Thursday, September 17, 2015

Tundu Lissu amshukia Dk.Slaa kwa madai ya kuponzwa na mkewe.

Mwanasheria wa CHADEMA na mgombea ubunge jimbo la Singida mashariki, Tundu Lissu,akizungumza kwenye mkutano wa kampeni ya Ukawa mkoa wa Singida uliofanyika kwenye uwanja wa Peoples mjini hapa.Pamoja na mambo mengine,Tundu amewaomba wakazi wa Singida, kumpa kura ya ndiyo mgombea urais kwa tiketi ya Ukawa, Edward Ngoyai Lowassa, wabunge na madiwani wa Ukawa,ili kuigaragaza CCM kwa madai imechoka na umechuja mbele ya macho ya Watanzania.

Mgombea ubunge jimbo la Singida mjini kupitia ukawa, Mgana Izumbe Msindai, akiomba kura kwenye mkutano wa kampeni wa Ukawa uliofanyika kwenye uwanja wa Peoples mjini hapa. Msindai ambaye amewahi kuwa mbunge wa jimbo la Iramba mashariki kwa vipindi vitatu mfululizo na mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM wa mikoa nchini,amewata wakazi wa jimbo la Singida mjini kujitokeza kwa wingi oktoba 25 mwaka huu kuichana chana CCM kwa kadi zao za kupigia kura.

Mwanafunzi wa Chuo kikuu Dodoma na mgombea ubunge jimbo la Mkalama mkoani Singida, mwenye umri wa miaka 22,Oscar Kapalale, akisalimia kwenye mkutano wa kampeni Ukawa mkoa wa Singida,uliofanyika kwenye uwanja wa Peoples mjini hapa.Oscar ametoa tahadhari kwamba udongo wa sindano, lakini inao uwezo mkubwa wa kuleta madhara kwa mtu mzima.
Aliyewahi kuwa diwani wa CCM halmashauri ya manispaa ya Singida, Pantaleo Sorongai,baada ya kushindwa kwenye kura za maoni,amekimbilia CHADEMA  kuchukua fomu ya kutetea nafasi hiyo safari hii kupitia tiketi ya CHADEMA.Nyuma ni mwenyekiti CHADEMA mkoa wa Singida, Shaban Limu.
Baadhi ya wagombea udiwani katika manispaa ya Singida kupitia tiketi ya CHADEMA.

SAKATA la DK. Willibord Slaa la kujiuzulu nafasi ya katibu mkuu wa CHADEMA na kuachana na siasa, limechukua sura mpya baada ya kubainika kuwa kitendo hicho kimechangiwa kwa kiasi kikubwa na mke wake (DK. Slaa).

Akihutubia mamia ya wakazi wa jimbo la Singida mjini, Mwanasheria wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu, alisema imebainika kwamba Dk. Slaa hana nguvu yo yote mbele ya mke wake ambaye inadaiwa hajafurahishwa na ujio wa Lowassa  CHADEMA.

Alisema udhaifu wa Dk. Slaa  umeonekana dhahiri baada ya kufukuzwa na mke wake ndani ya nyumba aliyojengewa na CHADEMA na kusababisha alale ndani ya gari usiku kucha.

“Maskini Dk. Slaa, nyumba ambayo amejengewa na CHADEMA , kumbe ameisajili kwa jina la mke wake. Baada ya kikao cha Kamati kuu ambacho Dk. Slaa alikiitisha ambacho kilikubaliana kwa kauli moja ya ujio wa Lowassa. Aliporejea nyumbani kwake na kumpa mke wake taarifa hii, mke wake huyo alimwamuru aondoke mara moja ndani ya nyumba hiyo kwa madai sio ya kwake”,alifafanua Tundu Lissu.

Alisema kwa ujumla uamuzi huo wa kujiuzulu wadhifa wake wa ukatibu mkuu na kuachana na siasa, haujatokana na dhamira yake bali unahisiwa umetokana na mke wake kuchukizwa na kitendo  cha Lowassa kujiunga na CHADEMA na kupewa nafasi ya kugombea Urais.

Akifafanua, Tundu Lissu amesema Dk. Slaa ndiye mwanzilishi au mshenga mkuu wa harakati za Lowassa kujiunga na CHADEMA.

Alisema mapema mei mwaka huu, Dk. Slaa alianza kumshawishi mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe wampokee Lowassa,kwa madai kwamba ni mtu pekee mwenye nguvu ya kukisabaratisha Chama Cha Mapinduzi.

“Baada ya Mwenyekiti Mbowe kukubaliana na ushawishi huo, kamati ya watu watatu iliundwa na Dk. Slaa alikuwa mmoja wao pamoja na askofu Gwajima ambayo ilipangiwa kukutana na timu ya Lowassa,kufanikisha lengo la Lowassa,kujiunga na CHADEMA,kisha aweze kupeperusha bendera ya Ukawa kusaka nafasi ya rais wa tano”,alisema.

Tundu alisema kamati hiyo ya watu watatu katoka CHADEMA na ile ya Lowassa ilifanya vikao karibu kila siku kwa kipindi cha miezi miwili mfululizo, mwisho wa siku,kwa pamoja wanakamati hao walikubaliana na wazo la kumpokea Lowassa.

“Baada ya makubaliano hayo ambayo Dk. Slaa alikubaliana nayo toka mwanzo hadi mwisho, aliitisha kikao cha dharau cha kamati kuu. Lakini  kabla ya kufanyika kwa kikao hicho, Dk. Slaa alibadilika ghafla  na kuanza kudai chama kimenunuliwa kizima kizima, na kwamba hakubaliani na kitendo hicho”,alisema mwanasheria huyo wa CHADEMA.

Hata hivyo,alisema nguvu kubwa ilitumika ikiwemo kumshirikisha baba yake mzazi mwenye umri mkubwa, kumshawishi mwanae Dk. Slaa akubaliane na maamuzi ya wengi, baada ya mazungumzo hayo yaliyochukua muda mrefu,alikubaliana na maamuzi ya wengi.

Tundu alisema Dk.Slaa aliporejea nyumbani kwake na kutoa taarifa kwa mke wake kwamba wamekubaliana Lowassa agombee urais kwa tiketi ya Ukawa, ndipo mwanamke huyo alipochukua uamuzi wa kumfukuza alipo  ndani ya nyumba iliyojengwa na CHADEMA na kupelekea katibu huyo mkuu wa zamani wa CHADEMA,alale ndani ya gari lake.

Katika hatua nyingine, Tundu Lissu ambaye amedai ameshirikishwa juu ya ujio wa Lowassa kwenye hatua ya mwisho tu, alisema Lowassa alipoitwa na kamati kuu ajisafishe  juu ya ufisadi wa Richmond, aliiambia kamati kuu ya CHADEMA, kuwa mhusika mkuu ni rais Kikwete.

“Katika kujisafisha huko,Lowassa alituambia wakati tukio hilo linafanyika,yeye alikuwa ni mtumishi mkuu wa serikali kazi yake ilikuwa ni kutekeleza maagizo kutoka kwa  rais na yale yaliyokuwa yanatolewa na vikao vya baraza la mawaziri.Kimsingi tulikubaliana kwamba Lowassa kama yeye,hahusiki na ufisadi huo”,alisema.

Baada ya kufafanua kuhusu sakata la Dk.Slaa kwa takiribani saa mbili,mwanasheria huyo alitumia fursa hiyo  kumbombea kura Lowassa kwa wakazi wa Mkoa wa Singida, ili kuiondosha madarakani CCM Kwa madai kwamba imechoka na haina jipya tena.

No comments:

Post a Comment