Monday, July 6, 2015

Makala ya kuongeza uzalishaji mazao ya Nyuki kwa kutumia mizinga ya kisasa na kuondokana na mizinga ya asili katika mkoa wa Singida.

HALMASHAURI ya wilaya ya Singida ina ukubwa wa kilomita za mraba 3,787 ambazo wananchi wake hujishughulisha na kilimo na ufugaji.
Mazao ya chakula na biashara yanayolimwa na wananchi hao ni pamoja na mtama,uwele,alzeti,vitunguu na dengu na zao la kipaumbele ni asali kwa ajili ya chakula na biashara.
Halmashauri ya wilaya ya Singida ina maeneo mapana ya ufugaji nyuki ikiwemo misitu ya watu binafsi na misitu ya ardhi ya Kijiji ukiwemo msitu wa Hifadhi wa Mgori,ambapo jumla ya hekta za misitu 55,000 zinatumika katika shughuli za ufugaji nyuki.
Katika Makala hii Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Singida,Linus Mtefu anaelezea namna Halmashauri hiyo ilivyojipanga kuongeza uzalishaji wa mazao ya nyuki ili kuondoa umaskini miongoni mwa wananchi wake.
Anasema Halmashauri ya wilaya ya Singida ina jumla ya
vikundi vya wafugaji 32 vyenye  wajumbe 480 na wafugaji binafsi waliosajiliwa wapaatao 15.
Anasema ili kuongeza uzalishaji wa zao la asali,Halmashauri imeendelea kutoa elimu ya ufugaji nyuki na kuwapatia wanavikundi zana mbali mbali za ufugaji nyuki ikiwemo mizinga,mavazi ya kurina asali na zana za uchakataji wa asali.
Anafafanua kuwa wahisani ikiwemo TASAF II pamojaa na SIDO wametoa mafunzo na zana za kufugia nyuki na uchakataji wa asali.
Kwa mujibu wa Mtefu ambaye pia ni afisa arhi na Maliasili wa wilaya ya Singida kwa msimu wa miaka miwili,Halmashauri imeweza kupata takwimu za uzalishaji mazao ya nyuki.
Anasema kwa mwaka 2012/2013 waliweza kuzalisha asali tani 4.25 zenye thamani ya shilingi 42,500,000/= na nta tani tano zenye thamani ya shilingi 25,000,000/= na  kwa mwaka 2013/2014 waliweza kuzalisha asali tani tano zenye thamani ya shilingi 50,000,000/= na nta tani tatu zenye thamani ya shilingi 15,000,000/=.
“Mh.mgeni rasmi,uzalishaji huu bado upo chini ya matarajio yetu tuongeze uzalishaji wa mazao ya nyuki kibiashara ili kuongeza kipato na lishe bora kwa wananchi na hatimaye kuondoa umaskini miongoni mwa wakazi wa Halmashauri ya wilaya ya Singida”anasema.
Anafafanua kaimu mkurugenzi huyo kwamba suala la ufugaji nyuki katika Halmashauri hiyo litashamiri kwa kiwango kikubwa sambamba na hifadhi madhubuti ya misitu na mazingira kwa ujumla.

Ili kufikia dhamira hiyo Mtefu anasema Halmashauri hiyo ina mpango wa kuimarisha huduma za ugani kwa kuongeza wataalamu katika sekta ya ufugaji nyuki,kuendelea kulinda kwa nguvu zote raslimali za misitu zilizopo,ukiwemo Msitu wa Mgori uliovamiwa na makundi ya watu mbalimbali kwa shughuli za ufugaji na kilimo.

“Kwa suala hili Halmashauri kwa msaada wa ofisi ya Mkuu wa wilaya mwaka 2014 ilifanya doria ya kuwatoa wavamizi mwaka,lakini operesheni hii ilikutana na vikwazo kutoka kwa baadhi ya watu wasioona umuhimu wa kuhifadhi raslimali hii adimu,hivyo Halmashauri itaendelea kusimamia ukweli ili kunusuru msitu huu”alifafanua zaidi.

