Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida, SACP Geofrey Kamwela.
Mwili wa mwanaume ambaye hajafahamika jina wala makazi yake anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 28,umeokotwa maeneo ya Misuna makaburini tarafa ya Mungumaji Singida mjini.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida, SACP Geofrey Kamwela, amesema mwili huo umeokotwa saa moja asubuhi ukiwa umetelekezwa kwenye makaburi ya Misuna.
Alisema mwanaume huyo siku ya tukio alikuwa amevaa shati la miramba miramba na suruali aina ya jinsi rangi ya bluu.
“Tulipata taarifa ya tukio hilo kutoka kwa mpita njia na askari walipofika eneo la tukio na kufanya uchunguzi,walibaini kuwa marehemu alifariki dunia baada ya
kuchomwa kisu kichwani mara mbili na kifuani mara nne na mtu/watu wasiofahamika”,alifafanua.
Kamanda Kamwela, ametoa wito kwa wananchi waliopotelewa na ndugu,wafike hospitali ya mkoa wa Singida,waweze kuutambua mwili huo.
Katika tukio jingine,Kamwela alisema kuwa Emmanuel Lucas (33) mkulima na mkazi wa Majengo Singida mjini,amekamatwa kwa tuhuma ya kumiliki kilo saba za madawa ya kulevya aina ya mirungi.
“Mkulima huyo tumemkamata saa 2.14 asubuhi nyumbani kwake Majengo akiwa ameficha mirungi hiyo chini ya kitanda chake”,alisema Kamwela.
No comments:
Post a Comment