Wanafunzi wenye Ulemavu wa shule ya msingi Ikungi mchanganyiko wilaya ya Ikungi mkoa wa Singida, wakiwajibika darasani.
Shule ya Msingi Ikungi Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya upungufu wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi wenye ulemavu wa kuona (upofu).
Hayo yamesemwa na Mwalimu Mkuu wa shule hiyo,Olivary Kamilly wakati akitoa taarifa yake kwenye mahafali ya 62 ya wahitimu 176 wa darasa la saba mwaka huu.
Amesema upungufu huo unaweza kuchangia wanafunzi hao wenye ulemavu wa kuona,wasifanye vizuri katika mitihani yao ukiwemo wa kumaliza elimu ya msingi.
Aidha, Kamilly alitaja baadhi ya changamoto zingine kuwa ni pamoja na ushirikiano mdogo wa wazazi wa watoto wenye ulemavu kwa kuwaficha watoto wao wenye ulemavu,ili wasipate fursa ya kupata elimu.
“Pia kuna baadhi ya wazazi wachache ambao huzua mambo ambayo huleta hali ya kutokuwa na maelewano mazuri kiasi kwamba hutumia muda mrefu kutatua mtafaruku huo,badala ya kusimamia utoaji wa taaluma”,alifafanua mwalimu mkuu huyo.
Pamoja na changamoto hizo,mwalimu Kamilly amesema wamejipanga vizuri kukabiliana na changamoto mbalimbali za kielimu na matarajio ni kushika nafasi ya kwanza kimkoa na kitaifa kwa ujumla.
“Mheshimiwa mkuu wa wilaya,tunatambua kipaumbele chako cha kutaka kuona elimu katika wilaya yako inapanda na inakuwa bora zaidi.Tunakuahidi
tutashirikiana nawe na kuhakikisha malengo yako ya sekta ya elimu,yanafikiwa”,amesema mwalimu Kamilly.
Kwa mujibu wa mwalimu Kamilly,shule hiyo kongwe imeendelea kufanya vizuri kwenye ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba kwa miaka mitatu mfululizo.Mwaka 2010,ilifaulisha kwa asilimia 79.3,2011 kwa asilimia 76.8 na mwaka jana,asilimia 93.5.
No comments:
Post a Comment