Anasema mambo mengine yaliyopo katika mipango ya Halmashauri ni pamoja na kuendelea kuhamasisha uanzishaji wa vikundi vya ufugaji nyuki,kutoa elimu kwa wafugaji nyuki kwenye maeneo yao kuanzisha mashamba darasa ya ufugaji,kuwaunganisha wafugaji nyuki na masoko ya ndani na nje ya Mkoa na kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wa mazao ya nyuki wanahakikiwa asali yao na kupata viwango vinavyokubalika kwa TBS na TFDA ili waweze kupata soko zuri la asali.

Hata hivyo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji huyo anasema pia kuwa palipo na mafanikio hapakosi changamoto ambazo amezitaja kuwa ni pamoja na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu faida zitokanazo na ufugaji nyuki,uhaba wa wataalamu wa sekta ya ufugaji nyuki katika vijiji na kata.

Changamoto zingine kwa mujibu wa Mtefu ni gharama kubwa za upatikanaji wa vifaa bora vya ufugaji nyuki ikiwemo mizinga ya kisasa na vifaa vya kurinia na kuchakata asali,hali ya hewa ya ukame au uhaba wa mvua unaopelekea kupungua kwa malisho ya nyuki kwa maana ya muda,uharibifu wa misitu ya asali ukiwemo Msitu wa Mgori na kwa shughuli za kilimo,ufugaji na makazi.

“Mh.Mgeni Rasmi,Katika kukabiliana na changamoto hizi Halmashauri imejipanga kufanya yafuatayo ambayo ni pamoja na kutoa elimu ya ufugaji nyuki,kuajiri Wataalamu wa Ugani,kufanya mipango ya matumizi bora ya ardhi na kuendelea kuwatoa wavamizi wa misitu ya asili”alisisitiza kaimu mkurugenzi mtendaji huyo.

Akisoma taarifa fupi ya ufugaji nyuki Mkoa wa Singida wakati wa maadhimisho ya kutundika mizinga kimkoa iliyofanyika katika Kijiji cha Pohama,wilaya ya Singida vijijini,ofisa misitu wa Mkoa huo,…….Kidua anasema ufugaji nyuki katika Mkoa wa Singida hufanyika kwa kiasi kikubwa kwa njia za asili kwa asilimia 98 na asilimia mbili kwa njia ya kisasa.

Anasema mpaka kufikia mwaka huu wa 2015 Mkoa ulikuwa na mizinga ya asili 127,430 na ya kisasa 14,531,mizinga hiyo inamilikiwa na watu binafsi pamoja na vikundi.Shughuli hizo za ufugaji nyuki zinafanywa kwenye maeneo ya wazi pamoja na misitu ya ardhi ya Kijiji yenye ukubwa wa hekta zipatazo 530,325 za misitu ya asili ambayo ni miombo na vichaka vya Itigi.

Katika kuongeza kasi ya ufugaji nyuki katika Mkoa,kwa msimu huu wa utundikaji mizinga,Mkoa unatarajia kutundika jumla ya mizinga ya kisasa mia sita katika maeneo mbalimbali.

Anasema mfuga nyuki tangu awali alidharauliwa na shughuli zake hazikupewa thamani yeyote hivyo kwa siku hiyo ya utundikaji mizinga,ni dalili tosha kuwa ufugaji nyuki ni miongoni mwa shughuli zenye uwezo wa kubadili maisha ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Afisa huyo mwenye dhamana ya kusimamia sekta ya misitu anasema Mkoa wa Singida unazo fursa nyingi zinazochangia katika ongezeko la shughuli za ufugaji nyuki na kuzitumia vizuri,Mkoa kwa kushirikiana na Halmashauri zote umeweka mikakati mbali mbali ya kufanikisha ongezeko la uzalishaji wa zao la asali na nta.

