Wednesday, November 18, 2015

YMC yaendesha mafunzo ya siku mbili ya utafiti wa taaluma shule za msingi Manispaa ya Singida.

Mratbu wa shirika la Uwezo mkoa wa Singida, Nason W.Nason, akitoa nasaha zake kwenye mafunzo yaliyohusu kufanywa kwa utafiti juu ya taaluma shule za msingi manispaa ya Singida.Wa pili kulia ni Kaimu Afisa Elimu shule za msingi manispaa ya Singida, Samwel Mwaikenda na (wa pili kushoto) ni Mkurugenzi wa YMC mkoa wa Singida, Fidelis Yunde.
Kaimu Afisa Elimu manispaa ya Singida, Samwel Mwaikenda, akizungumza kwenye ufungaji wa mafunzo ya namna bora ya kufanya utafiti wa taaluma katika shule za msingi manispaa ya Singida.Wa pili kushoto ni Mkurugenzi wa shirika la YMC mkoa wa Singida, Fidelis Yunde.
Kaimu Afisa Elimu shule za msingi manispaa ya Singida, Samwel Mwaikenda, akimkabidhi kijana Juma cheti kwa kuhitimu mafunzo juu ya utafiti wa taaluma katika shule za msingi manispaa ya Singida. Mkurugenzi wa shirika la YMC mkoani Singida, Fidelis Yunde (suti nyeusi) na wa kwanza kulia, ni Mratibu wa shirika la Uwezo Nason W.Nason.

Baadhi ya vijana waliohudhuria mafunzo ya siku mbili yaliyohusu kufanya utafiti juu ya taaluma katika shule za msingi manispaa ya Singida,wakisikiliza ufungaji wa mafunzo hayo.
HALMASHAURI ya manispaa ya Singida, imeahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) na wadau wengine wa maendeleo katika kuboresha sekta mbalimbali,ikiwemo ya elimu.

Ahadi hiyo imetolewa na Kaimu Afisa Elimu shule za msingi manispaa ya Singida, Samwel Mwaikenda,wakati akifunga mafunzo ya siku mbili yaliyohusu utafiti wa taaluma kwenye shule za msingi katika manispaa hiyo.

Alisema NGos na wadau mbalimbali wamekuwa na mchango mkubwa ambao umesaidia manispaa ya Singida kupiga hatua kubwa ya maendeleo.

“Sina uhakika lakini nadhani pengine bila haya mashirika na wadau wengine,manispaa yetu isingekuwa na maendeleo haya makubwa tunayojuvunia  hivi sasa”,alisema.

Kuhusu mafunzo hayo ya utafiti, Mwaikenda amewataka walengwa wa mafunzo hayo wakafanye utafiti ulioshiba ukweli na uhalisia.

“Niwapongeze YMC kwa kuandaa mafunzo haya muhimu ya utafiti wa hali halisi ya taaluma ya elimu kwa wanafunzi wenye umri wa kati ya miaka saba na 16.Ni matarajio yetu kwamba utafiti mtakaoufanya,panoja na mambo mengine,utasaidia sana kuboresha taaluma kwenye shule zetu za msingi”,alifafanua kaimu afisa elimu huyo.

Awali Mkurugenzi wa shirika la YMC mkoa wa Singida.Ferdelius  Yunde,alisema madhumuni na malengo ya mafunzo hayo,ni kuwajengea uwezo vijana 60 wa kuweza kufanya utafiti juu taaluma kwa watoto wenye umri wa miaka saba hadi 16.

Akifafanua, Yunde alisema kuwa vijana hao watafanya utafiti huo kwa kuzingatia uwezo wa kusoma mtoto,lishe pamoja na mambo mengine watakayoelekezwa, ili waweze kutekeleza kwa ufanisi mkubwa kazi hiyo muhimu.

“Nitumie nafasi hii kuwahimiza kwamba nendeni mkaifanye kazi hii kwa uaminifu mkubwa.Fanyeni tafiti kama mlivyoelekezwa mkizingatia ukweli,endapo panakuwa na changamoto zilizo nje ya uwezo wenu,toeni taarifa na tutasaidia kupata ufumbuzi wa kudumu”,alifafanua zaidi Yunde.

Aidha, amewataka watambue kwamba utafiti wao utasaidia serikali na wadau wengine kutambua mapungufu yaliyopo katika shule za msingi,na hivyo kuyatafutia majawabu sahihi.

Kwa upande wake Mratibu wa shirika la Uwezo, lililopo chini ya shirika la Twaweza, Nason W.Nason,alisema tafiti hizo zitasaidia kushindanisha shule za msngi hapa nchini na pia katika nchi za Afrika mashariki, huku lengo kubwa likiwa na kuboresha talaama kwenye shule za msingi.

Kwa mujibu wa mkurugenzi Yunde,mafunzo hayo yameratibiwa shirika la YMC na kufadhiliwa na shirika la Uwezo lililo chini ya shirika la Twaweza.

No comments:

Post a Comment