Wednesday, November 18, 2015

Wanawake wajawazito Manyoni wanapoteza maisha kwa kufuata Huduma za Afya umbali wa zaidi ya KM 30 hadi 40.

Mmoja wa watoto waliofika katika ofisi za Kijiji cha Maweni kwa ajili ya kuhudhuria Kliniki tembezi kutoka katika Hospitali ya misheni ya Kilimatinde,wilayani Manyoni akipimwa uzito na wahudumu wa afya wa Hospitali hiyo.
Watoto wakisalimiana wakati wakisubiri kupatiwa huduma za chanjo kutoka kwa wataalamu wa afya kutoka katika Hospitali ya misheni ya Kilimatinde,wilayani Manyoni.

Jengo la zahanati inayojengwa kwa nguvu za wananchi ambayo itakapokamilika inatarajia kutumia zaidi ya shilingi milioni mia moja.
Ujenzi wa nyumba ya mtumishi wa zahanati inayojengwa kwa nguvu za wananchi wa Maweni ambayo bado inahitaji nguvu kubwa kukamilika.

WANAWAKE wajawazito wa Kijiji cha Maweni, wilayani Manyoni, Mkoani Singida wamekuwa wakipoteza maisha yao kwa kwenda kufuata huduma za afya ya uzazi kwa wakunga wa jadi waliopo umbali wa zaidi ya kilomita kati ya 30 hadi 40 kutokana na kijiji hicho kutokuwa na kituo cha afya au zahanati tangu nchi ilipopata uhuru.

Hayo yalibainishwa na baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Maweni kwenye mahojiano maalumu na mwandishi wa habari hizi aliyetaka kufahamu sababu za ujenzi wa zahanati ya Kijiji hicho kutokamilika licha ya kupauliwa kwa muda mrefu hivi sasa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao, Joyce Karikawe alisema kwa muda mrefu sasa akina mama wajazito hawana huduma za afya jambo linalowafanya watembee umbali mrefu kutoka katika Kijiji hicho hadi kwenye Hospitali ya misheni ya Kilimatinde umbali wa takribani kilomita zisizopungua 30.

Aidha Karikawe alifafanua kwamba pamoja na kufuata huduma hizo Kilimatinde lakini bado kuna baadhi yao wamekuwa wakienda kujifungulia kwa wakunga wa jadi waliopo kwenye maeneo ya kata hiyo,ambayo hata hivyo hupata matatizo makubwa sana,ikiwemo kupoteza maisha yao.

Kutokana na adha hiyo inayowapata wanawake na wananchi kwa ujumla wa kijiji hicho,Karikawe alibainisha kwamba kumewalazimu kufikia maamuzi ya kujenga zahanati katika Kijiji hicho itakayowawezesha kukabiliana na vifo vya akina mama wajawazito vinavyotokana na kutembea umbali mrefu kufuata huduma hizo.

Naye mkazi wa Kijiji cha Maweni, Jacobo Jacksoni Karikawe alifafanua kuwa tatizo la kukosekana kwa zahanati katika Kijiji hicho ni la muda mrefu tangu nchi ilipopata uhuru wake,lakini kutokana na jitihada za diwani wao waliomchagua mwaka 2010 hadi 2015,aliwaonyesha moyo na kuwatia nguvu hadi wameweza kuinua jengo hilo la zahanati.

“Lakini jengo hili bado halijakamilika, jengo hili tunaomba msaada kutoka serikalini kwa sababu kuna akina mama wanatoka umbali wa kilomita 15 hadi 20 wanapata matatizo wengine wanajifungulia njiani”alisisitiza Karikawe.

Hivyo mwanachi huyo alitumia fursa hiyo kuwakumbusha viongozi wa kuchaguliwa kutosahau ahadi wanazowaahidi wananchi wakati wa kampeni za auchaguzi ili waweze kurejesha imani kwa serikali na kuonya kwamba kutotekelezwa kwa ahadi kunachangia wananchi kutokuwa na imanai na vyama vya siasa wakati wa kuomba kura.

Kwa upande wake Yustasi Wilsoni Mahajile aliweka bayana kuwa kutokana na kukosekana kwa huduma hiyo muhimu imekuwa vigumu kwao kukutana na vidonge Kijijini hapo,zaidi ya kwenda kuvifuata kwenye vijiji jirani cha Mvumi,Kintinku hali inayochangia magonjwa ya milipuko pamoja na idadi kubwa ya wagonjwa kupoteza maisha yao.

“Yaani ukishakosa huduma ya afya ina maana magonjwa ya milipuko yanaweza yakatokea na wallio wengi tunakufa,halafu yaani unapokosa dawa ina maana kwamba unatarajia kifo kwa hivyo ukipata zahanati itakuwa ni kimbilio la kuweza kupata maisha pale”alifafanua. 

Hata hivyo kwa upande wake aliyekuwa diwani wa kata hiyo ambaye pia ameshinda katika uchaguzi uliofanyika okt, 25,mwaka huu, Abduli Mwengwa alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2015/2016 Halmashauri ya wilaya ya Manyoni imetenga zaidi ya shilingi milioni 30 kwa ajili ya kusaidia kukamilisha ujenzi wa zahanati ya Kijiji hicho.


Kaimu ofisa mtendaji wa Kijiji cha Maweni,Merina Nyambuya alisema ujenzi wa zahanati ya Kijiji hicho ulioanza mwaka 2012 kwa nguvu za wananchi unatarajia kutumia zaidi ya shilingi milioni mia moja utakapokamilika na kwamba mpaka sasa lilipofikia hatua ya umaliziaji limetumia zaidi ya shilingi milioni 41.

No comments:

Post a Comment