Saturday, December 3, 2011

Sakata La Wafanyabia​shara Wa Kuku Singida

Wauza kuku wakichukua mizoga kutoka kwenye mfereji.

Wauza kuku wakionysha kuku waliokufa kwa joto kali.

Wauza kuku Singida wakishuhudia kuku waliokufa kwa joto kali.

WAFANYABIASHARA wa kuku mjini Singida wamelalamikia mkurugenzi wa manispaa kwa madai kuwa amesababisha maelfu ya kuku kufa,wakati akidai ushuru, wakati alipolishikilia lori lililopakia kuku kwenda jijini Dar es Salaam, kwa saa 24.
Akiongea na waandishi wa habari eneo la soko kuu jana, mkurugenzi wa wauza kuku mjini Singida, Selemani Mohammed Kuku alisema, kutokana na hasara kubwa waliyoipata,wanatarajia kuipandisha kizimbani manispaa hiyo, ili awalipe fidia.
Kwa mujibu wa Kuku, wafanyabiashara katika soko hilo wamepata hasara ya maelfu ya fedha, kutokana na kuku zaidi ya 2,000 kufa, kwa kukosa hewa, baada ya lori walilokodi kushikiliwa na manispaa, kwa zaidi ya saa 24.
Kuku ambaye pia mwenyekiti wa mtaa wa Majengo mjini hapa kwa tiketi ya CCM, alidai busara ndogo ingetumika kudai fedha za ushuru,zingeokoa kiasi kikubwa cha fedha za wajasiriamali hao, ambazo zimepotea bila sababu ya msingi.
“Sikilizeni ndugu waandishi,nina miaka zaidi ya 40 nikifanya biashara hii ya kuku, lakini utaratibu uliotumika kushikilia lori siyo sahihi….kuku akipakiwa jioni, gari linakimbia kasi ili kupata hewa ya kutosha na hadi alfajiri liwe sokoni,Dar es Salaam….,”alisema kwa masikitiko Kuku.
Alisema tayari mwanasheria wao ambaye hakutaka kumtaja jina, anakamilisha taratibu za kisheria,ili mkurugenzi alazimishwe kuwalipa stahili zao.
Waandishi wa habari waliotembelea eneo la soko la kuku mjini Singida walijionea maelfu ya mizoga ya kuku, ikiwa imerundikwa pamoja, huku baadhi ya wafanyabiashara wakiwa na huzuni na kujawa na hasira kali, hata baadhi yao kuthubutu kutoa lugha chafu juu ya kitendo hicho na wengine wakiomba kupewa kadi mpya, toka vyama vya siasa.
Hata hivyo baadhi ya askari polisi walioongea na NIPASHE kwa sharti la kutotajwa majina, walilaumu kitendo cha uongozi wa manispaa kutumia jeshi la polisi kudhibiti vurugu, badala ya kutumia askari wake wao, waliowaajiri.
Jumatano wiki hii, katika vurugu hizo,ambazo zilizotokana na lori lililopakia kuku,kushikiliwa na manispaa,baada ya askari wa usalama barabarani kulizuia lori la Fuso namba T. 125 BES likiwa njiani kwenda Dar es Salaam, askari mmoja alichaniwa sare ya shati na kusababisha wafanyabiashara kumi, kutiwa nguvuni na polisi.
Uongozi wa Manispaa ulikuwa unadai ada ya ushuru mpya wa kuku mmoja kwa Sh.300, sawa na Sh.30,000,kwa tenga moja lenye uwezo wa kubeba kuku 30, badala ya ule wa zamani wa Sh.1,000.
Kwa upande wake, kaimu mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Salome Singano, alisema, ada hizo mpya zimetokana na maamuzi ya baraza la madiwani la aprili,mwaka huu,iliyosainiwa na waziri mkuu, kabla ya kutangazwa katika gazeti la serikali,Oktoba7,2011. Alisema, mchakato wa sheria hiyo inayojulikana kama ’Sheria ndogo ya halmashauri ya manispaa ya Singida, ada na ushuru 2011’, ilipelekwa kwanza kwa wananchi na kubandikwa kwenye mbao za matangazo, kabla ya kurudishwa baraza na baadaye kwa waziri mkuu.MAELEZO YA PICHA:WAFANYABIASHARA soko la kuku mjini Singida,huku wakinyanyua kuku waliokufa kwa kukosa hewa, baada ya lori la Fuso walilokodi kushikiliwa manispaa kwa saa 24, wakidai ushuru wa Sh.300 kwa kuku mmoja, badala ya Sh.1,000 kwa tenga moja la kuku 80.

No comments:

Post a Comment