Anaitaja baadhi ya mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kuhamasisha wafugaji nyuki kutundika mizinga yao mapema ili kuendana na msimu wa makundi ya nyuki,kushirikiana na wadau mbalimbali wa ufugaji nyuki kuweza kupata vifaa mfano mizinga,mavazi na kadhalika ili kuwasaidia wafugaji.

Nyingine ni kuimarisha huduma za ugani vijijini ikiwemo kuendesha zoezi la ugawaji makundi ya nyuki yaliyo makubwa kwenye mizinga na kufukuza makundi mavivu katika uzalishaji,kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye mizinga ili kubaini na kurekebisha mapungufu mbalimbali na kutumia sheria na kanuni zilizopo ili kudhibiti uharibifu wa misitu unaoendelea kwenye maeneo yaliyohifadhiwa,na kutoa mfano mzuri ni uharibifu unaoendelea ndani ya msitu wa Mgori.


Hata hivyo Kidua anasema zipo changamoto zinazokabili sekta ya ufugaji nyuki katika Mkoa wa Singida ambazo ni pamoja na upungufu wa wataalaamu wa ugani,uharibifu wa mazingira unaopelekea kupungua kwa makazi ya makundi ya nyuki na uelewa mdogo miongoni mwa wafugaji nyuki juu ya suala zima la kufuga nyuki kibiashara.Hali hiyo inapelekea wafugaji nyuki kuendelea kufungasha asali yao kwenye vyombo visivyofaa mfano chupa zilizotumika kwenye vileo mbalimbali mfano konyagi.

Aidha Kidua anazitaja changamoto kuwa ni msukumo mdogo unaotolewa na baadhi ya Halmashauri kwenye sekta ya ufugaji nyuki pamoja na kuongezeka kwa mabadiliko ya tabianchi yanayoathiri shughuli za ufugaji nyuki wenyewe.

Ili kukabiliana na changamoto hizo Kidua anasema Mkoa umejipanga kutumia mbinu shirikishi katika hifadhi ya misitu ya ardhi ya vijiji, vikundi, taasisi na watu binafsi, kuongeza thamani ya mazao ya nyuki ili kupata soko la ndani na nje ya nchi,kuendelea kuomba nafasi za ajira za wataalamu wa ufugaji nyuki kwenye Tume ya Utumishi wa Umma na kuendelea kuwatumia wataalamu wa ufugaji nyuki wa Wakala wa Misitu Tanzania ili waendelee kutoa huduma za ugani wilayani.

Akiwahutubia wananchi wa Kijiji cha Pohama,tarafa ya Mgori,wilaya Singida vijijini wakati wa maadhimisho ya siku ya Taifa ya Utundikaji mizinga ngazi ya Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk.Parseko Kone anasema lengo kuu la siku ya  kutundika mizinga ni kuhamasisha ufugaji nyuki ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya nyuki kwa kuzingatia ubora na teknolojia sahihi,na kwa msimu huu jumla ya mizinga mia sita imetundikwa katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Singida.

Anafafanua mkuu huyo wa Mkoa kwamba kwa kutumia teknolojia sahihi wananchi watazalisha mazao mengi na yenye ubora unaokidhi viwango vya soko la kitaifa na kimataifa.Hiyo itawezesha wafugaji nyuki kupata bei nzuri na kuwaongezea kipato na hivyo kuchangia katika kuboresha hali za maisha na kukuza uchumi wa nchi pia.

“Ndugu wananchi,Taifa limeamua kutenga siku ya leo iwe ni siku ya kutundika mizinga ambapo maadhimisho ya kwanza ya kitaifa yalifanyika katika Mkoa wetu,wilayani Manyoni katika Manzuki ya Taifa ya Aghondi mnamo tarehe 04,machi,2013 na kuhudhuriwa na Mhe.Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”alisisitiza Dk.Kone.

