotakiwa kuelezea kinachochangia kujaa kwa ghuba la soko la Msufini, lililopo katika Mtaa wa Mitunduruni,mlinzi wa ghuba hilo,Shadraki Kiteu alifafanua kwamba kinachochangia kujaa kwa taka hizo ni kukosekana kwa magari ya kuzolea taka hizo kutokana na yaliyokuwepo wamiliki wake wameamua kususia kazi hiyo kwa kutolipwa.

Akizungumza kwa njia ya simu kuhusu tuhuma za wananchi wa Manispaa ya Singida,Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida,Joseph Mchina alisema hali ya uzalishaji na ukusanyaji wa takangumu ni kama inavyoonekana na kwamba zoezi la kuziondoa litaanza kesho ili uchafu uweze kuondoka na kuwepo historia ya usafi katika mji huo.

“Jamani hata sisi hatuifurahii hali hiyo ya uchafu,lakini zoezi la kuziondoa taka ngumu litaanza leo (jumatano 20/05/2015)…hali hii imetokana na magari yetu ya kuzolea taka kuchelewa kuwasili,kwani kusingekuwa na uchafu huo uliopo,

Na kuongeza kwamba,”tafadhali brother tuonane kesho ili niweze kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu zoezi la uandikishaji linalotarajiwa kuanza hivi karibuni na tuachane na suala la madampo kwani hilo linafahamika kwa kila mwananchi”alisisitiza mkurugenzi huyo na kukata simu. 

No comments:

Post a Comment