Mbunge wa Singida mjini, Mh. Mohammed Dewji.
HALMASHAURI ya Manispaa ya Singida inatarajia kuwasilisha serikalini maombi maalum ya kuomba jumla ya shilingi 3.5 bilioni kwa ajili ya kugharamia maeneo manne ambayo ni ya kipaumbele katika mwaka wake wa fedha wa 2014/2015.
Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida,Deus Lusiga wakati akiwasilisha mapendekezo ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha mbele ya kikao maalum ya baraza la madiwani kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa manispaa hiyo.
Amesema Manispaa ya Singida imefikia uamuzi huo kutokana na ufinyu wa mapato na uwepo wa changamoto ya kujitosheleza katika mahitaji yake.
Lusiga alitaja vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa jengo jipya la Manispaa linalotarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi 2.7 bilioni.
Kaimu Mkurugenzi huyo alitaja vipaumbele vingine kuwa ni ununuzi wa gari na vifaa vya kuzolea taka ngumu na maji ambayo itagharimu 300 milioni,ujenzi wa madaraja,milioni 200 na ukamilishaji wa nyumba za walimu na madarasa katika shule za msingi ambapo zitatumika shilingi 300 milioni.
Kikao hicho kilichokuwa chini ya Mstahiki Meya,Sheikh Salum Mahami kwa kauli moja kimeazimia kwamba Mbunge wa Jimbo la Singida mjini,Mohammed Gullam Dewji asimamie maombi serikali ili matarajio yaweze kufikiwa.
Awali akifungua kikao hicho,Mstahiki Meya Sheikh Mahami alitumia fursa hiyo kuviomba vyombo vya habari kuitangaza vema na kwa usahihi bajeti hiyo ili
pamoja na mambo mengine jamii iweze kufahamu uwezo wa Manispaa yao katika kuwahudumia na kuwaletea maendeleo endelevu.
“Katika vikao hivi vya bajeti,vyombo vya habari ni muhimu mno kuwepo vitasaidia sana wananchi kujua bajeti ya mwaka husika ya Manispaa yetu na inatarajia kutekeleza miradi ipi ya maendeleo katika mwaka wa fedha husika”,alifafanua Sheikh Mahami.
No comments:
Post a Comment