Kwa mujibu wa Dk.Kone mnamo mwaka 2006 Mkoa ulitunga kitabu cha mwongozo wa kilimo na ufugaji na kuainisha mazao ya kipaumbele katika Mkoa,na moja ya mazao hayo ni asali.Mkoa ulichagua zao hilo kutokana na sababu nyingi ikiwemo bei nzuri ya zao la asali katika soko la ndani na nje ya nchi,urahisi wa shughuli yenyewe ya ufugaji nyuki isiyohitaji muda mwingi na mtaji mkubwa katika utekelezaji wake na hali ya hewa na uoto wa asili uliopo katika Mkoa wa Singida.

Anasema Mkoa wa Singida ni miongoni mwa Mikoa yenye raslimali nyingi na nzuri zinazofaa kwa shughuli za ufugaji nyuki,kwa kuwa una misitu ya jamii ya miombo,mbuga na jamii ya vichaka vya Itigi ambavyo ni adimu duniani na vyenye uwezo wa kutoa asali bora ya kupigiwa mfano katika soko la asali ndani na nje ya nchi.

Hata hivyo Dk.Kone anafafanua kuwa fursa za uzalishaji wa mazao ya nyuki katika Mkoa wa Singida ni kubwa,na kwa kuzingatia kuwa makundi ya nyuki bado ni mengi,maeneo ya ufugaji yapo na wananchi wengi wanao utaalamu na uzoefu wa asili wa ufugaji nyuki,kinachotakiwa kwa upande wa serikali ni kuhamasisha na kuboresha ufugaji bora wa nyuki kwa kutumia teknolojia sahihi.

Kwa kutambua fursa hizo,Mkoa umeweka mikakati kadhaa ili kuhakikisha kuwa ufugaji wa nyuki unashamiri na kuwapatia wananchi kipato kizuri cha kujikimu katika mahitaji ya kila siku.

Ameitaja baadhi ya mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kuelimisha na kuhamasisha wananchi,viongozi wa kiserikali,kisiasa kuhusu faida zinazopatikana kutokana na ufugaji wa nyuki,kuajiri wataalamu wa fani ya ufugaji nyuki wa kutosha wenye sifa na kuwapatia vitendeakazi,ikiwemo kuanzisha vitengo vya ufugaji nyuki katika Halmashauri kama alivyoagiza Waziri Mkuu kwenye maadhimisho yaliyofanyika Manyoni.

Kuanzisha vikundi vya wafugaji nyuki ili wapate huduma ya pamoja kwa kufikiwa kwa urahisi na kutengewa maeneo ya kufugia nyuki kisheria,kuweka mkazo katika kuyapatia makundi ya jamii ambayo hutegemea sana asali kama sehemu ya chakula chao kikuu na kutoa mfano kabila la Wahadzabe na Wabarbaig  wataalamu wa kuwafundisha juu ya ufugaji bora na endelevu badala ya kutegemea asali kutoka kwenye mapango ya miti na ardhi.

“Pamoja na elimu hiyo,nimeambiwa kuwa jamii ya Wahadzabe wamepatiwa mizinga ipatayo 360 ya kisasa,hii ni hatua nzuri katika kuwajali na kuwapatia mahitaji yao ndugu zetu hawa”alifafanua Dk.Kone.

Kushawishi wakulima kuanzisha ufugaji wa nyuki katika mashamba yao ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara kwa njia ya uchavushaji maua.Pia anakiri kuwa ameelezwa kwamba asali itokanayo na maua ya alzeti ni nzuri sana.

Aiidha Dk.Kone anautaja mkakati mwingine kuwa ni kuhakikisha kwamba kila Halmashauri imeunda ushirika ambao utawasaidia wafugaji kupata soko la mazao ya nyuki kwa kuwa na sehemu moja ya kuuzia mazao hayo.Vile vile pia mkakati huo utatekeleza agizo la Mh.Waziri mkuu la kuunda ushirika wa wafugaji nyuki katika kila Mkoa.

