Tuesday, May 12, 2015

TASAF yashindwa kukamilisha ujenzi wa meza za soko la kijiji cha Ndago, wilayani Iramba.

Soko la Kijiji cha Ndago,wilayani Iramba lililoshindikana kukamilishwa kwa meza za kufanyia biashara kwa wananchi wa Kijiji hicho kutokana na TASAF awamu ya pili kujitoa kukamilisha ujenzi wa meza hizo kwa kukosa fedha za kufanyikazi hiyo,baada ya kutotengwa kwa fedha za kazi hiyo.


MFUKO wa Maendeleo ya jamii (TASAF) Wilaya ya Iramba,Mkoani Singida umeshindwa kukamilisha ujenzi wa meza za soko la Kijiji cha Ndago kwa zaidi ya miaka mitano sasa baada ya awamu ya tatu ya mpango huo kumalizika kutokana na kutokuwa na fedha zilizotengwa kwa ajili ya kazi hiyo.

Kutokana na meza kutokamilika kumechangia soko hilo kutoanza kutumika na hivyo kuwafanya baadhi ya wafanyabiashara wa Kijiji hicho kufanya ufunguzi usio rasmi na kuanza kupanga biashara ndogo ndogo kama vile nyanya,vitunguu na viazi vitamu chini kwenye sakafu.

Baadhi ya madereva wa bodaboda wa Kijiji cha Nguvumali,kata ya Ndago walibainisha hayo kwa nyakati tofauti walipokuwa wakiongea na gazeti hili lililotaka kufahamu sababu za kutokamilika kwa soko hilo kwa muda merefu sasa ili liweze kuanza kutumiwa na wananchi wa maeneo hayo.

Madereva hao wa bodaboda,Abeli Julius Nkengele,mkazi wa Kijiji cha Nguvumali alifafanua kuwa kuendelea kuchelewa kukamilika kwa soko hilo kunazidi kuongeza gharama za ujenzi wa meza kupanda huku soko likizidi kuendelea kuchakaa na hivyo kuifanya serikali kuingia gharama zingine kubwa kuliko zile zilizokadiriwa kutumika.

Bodaboda hao walifafanua kuwa kukosekana kwa huduma katika soko kunawakosesha mapato katika biashara wanayofanya na kuongeza kuwa kuwepo kwa soko hilo kutawasaidia kupata wateja wenye mizigo inayohitajika kubebwa kwa kutumia usafiri wa pikipiki zao.

“Kuhusu habari ya soko yaani mpaka sasa hivi lilivyofikia,vitu vinazidi kupanda bei na soko linazidi kuchakaa,kwa hiyo serikali itazidi kuingia gharama nyingine ndefu kulikoni kwa sababu vitu madukani vinapanda bei na soko linazidi kuchakaa”alisisitiza Nkengele.

Kwa mujibu wa Nkengele aliishauri serikali kufanya utaratibu wa kuhakikisha soko hilo linakamilika na kuanza kutumiwa na wananchi wa Kijiji hicho kama ilivyokusudiwa na mpango wa Tasaf awamu ya tatu,jambo litakalowasaidia hata wao kupandisha mapato yao kwa siku.

Kwa upande wake mkazi wa Kijiji cha Nguvumali,Peter Maiko ambaye pia ni dereva wa bodaboda aliweka wazi kwamba kutokamilika kwa soko hilo kunatokana na uongozi mbovu wa Kijiji cha Ndago kwa kushindwa kufuatilia wilayani na kusimamia kikamilifu ili meza hizo ziweze kujengwa.

“Kama ni uongozi umeshashindwa basi wakabidhi wafanyabiashara ili wafanye kwa mkataba,ili mtu ajenge meza na akishamaliza afanye biashara mpaka gharama zake zitakapofikia ndipo aendelee kulipa ushuru wa soko,maana tunahitaji kufanyakazi hapa sokoni”alifafanua Maiko.

Akizungumzia malalamiko ya wananchi wa Kijiji hicho,diwani wa kata ya Ndago,Shabani Lyanga Msholo alisema soko hilo lililokuwa likijengwa na tasaf awamu ya pili haliweze kuendelea kujengwa tena kutokana na fedha zilizotengwa kwa kazi hiyo kumalizika na hivyo kwa sasa wananchi wanatakiwa kuchanga fedha za kumalizia ujenzi wa meza katika soko hilo.

Franki Kitundu ni afisa mtendaji wa kata ya Ndago licha ya kukiri kukosekana kwa meza katika soko hilo,lakini hata hivyo alisema kuchelewa kuanza kutumika kwa soko hilo kunatokana na kukosekana fedha za kumalizia ujenzi huo na kuongeza kuwa hakuna fedha zozote zilizotolewa kwa serikali ya Kijiji,bali Tasaf ndiyo wanafahamu zilipo fedha za kumalizia ujenzi wa meza hizo.

Halima Mpita ni Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba alisema tasaf awamu ya pili ilishajitoa kukamilisha soko hilo kwa hivyo Halmashauri inaendelea kutafuta fedha kwenye vyanzo vyake ili iweze kukamilisha ujenzi wa meza hizo haraka iwezekanavyo.

No comments:

Post a Comment