Sunday, June 28, 2015

WaterAid Tanzania, Singpress kushirikiana mradi wa Mwanzo mwema

Mwakilishi wa shirika la WaterAid Tanzania, Ibrahimu Kabole, akitoa ufafanuzi juu ya mradi wa ‘Mwanzo Mwema’ (A Good Start) ambao pamoja na mambo mengine, utashughulikia afya ya uzazi kwa akina mama wajawazito. Mradi huo unafadhiliwa na serikali ya Sweden.Kulia ni balozi wa Sweden hapa nchini, Lennarth Hjelmaker.

SHIRIKA lisilo la kiserikali la WaterAid Tanzania,limeahidi kushirikiana na klabu ya waandishi wa habari (Singpress) mkoa wa Singida, kwenye utekelezaji wa mradi wa ‘Mwanzo mwema’ (A Good Start) unaodhaminiwa na serikali ya Sweden kupitia shirika la Riksfӧbundet FӧR Sexual Upplysning (RFSU).

Ahadi hiyo imetolewa na Mwakilishi wa shirika la WaterAid Tanzania Dk.Ibrahimu Kabole,muda mfupi baada ya mradi wa Mwnzao Mwema utakaogharamu zaidi ya shilingi 1.4 biloni,kuzinduliwa rasmi mjini hapa na balozi wa Sweden nchini Lennarth Hjelmaker.

Alisema mradi wa Mwanzo Mwema utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu katika halmashauri ya wilaya ya Iramba na manispaa ya Singida,lengo lake ni pamoja na kutoa elimu juu ya uzazi wa mpango,haki za binadamu na mambo yanayoambatana na uzazi.

Dk.Kabole alisema pia
kuwa itatolewa elimu juu ya haki ya wasichana kuamua kuolewa na vile vile kuhamasisha wasichana ikiwemo wale ambao hawakumaliza darsa la saba kupata haki yao ya elimu kadri uwezo wao utakavyowaruhusu.

“Vile vile mradi huu, katika kipindi chake cha utekelezaji,utajikita katika kupunguza/kumaliza kero ya uhaba wa maji,vitendea kazi na kuboresha usafi wa mazingira katika vituo vya kutolea huduma ya afya, ili vituo hivyo viwe kimbilio kwa akina mama wajawazito kujifungulia huko”, alifafanua Dk.Kabole.

Mwakilishi huyo alisema ili malengo ya mradi huo wa aina yake nchini yaweze kufikiwa kwa wakati uliopangwa,mchango wa waandishi wa habari kupitia taaluma yao,unahitajika mno.

“Waandishi wa habari wakitumia vyema taaluma yao katika kuandaa vipindi maalumu au kuandika  makala kwenye magazeti mbalimbali kuelimisha na kuhamasisha jamii umuhimu wa  afya ya uzazi,usafi wa mazingira katika maeneo ya vituo vya kutolea huduma ya afya, wasichana ambao hawajapata elimu waipate haki hiyo,pia wajue kuwa wana haki ya  kuolewa ipo mikononi mwao na haki za binadamu kwa ujumla, lengo la mradi huu litafikiwa kwa ufanisi mkubwa”,alifafanua Dk.Kabole.

Shirika la WaterAid Tanzania litashirikiana na mashirika mengine ya SEMA, Amref, RFSU katika kutekeleza mradi huo unaofadhiliwa na serikali ya Sweden.


Sweden pia  imekuwa mdau mkubwa katika kuendeleza tasnia ya habari nchini kwa kipindi kirefu  ikishirikiana na Umoja wa vilabu vya waandishi wa habari Tanzania (UTPC).Ufadhili wa nchi ya Sweden  umekuwa na miradi ya kutoa mafunzo mbalimbali  kwa waandishi wa habari nchini, na kufadhili vyombo mbalimbali vya ofisi mbalimbali kwa  ofisi za vilabu vya waandishi wa habari mikoani.

No comments:

Post a Comment