Mkuu wa wilaya mpya ya Mkalama
mkoani Singida,Edward Ole Lenga akihimiza shughuli za maendeleo katika
mkutano wa hadhara uliofanyika hivi karibuni katika kijiji cha Gumanga
kata ya Nduguti.
Serikali
ya wilaya ya Mkalama mkoani Singida imeiomba serikali kuu kupitia
OWM-TAMISEMI, kuipatia mamlaka kamili ya halmashauri, ili pamoja na
mambo mengine, kukidhi haja ya maendeleo kwa wananchi wa wilaya hiyo
teule.
Ombi
hilo limetolewa na Mkuu wa wilaya hiyo Edward Ole Lenga, wakati akitoa
taarifa yake ya utekelezaji wa ilani ya CCM ya uchaguzi kwa kipindi cha
kuanzia mwaka 2005 hadi Desemba mwaka jana.
Amesema
upo umuhimu mkubwa wa uwepo wa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri na
wakuu wa idara mbalimbali, kwa ajili ya kuharakisha upatikanaji wa
maendeleo endelevu.
Amesema
kutokana na umuhimu huo, kuna haja kubwa kuanzishwa mapema kwa
halmashauri itakayokuwa kamili kwa kuwa na Mkurugenzi Mtendaji na wakuu
wa idara zote.
Katika
hatua nyingine, Lenga amesema katika kipindi cha kuanzia mwaka
2005/2006 hadi 2011/2012, uzalishaji wa zao la uwele umeongezeka toka
tani 0.8 hadi tani 1.5 kwa hekta, mtama toka tani 1.0 hadi tani 1.5 na
maharage tani 0.3 hadi tani 0.5 kwa hekta.
Lenga
amesema uzalishaji wa mazao hayo umeiongezeka kutokana na matumizi ya
mbolea ya samandi ambayo yameongezeka toka tani 239,658 mwaka 2005/2006
hadi tani 280,000 mwaka 2011/2012.
Aidha, Mkuu huyo wa wilaya amesema kumekuwa na ongezeko la matumizi ya zana bora za kilimo.
Amesema
takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa mwaka 2005 kulikuwa na matrekta 24 na
powertiller 4, hadi kufikia juni 2012, idadi ya zana hizi imeongezeka
na kufikia matrekta 48 na powertiller 31.
Kuhusu
mipango ya baadaye ya wilaya hiyo, Lenga ametaja baadhi ya mipango hiyo
kuwa ni pamoja na kufufua na kuimarisha kilimo cha umwagiliaji ambapo
lengo ni kumwagilia ekari 1,000 ifikapo mwaka 2015 na kuimarisha vyama
vya ushirika wa mazao, ili wakulima waweze kuuza mazao yao ya biashara
kwa faida.
No comments:
Post a Comment