Wednesday, October 7, 2015

Ajali ya basi la City Boys yaua 3, Singida, mwingine agongwa na Noah.1

Kamanda wa polisI Mkoani Singida (ACP) Thobias Sedoyeka (pichani)akizungumza na waandishi wa habari  juu ya kutokea kwa ajali ya basi la City Boys na kusababisha vifo vya watu watatu Wilayani Iramba  na mwingine kugongwa na Noah Singida vijijini.

WATU wanne wamefariki dunia Mkoani Singida baada ya kupata ajali ya kugongwa na basi la City Boys na mwingine Noah wakati wakivuka barabara eneo la Ulemo barabara kuu ya Singida- Nzega.

Kamanda wa polisi Mkoani Singida (ACP), Thobias Sedoyeka alisema ajaili hiyo imetokea jana majira ya 1:00 usiku katika kijiji cha Kitukutu Kata ya Ulemo, Tarafa ya Kinampanda ,Wilayani Iramba.

Alisema siku ya tukio, basi lenye namba za usajili T 846 CDU aina ya Scania  mali ya kampuni ya City Boys likitokea Jijini Dar es Salaam kwenda Kahama lilikuwa likiendeshwa na dereva Adam George (33) mkazi wa Dar es Salaam.

 Aidha alisema dereva huyo alipofika eneo na Kitukutu kutokana na kile kinachosadikiwa kuwa ni
mwendo kasi alijaribu kumkwepa  Samweli Shango (70) ambapo alimparaza kabla ya kuhama upande wa pili wa barabara ndipo aliwagonga wengine wawili ambao ni Agustino Danford ( 34) na  Elibariki Mlega (33) wote wakulima na wakazi wa kijiji hicho.

Hata hivyo alisema chanzo cha ajali hiyo pamoja na uzembe wa dreva ni kwamba marehemu hao  walikuwa wakivuka barabara huku wakiwa wamelewa pombe hali iliyosababisha kutokuheshimu sheria za usalama barabarani.

Katika ajali nyingine mtembea kwa miguu  Elirehemia Bulal (22) mkazi wa kijiji cha Kinyamwenda Tarafa ya Mgori Singida vijijini aligongwa na gari dogo yenye namba za usajili T 387 DDR   aina ya Toyota Noah na kufa papo hapo.

Aidha alisema dereva wa gari hilo Joseph Lesikali (35) mkazi wa Arusha akitokea Mkoani Singida – Manyara, alipofika katika eneo hilo akiwa na mwendo kasi alimgonga mtembea kwa miguu huyo na kufariki dunia.

Hata hivyo kamanda Sedoyeka alisema chanzo cha ajali hizo ni kutokana na uzembe wa madereva kutokuheshimu watumiaji wengine wa barabara, na hivyo kusababisha vifo hivyo.

Sedoyeka alisema katika eneo la Kitukutu Ulemo, Wilayani Iramba wananchi walipanga magogo na mawe kufunga barabara, wakishinikiwa matuta, hali iliyoleta tafrani na hivyo polisi kutumia mabomu ya machozi kutawanya watu hao.

“ Ni kweli tulitumia mabomu ya machozi kutawanya watu pale kwa kuwa walikaidi amri halali ya polisi ya kuwataka wasiweke vizuizi barabarani katika eneo hilo, licha ya kuwaeleza kutii sheria bila shuruti.” Alisema ACP Sedoyeka.


“Nitoe wito kwa madereva kufuata sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika ikizingatiwa kuwa hivi sasa tupo katika kipindi cha Kampeni ambapo kuna mikusanyiko ya watu katika maeneo mbaliambali na pia watumiaji wengine kama waendesha boda boda, mikokoteni na waenda kwa miguu wajaribu kuwa makini namatumizi ya barabara.” Alisisitiza Sedoyeka.

No comments:

Post a Comment