“Bahati nzuri tumeanza mchakato wa kuunda chombo cha wafugaji nyuki ngazi ya Taifa,ambapo mimi ni Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi”anasisitiza mkuu huyo wa Mkoa.

Kwa mujibu wa Dk.Kone katika kutekeleza mikakati hiyo iliyopendekezwa,Mkoa umejipanga kwa kuanza na kutambua na kupima maeneo yote yanayofaa kwa shughuli za ufugaji nyuki,kuorodhesha wafugaji nyuki waliopo na maeneo wanayofugia ili yaweze kutambuliwa na kuendelezwa na kujenga kiwanda cha kuchakata asali ambacho tayari serikali kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Ulimwenguni (ILO) imejenga kiwanda tayari kwa matumizi.

Kuhakikisha kuwa asali inayozalishwa katika Mkoa wa Singida inaendelea kushika nafasi ya kwanza kwenye mashindano ya Kikanda na Kitaifa kwa kuendelea kuzalisha   asali yenye ubora wa hali ya juu.

“Tunapozungumzia ufugaji nyuki hatutakwepa suala zima la hifadhi ya mazingira,kwani bila hifadhi ya mazingira iliyo madhubuti suala la ufugaji nyuki litakuwa hadithi tu.Aidha ili tuweze kufanikiwa katika hifadhi ya mazingira naziagiza Halmashauri zote za Mkoa wa Singida kufanya mambo yafuatayo”alisisitiza Mkuu wa Mkoa huyo.

Kwa mujibu wa agizo la Dk.Kone,kila Halmashauri haina budi kuwaondoa wavamizi wa misitu hasa kwenye misitu ya vijiji vya Mgori,Minyughe,Mlilii,Sekenke/Tulya,Wembere,Chaya na maeneo yaliyoharibiwa,kuongeza juhudi katika kupanda miti na kuitunza kwenye maeneo mbalimbali yakiwemo makazi,machimboni na vyanzo vya maji.

Kuzuia ukataji miti ya asili kwa ajili ya kukaushia tumbaku na kuwashauri wakulima wa tumbaku kupanda miti kwa ajili ya matumizi yao,kutunga na kuhimiza matumizi ya sheria ndogo za uhifadhi wa mamzingira,ardhi na vyanzo vya maji pamoja na kutumia kamati za mazingira za vijiji kuzuia uchomaji na ukataji miti ovyo kwa shughuli za uchomaji mkaa.

“Ndugu wananchi,Leo hii tumetundika mizinga ya kisasa kwenye eneo la ukanda wa pili wa msitu wa hifadhi wa Mgori Kijiji cha Pohama eneo hili ni zuri kwa shughuli za ufugaji nyuki kama tulivyoona,eneo hili lina mimea ifaayo kwa shughuli za ufugaji nyuki pamoja na maji ya kutosha”anasema Dk.Kone.

Kutokana na hali hiyo mkuu huyo wa Mkoa anatumia fursa hiyo kuwasihi sana wananchi wa eneo hilo wakiwemo wanakikundi cha ufugaji nyuki kuweka mizinga ya kutosha ili eneo hilo litumike inavyopaswa.

“Ningependa kutumia fursa hii pia kuwapongeza wananchi ambao wanatengeneza mizinga yao wenyewe na kuitundika.Napenda pia kuwapongeza na kuwatia moyo wale wote wanaomiliki misitu ya asili na ile ya kupandwa kwa lengo la kuhifadhi mazingira na pia kuitumia katika kuongeza kipato na kwa mahitaji yao binafsi”anasisitiza kiongozi huyo wa mkoa.

Dk.Kone hata hivyo anatumia fursa hiyo kutoa wito kwa kila familia kuanzisha utaratibu wa kujitengenezea mizinga miwili tu na kuitundika kila mwaka,sambamba na kuunda vikundi kwani wakiwa kwenye vikundi ni rahisi kupata misaada.

No comments:

Post a Comment