Saturday, December 31, 2011

Mkuu wa kanisa KKKT nchini Alex Malasusa(kulia), akiwa na Askofu wa kanisa hilo Dayosisi ya kati, Singida, akiwa amesimama mbele ya msalaba wa Yubile ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa kanisa hilo Mkoani Singida, mwaka 1911, mbele ya msalaba ni mti mkubwa uliotumika kama kanisa la kwanza,ambapo watu wanne mwaka huo walibatizwa hapo na wamisionari Leipzing kutoka nchini Ujerumani.

Mmoja wa Wachungaji wa kanisa hilo kutoka Ujerumani, akitumia sherehe hizo kubatiza mtoto katika eneo lililotumiwa kwa mara ya kwanza na Wamisionari mwaka 1911, kwa kutumia jiwe lililotunzia maji ya ubatizo,(kushoto) ni askofu mkuu wa KKKT nchini, Alex Malasusa.


Askofu mkuu wa KKKT Alex Malasusa (kulia),akiwa amesimama na Askofu wa Dayosisi ya kati, Eliufoo Sima, mbele ya msalaba uliojengwa mbele ya mti (nyuma) ambao ulitumiwa na wamisionari kutoka Ujerumani, kama kanisa mwaka 1911, ambapo watu wazima wanne walibatizwa

ASKOFU mstaafu wa Kanisa la KKKT, Dayosisi ya kaskazini, iliyopo Mkoa wa Kilimanjaro, Erasto Kweka, amewataka waumini wa dini na wananchi kwa ujumla kufanya kazi kwa bidii, ili kujiletea maendeleo.

Amesema hayo,kwenye sherehe za Jubile ya miaka mia moja ya KKKT, Dayosisi ya kati, ambazo kilele chake kitafikia leo(Jumapili),eneo la kitovu cha kanisa hilo, katika kijiji cha Ruruma, kilichopo Iramba,Mkoani Singida.

Wageni mbalimbali, wakiwemo wachungaji,maaskofu na wengine kutoka nje ya nchi,wamealikwa kwenye sherehe hizo,baadhi wakiwemo kutoka barani Ulaya na nchini Marekani, kutokana na umuhimu na mchango wao katika kueneza Injili, Dayosisi ya kati.

Askofu wa Dayosisi ya kati, Eliufoo Sima, amesema Wamisionari wa kwanza eneo hilo ni Leipzing Lutheran la Ujerumani 1911-1917,baadaye Augustina la Marekani mwaka 1926-1958, kisha kanisa likaendeshwa na wazalendo kuanzia mwaka 1958 hadi sasa.

Thursday, December 8, 2011

Jamii Ya Wahadzabe

Mhadzabe Bw. Maidona Wazaeli akiwa mbele ya nyumba yake.

Jengo moja lenye vyumba viwili vya madarasa ambalo halijakamilika kwa ajili ya wanafunzi wa chekechea, lililojengwa na kanisa la KKKT Dayosisi ya kati kwa gharama ya Sh.Milioni 25/=.

Nyumba ya Mhadzabe inavyoonekana baada ya kukamilika na watu kuishi ndani.

Picha ya mtoto wa Kihadzabe, kweli mtoto wa nyoka ni nyoka. Mtoto huyo anajifunza jinsi ya kutumia pinde na mshale hukohuko porini.

Mwandishi wa Habari Leo na Dailynews mkoa wa Singida Bw. Abby Nkungu akitoka ndani ya nyumba ya Mhadzabe.

Ndugu zetu Wahadzabe bado wanahitaji msaada ingawa jamii ya wafugaji inawaingilia katika makazi yao kwenye pori la Kipamba, wilayani Iramba,Singida.

Maadhimisho ya Siku Ya Mlipa Kodi Singida

Mkuu wa mkoa Singida Dk.Parseko Kone Akizungumza na wafanyabiashara katika jukwaa la Mabula,la kanisa Katoliki mjini Singida, ambao walifanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato na kuzawadiwa cheti maalumu na TRA

Mwenyekiti SINGPRESS akipokea cheti

Chama Cha Waandishi wa habari mkoa wa Singida(SINGPRESS), nacho kilizawadiwa cheti baada ya kushika nafasi ya pili, nyuma ya ofisi ya mkuu wa mkoa, kwa UHAMASISHAJI wa ukusanyaji mapato na kazi zingine za TRA. Nafasi ya tatu ilinyakuliwa na Faisal Cable network.

