Wednesday, October 7, 2015

Nitaondoa njaa, wakulima watatumia helkopta kumwagilia mashamba, nitajenga vituo maalumu vya Albino na wazee – Rungwe

Mgombea Urais wa CHAUMA,Hashim Rungwe katika pozi tofauti akihutubia wananchi wa Singida mjini jana.
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha ukombozi wa Umma (CHAUMA) Hashim Rungwe akizungumza kwenye Mkutano wa Kampeni Mkoani  Singida, ambapo aliahidi kuwaondolea wananchi njaa.
Mgombea mwenza wa CHAUMA Issa Abas Husein nae akihutubia wananchi wa Singida mjini.
WANANCHI wakimsikiliza Mgombea Urais wa CHAUMA kwenye kituo cha stendi ya zamani Mjini Singida jana.

 Mgombea Urais Rungwe akihutubia kwa staili mbalimbali.
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA) Hashim Rungwe akizungumza na waandishi wa habari juu ya hali ya kampeni ilivyo hadi hadi sasa.

MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA) Hashim Rungwe, amesema akichaguliwa kuwa Rais atajenga vituo maalumu vya walemavu wa ngozi Albino pamoja na wazee ili waishi kwa amani na utulivu.

Rungwe aliyasema hayo jana wakati akizungumza kwenye mkutano wa kampeni  wa chama chake uliofanyika kituo cha zamani cha mabasi, Mjini Singida.

Alisema lengo la kutengeneza vituo hivyo ni kutokana na walemavu hao kuandamwa kila mara na watu wasiowatakia mema na kuwavizia kila kona ili waweze kuwakata viungo vyao kutokana na imani potofu.

“ Hawa mimi nitawajengea vituo maalum na watakaa huko kwa maisha yao ikiwa ni pamoja na kuwapatia elimu bora ili na wao wajione kuwa wako katika nchi ya amani na utulivu, pia wazee tutawatunza kwa kufanya kazi sisi,wako wasiojiweza nao pia nitafanya hivyo hivyo, sawa jamani. “ Alisema Rugwe na kuamsha nderemo na vifijo.

Aidha alisema mbali na kujenga vituo hivyo pia serikali atakayounda haitakuwa na msururu wa mawaziri kwani kufanya hivyo ni kuwanyima watu wengine fursa za uongozi ndani ya nchi hii.

Pia alisema endapo atachaguliwa kuwa Rais atahakikisha kuwa magari yatakayotumika kwa viongozi ni yale aina ya Landrover Defender ambayo gharama zake sio kubwa kama ilivyo kwa mashangingi ambayo yanauzwa bei ghali wakati wananchi wanataabika na njaa.

“  Njaa ni mbaya jamani , kila kona ni njaa tu, hii kitu kwangu haitakuwepo kila mtu afanye kazi sio kulia lia njaa, njaa, njaa wakati nguvu tunazo za kuweza kufanya kazi, kila mtu afanye kazi.”Alisisitiza Rungwe huku akishangiliwa kutokana na staili yake ya kuhutubia kwa mbwembwe.

Katika hatua nyingine Mgombea huyo alisema Serikali yake itanunua ndege aina ya helpkopta kwa ajili ya kumwagilia mashamba ya wakulima mara tatu kwa wiki lengo ni kuhakikisha uzalishaji wa mazao ya chakula unapatikana wakati wote bila kutegemea mvua.

“Hili linawezekana tuna maziwa na mito mingi hivyo hakuna sababu ya wakulima kutegemea mvua, ndege zitafanya kazi ya kumwagilia mashamba yenu, na hili ni jambo linalowezekana, nimetembea nchi nyingi za Saudi Arabia na kiarabu zinatumia utaratibu huu.” Alisema Rungwe na kushangiliwa.

Aidha alisema ni wakati sasa wa CCM kupumzishwa kwani hawana jipya na kuwa wamechoka na sera zilezile kuwa watawaletea maendeleo kwani miaka 50 sasa bado Watanzania wana hali mbaya na kila kona utasikia njaa mbaya njaa mbaya.


“Tuwapumzishe hawa wamechoka , wanatuita malofa na wapumbavu sasa ni wakati wa malofa na wapumbavu kuongoza nchi hii, uwezo wao wa kuongoza ni mdogo, betri hazina chaji wapuuzeni hawa, mimi betri ina chaji imejaa full, nipeni miaka mitano muone kazi yangu.” Alisema.

No comments:

Post a Comment