Thursday, May 7, 2015

RC Singida awataka wafanyakazi kutekeleza majukumu yao katika kuzingatia mikataba.

Kaimu mkuu wa mkoa wa Singida na DC wilaya ya Singida, Saidi Alli Amanzi, akimkabidhi cheti cha mfanyakazi bora Nyalandu, ambaye ni Katibu tarafa wa tarafa ya Nduguti wilaya ya Mkalama, jana kwenye kilele cha sherehe za wafanyakazi duniani (mei mosi) zilizofanyika kwenye uwanja wa Namfua mjini hapa.

MKUU wa mkoa wa Singida, Dk.Parseko Vicent Kone, amewaasa watumishi wa umma kuwa wasiwe wepesi wa kudai haki zao, bali kwanza watimize wajibu wao kikamilifu kwa madai kwamba haki na wajibu huambatana pamoja.

Dk.Kone ametoa usia huo wakati akizungumza kwenye kilele cha sherehe za sikukuu ya wafanyakazi (Mei Mosi) mwaka huu, zilizofanyika kimkoa katika uwanja wa Namfua mjini hapa.

Alisema wafanyakazi wahakikishe wanatekeleza majukumu yao kwa mujibu wa mikataba yao ya kazi na kwa njia hiyo, watakuwa wamejijengea mazingira mazuri ya kudai haki zao kwa mwajiri.

Aidha,katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa wilaya ya Singida, Saidi Alli Amanzi, Dk.Kone alisema
ombi la wafanyakazi la kupunguziwa kodi kutoka kwenye mishahara yao,amelichukua na atalifikisha kwenye mamlaka zinazohusika.

“Kwa ujumla, nimeyapokea mengi mliyowasilisha kupitia risala yenu. Yapo ambayo serikali ya mkoa itahitaji kufanya mawasliano na mamlaka mbalimbali husika au wizara, ili kutatua kero hizo, kikubwa muwe na subira na wakati huo huo, endeleeni kuchapa kazi kwa bidii wakati kero zenu zinatafutiwa ufumbuzi”,alisema Mkuu huyo wa mkoa.

Katika hatua nyingine, Dk.Kone alitumia nafasi hiyo kuwataka watendaji waliokabidhiwa dhamana ya kuhudumia watumishi,kuacha mara moja matumizi ya lugha ambazo hadhirizishi mbele ya watumishi wa chini yao, kwa vile lugha chafu pia inakatisha tamaa watumishi wa ngazi za chini.

“Aidha, katika risala yenu imeelezwa kwamba kuna baadhi ya halmashauri hazina mabaraza ya wafanyakazi kabisa,hii ni kukiuka agizo la Rais na hazijaunda mabaraza ya wafanyakazi, kufanya hivyo haraka iwezekanavyo,ili kuwapo fursa wafanyakazi wao kupata sehemu ya kusemea matatizo yao”,alifafanua Dk.Kone.

Awali mratibu wa shehere hizo ambaye ni katibu TUICO mkoa wa Singida, Edwin Nampesya,alisema TUCTA inasikitishwa na uongozi wa hospitali ya Kilimantinde inayomilikiwa na kanisa Anglican, hospitali ya misheni ya kijiji cha Puma na ile hospitali ya Lutheran ya Iambi, kukataa kutambua vyama vya wafanyakazi, kitendo kinachosababisha wafanyakazi wakose  mahali pa kusema matatizo yao.

“Cha kusikitisha zaidi ni pale wafanyakazi wanapotaka kuunda tawi lao,huonekana kama maadui wakubwa na kutishiwa kufukuzwa kazi. Tunaomba uongozi wa serikali mkoa uingilie kati suala hili kwa umakini”,alisema Nampesya.


Kupitia risala yao wafanyakazi wa mkoa wa Singida,wameomba zoezi la kupiga kura lifanyike siku ya Jumatatu, Jumanne, Jumatano,Aalhamisi na lisiguse kabisa siku za Ijumaa, Jumamosi na Jumapili,ili kutoa nafasi kwa waumini kufanya ibada bila bugudha yoyote

No comments:

Post a Comment