Wadau walioshiriki katika hafla hiyo

Ofisi za TRA Singida

Sunday, December 4, 2011

Ujumbe Kwa Walaji Kabla Ya Kununua Msosi Singida


Ujumbe wa leo Jumpili kutoka Singida

Bei ya vyakula katika soko kuu la mjini Singida imepaa na kupelekea mfanyabiashara aliyetambuliwa kwa jina moja la Mr. Mborrouw kutoa ujumbe elekezi kwa wateja wake ili wauelewe ipasavyo- 'Huwezi Kuamini' na 'life is difficut', jumbe hizi zipo kwenye magunia ya mchele anaowazia wateja

Saturday, December 3, 2011

Lowassa amwaga sumu Singida asema;"Mungu Yupo Na Mimi Nitayashinda Majaribu"

Askofu Mkuu wa Kanisa la kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT Dayosisi ya Kati Mch, Eliufoo Sima akitoa mahubiri katika kanisa hilo usharika wa Amani Sabasaba mjini Singida wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa hilo ulioendeshwa na Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowasa.

Askofu wa KKKT Mchungaji Eliufoo Sima akipokea kiasi cha shilingi milioni 10 taslimu kutoka kwa Mhe.Lowasa kama mchango wake katika kufanikisha harambee ya ujenzi wa kanisa hilo.

WAZIRI Mkuu Mstaafu Mhe.Edward Lowasa amesema kuwa pamoja na kusemwa maneno mengi sana kwenye vyombo vya habari juu yake lakini anamwami mungu kuwa anampigania kila kukicha.
Mwandishi wa mtandao huu kutoka mkoani Singida Hillary Shoo anaripoti kuwa Lowasa ameyasema hayo leo mjini Singida wakati wa harambee ya ujenzi wa kanisa la KKKT usharika wa Amani sabasaba mjini Singida. “Wale wanaofuatilia siasa za nchi yetu kuna maneno mengi saana lakini bwana ni mwema na mwaminifu hatimae tumeshinda”.Alisema. Alisema mara baada ya taarifa hizo siku moja akiwa nyumbani kwake na mkewe huku wakiangalia TV na kutaka kujua magazeti yanasemaje asubuhi kulikuwa na maneno mengi yaliyosemwa ya hovyo hovyo juu yake mengine walishindwa kuyasoma.


“Lakini mke wangu alienda chumba cha pili na kuchukua biblia na kunifungulia maneno ya bibilia kitabu cha Isaya 41:10, usiogope kwa maana mimi niko pamoja nawe tusifadhaike kwa maana mimi ni mungu wako nitakutia nguvu naam nitakusaidia, naam nitakushika mkono wa kuume wa haki yangu.” Alisema na kuongeza kwa maneno hayo niliendelea sana lakini baba askofu nisamehe nichukue hadhara hii kuwashukuru watu wengi sana walioniombea na hatimae kufika hapa nilipo. “Wapo waislamu na mashekhe walifanya dua kwa niaba yangu, nawashukuru sana, pia wapo wakristo walioniombea nao nawashukuru sana, mapadri, mashemasi na watawa, wachungaji na wainjilisti wa madhehebu yote, kwaya bmbalimbali na waimbaji wa nyimbo za injili, wanamaombi wote, wanamtandao wao wa ajabu una nguvu kweli kweli na maaskofu wa makanisa yote ya kikristo pia nawashukuru sana.” Alisema Lowasa.


Aidha Mhe Lowasa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli alisema kuwa maneno mengi ya kisiasa yalisemwa juu yake lakini kimsingi hayakuwa ya kweli ya ukweli na siasa zinazoendelea kwa sasa ni za kuchafuana. Pia Lowasa alinukuu maandiko mengine ambayo aliyasoma kutoka kitabu kitakatifu cha Warumi ambayo aliyasoma mwenyewe. “ Lakini ikiwa roho yake yeye aliyemfufua yesu katika wafu anakaa ndani yenu yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu hataihuisha miili yemu iliyo katika hali ya kufa kwa Roho wake anakaa ndani yenu” alinukuu Lowasa.Aidha alisema kutokana na misukosuko ya kisiasa ambayo amekumbana nayo amekuwa akimwona mungu akimtetea na utetezi huo ameupata kutoka kwa mungu, kutokana na maombi ya watakatifu kutoka dini mbalimbali ambao wako pamoja.


Wale wote ambao wamaamini kuwa nafanya kazi kwa kusimamia haki ya mungu na kazi zote kwa ujumla waliniombea usiku na mchana na kwa hilo mungu kawasikia na kanifanya kuendelea tofauti na uchafu ambao mimekuwa nikibambikizwa na siasa za kuchafuana. Hata hivyo Lowasa alidai kuwa kama kiongozi hana mungu ndani yake hawezi kuhimili mikiki ya kisiasa kwani kinachotakiwa ni kumwomba mungu ili aweze kutetea kazi zinazofanywa na mtu mwenye haki. “Nimekuja kwenye harambee sio kupiga maneno ya kisiasa, nilimwambia baba askofu tuna utamaduni wa kualikwa haramabee nyingi sana , lakini kabla ya kukubali unauliza kwamba hao unaoshiriki nao wamefanya nini, nyie mmefanya kazi kubwa sana nawashukuru na nafurahi kwenye harambee hii.” Alisistiza na kuongeza.


