Kaimu Katibu Tawala wa mkoa wa Singida, Aziza Mumba akikata utepe kuzindua nyota mpya ya kijani.
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Aziza Mumba akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Singida wakati wa uzinduzi wa kampeni mpya ya nyota ya kijani kwenye viwanja vya peoples Mjini Singida.
Kaimu Mganga mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Mussa Kimala akizungumza kwenye sherehe hizo.
Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dk Martha Shekinyau akizungumza kwenye uzinduzi huo kwa niaba ya Wizara.
Kikundi cha hamasa cha Mbalamwezi wakitoa burudani.
Baadhi ya viongozi wa Mkoa na Wizara ya Afya wakiwa wamekaa meza kuu.
Burudani mbalimbali za kuvuta kamba kati ya watumishi wa idara ya afya na wadau mbalimbali.
Washindi wa shindano la kufukuza kuku wakiwa na vitoweo vyao baada ya kushinda.
WANANDOA wametakiwa kutekeleza kwa vitendo suala la uzazi wa mpango, ili kuokoa vifo vitokanavyo na uzazi na hatimaye kutoa fursa nzuri zaidi kwa familia kuweza kustawi vyema na kuimarika kiuchumi.
Rai hiyo imetolewa jana mjini hapa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Aziza Mumba, wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni za uzazi wa mpango, naojulikana ‘Nyota mpya ya Kijani’, kupitia wizara yaafya na ustawi wa jamii, uliofanyika Kikanda katika Mkoa wa Singida.
Uzinduzi wa mpango huo, umegawanywa kanda kuu tatu wakati kwa kanda ya kati ukiwa umefanyika mkoani Singida, kwa kanda ya magharibi umefanyika Mkoani Katavi na kanda ya mashariki ulifanyika Jijini Dar es Salaam.
Mumba alisema kuwa, uzinduzi wa kampeni hizo ni sehemu ya mkakati wa wizara ya afya na ustawi wa jamii kwa kushirikiana na asasi zinazotoa huduma ya afya ya uzazi, kuongeza kiwango cha matumizi ya huduma za uzazi katika familia, kwa mikoa hiyo.
“Kampeni hii maalumu itachangia sana kuhamasisha wananchi kutumia huduma za uzazi wa mpango pia kusogeza huduma hizi kwa wananchi, hasa wanaoishi vijijini…nia ni kuongeza watumiaji wa huduma hii kutoka milioni 2.1 kwa mwaka hadi milioni 4.2,”alisema.
Kwa upande wake mshauri mwandamizi wa masula ya afya kutoka chuo kikuu cha John Hopkins, Dk. Rose Madinda alisema kuwa, ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, lazima zitumike njia zote mbili, ya asili na ya kitaalamu.
Aidha Dk. Rose alilaumu tabia ya ndugu, hasa wakwe na mawifi kusababisha mifarakano katika familia za kiafrika kwa kushinikiza kuwa na idadi kubwa ya watoto, hivyo kuchochea migogoro kwa familia husika.
“Utakuta familia inafuata vizuri tu uzazi wa mpango, lakini wao kwa tama zao za kutaka watoto wengi, wanaanza kulalamika mbona sisi tulizaliwa saba, kwa nini wewe na kaka maze watoto wachache!!?…sisi hatukubali umfanyie hivi kaka yetu,”alisema Dk. Rose.
Dk. Rose alisema ongezeko kubwa la watoto kwenye familia nyingi maeneo ya vijijini na mijini, kunachangiwa na sababu mbalimbali, ikiwemo elimu duni ya uzazi wa mpango na imani potofu kwa madhehebu ya dini.
Kutokana na hali hiyo, Dk. Rose aliiasa jamii, hasa ndugu kutoka upande wa wanaume, kuacha kuingilia suala la idadi ya watoto, badala yake suala hilo iachiwe familia husika, ili iweze kuzaa kwa kufuata uzazi wa mpango.
No comments:
Post a Comment