“Kwa sababu ni njia mojawapo ya kuthibitisha kwamba wananchi wanaweza kufanya mambo yao kwani kanisa kama hili miaka ya nyuma lingeweza kujengwa na wafadhili wa nje lakini leo limejengwa na wananchi wenyewe. Mapema askofu mkuu wa KKKT Dayosisi ya kati Mchungaji,Eliufoo Sima anaamini utulivu wa viongozi wa nchi hii ni dhahiri kwamba Taifa hili kwa jinsi ya utamaduni na mapokeo yake , na mambo magumu yanayotokea siku hadi siku, litafanikiwa kutengeneza njia thabiti ya mafanikio ya watu wake. Askofu Sima alisema kumekuwepo na madai mengi kuwa nchi yetu ni maskini lakini angependa viongozi kuyashughulikia kwa umakini mkubwa ili kuondoa manung’uniko miongoni mwao ili yasiharibu tabia njema ya baadhi yao. Hataa hivyo Askofu Sima alimwagia sifa Mhe.Lowasa na kusema kuwa ni tofauti na viongozi wengine ambao unaweza kuwatafuta kwenye simu kwa muda mwingi na wakawa hawapatikani.


“Kwa kweli wewe ni kiongozi wa pekee,tofauti na wengine,unaweza ukmtafuta kwenye simu hata mara tano na hapatikani, lakini wewe kila ninapokupigia unapokea simu yangu,na hata katika harembee hii nilipokupigia nikakuomba uje Singida ukasema upo njiani unaenda Dodoma,”. “Lakini na mimi nikakwambia nipo njiani naenda Morogoro,ukasema basi tukutane njiani,mtu mkubwa kama wewe kukutana njiani hiyo ni ajabu.”alisema Askofu. Katika harambee hiyo Mhe.Lowasa amechangia kiasi cha shilingi milioni kumi ambapo makusanyo yote yaliyopatikana katika ujenzi wa kanisa la Kanisa la Kiinjili la Kirutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Amani zilipatikana zaidi ya shilingi milioni 138. Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini liliko Kanisa hilo Mohammed Dewji (MO) alichangia shilingi milioni 10, Mfanya biashara maarufu hapa nchini aliyemtaja kwa jina moja tu la Patel amechangia mabati ya kuezekea kanisa hilo yenye thamani ya shilingi milioni 50. Kanisa hilo la usharika wa amani linatarajiwa kukamilika mapema hapo mwakani kwa gharama ya kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 480.

Sakata La Wafanyabia​shara Wa Kuku Singida

Wauza kuku wakichukua mizoga kutoka kwenye mfereji.

Wauza kuku wakionysha kuku waliokufa kwa joto kali.

Wauza kuku Singida wakishuhudia kuku waliokufa kwa joto kali.

WAFANYABIASHARA wa kuku mjini Singida wamelalamikia mkurugenzi wa manispaa kwa madai kuwa amesababisha maelfu ya kuku kufa,wakati akidai ushuru, wakati alipolishikilia lori lililopakia kuku kwenda jijini Dar es Salaam, kwa saa 24.
Akiongea na waandishi wa habari eneo la soko kuu jana, mkurugenzi wa wauza kuku mjini Singida, Selemani Mohammed Kuku alisema, kutokana na hasara kubwa waliyoipata,wanatarajia kuipandisha kizimbani manispaa hiyo, ili awalipe fidia.
Kwa mujibu wa Kuku, wafanyabiashara katika soko hilo wamepata hasara ya maelfu ya fedha, kutokana na kuku zaidi ya 2,000 kufa, kwa kukosa hewa, baada ya lori walilokodi kushikiliwa na manispaa, kwa zaidi ya saa 24.
Kuku ambaye pia mwenyekiti wa mtaa wa Majengo mjini hapa kwa tiketi ya CCM, alidai busara ndogo ingetumika kudai fedha za ushuru,zingeokoa kiasi kikubwa cha fedha za wajasiriamali hao, ambazo zimepotea bila sababu ya msingi.
“Sikilizeni ndugu waandishi,nina miaka zaidi ya 40 nikifanya biashara hii ya kuku, lakini utaratibu uliotumika kushikilia lori siyo sahihi….kuku akipakiwa jioni, gari linakimbia kasi ili kupata hewa ya kutosha na hadi alfajiri liwe sokoni,Dar es Salaam….,”alisema kwa masikitiko Kuku.
Alisema tayari mwanasheria wao ambaye hakutaka kumtaja jina, anakamilisha taratibu za kisheria,ili mkurugenzi alazimishwe kuwalipa stahili zao.
Waandishi wa habari waliotembelea eneo la soko la kuku mjini Singida walijionea maelfu ya mizoga ya kuku, ikiwa imerundikwa pamoja, huku baadhi ya wafanyabiashara wakiwa na huzuni na kujawa na hasira kali, hata baadhi yao kuthubutu kutoa lugha chafu juu ya kitendo hicho na wengine wakiomba kupewa kadi mpya, toka vyama vya siasa.
Hata hivyo baadhi ya askari polisi walioongea na NIPASHE kwa sharti la kutotajwa majina, walilaumu kitendo cha uongozi wa manispaa kutumia jeshi la polisi kudhibiti vurugu, badala ya kutumia askari wake wao, waliowaajiri.
Jumatano wiki hii, katika vurugu hizo,ambazo zilizotokana na lori lililopakia kuku,kushikiliwa na manispaa,baada ya askari wa usalama barabarani kulizuia lori la Fuso namba T. 125 BES likiwa njiani kwenda Dar es Salaam, askari mmoja alichaniwa sare ya shati na kusababisha wafanyabiashara kumi, kutiwa nguvuni na polisi.
Uongozi wa Manispaa ulikuwa unadai ada ya ushuru mpya wa kuku mmoja kwa Sh.300, sawa na Sh.30,000,kwa tenga moja lenye uwezo wa kubeba kuku 30, badala ya ule wa zamani wa Sh.1,000.
Kwa upande wake, kaimu mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Salome Singano, alisema, ada hizo mpya zimetokana na maamuzi ya baraza la madiwani la aprili,mwaka huu,iliyosainiwa na waziri mkuu, kabla ya kutangazwa katika gazeti la serikali,Oktoba7,2011. Alisema, mchakato wa sheria hiyo inayojulikana kama ’Sheria ndogo ya halmashauri ya manispaa ya Singida, ada na ushuru 2011’, ilipelekwa kwanza kwa wananchi na kubandikwa kwenye mbao za matangazo, kabla ya kurudishwa baraza na baadaye kwa waziri mkuu.MAELEZO YA PICHA:WAFANYABIASHARA soko la kuku mjini Singida,huku wakinyanyua kuku waliokufa kwa kukosa hewa, baada ya lori la Fuso walilokodi kushikiliwa manispaa kwa saa 24, wakidai ushuru wa Sh.300 kwa kuku mmoja, badala ya Sh.1,000 kwa tenga moja la kuku 80.

Jamii Ya Wafugaji Na Wahadzabe Iramba mkoani Singida Wajitokeza Kwenye Chanjo

Mama wa jamii ya wafugaji wa eneo hilo akiwa na watoto wake watano, huku mmojawapo akipatiwa dawa ya minyoo.

Bibi wa jamii ya wafugaji wilayani Iramba, akiwa na mjukuu wake alipompeleka kwenye chanjo, na kupatiwa matone ya vitamini A,katika zoezi la chanjo kitaifa lililomalizika Novemba 16,mwaka huu.

JAMII ya Wahadzabe katika kitongoji cha Kipamba,wilaya Iramba,mkoa wa Singida, wamejitokeza kushiriki chanjo ya surua,polio,vitamin A na dawa za minyoo.
Hali hiyo ni tofauti ikilinganishwa na miaka ya nyuma, ambapo walikuwa wakikimbilia porini kila zoezi hilo lilipokuwa likifanyika.
Katika zoezi hilo lililokamilika novemba 16,mwaka huu nchini pote, watoto 86 wa jamii hiyo na wafugaji wanaoishi kwenye kitongoji hicho walikuwa wamechanjwa.
Kitongoji hicho kipo upande wa mkoa wa Singida, mpakani na mikoa mingine ya Manyara na Arusha, na huduma hiyo ilitolewa na timu ya wataalamu wa afya,kutoka hospitali ya wilaya ya Iramba.
Mganga mkuu wa wilaya ya Iramba Dk.Doroth Kijugu, alisema mafanikio hayo, yametokana na ushirikiano baina ya pande hizo mbili, ambapo sasa jamii hiyo imeanza kujenga imani kuhusiana na tiba za kisasa.
Aidha Dk.Kijugu aliahidi kuwa idara ya afya wilayani humo, itaendelea kuwa karibu zaidi na jamii hiyo, kwa kuhakikisha wanapata tiba sahihi, ili kuwaepusha na matumizi ya dawa walizozizoea, za mizizi na magamba ya miti.