Kaimu Katibu Tawala wa mkoa wa Singida, Aziza Mumba akikata utepe kuzindua nyota mpya ya kijani.
Baadhi ya wananchi wa kata ya Mang’onyi wakiwa kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mkuu kumnadi mgombea wa ubunge wa jimbo hilo.
ZAIDI ya wakazi 5,000 wa Kijiji cha Sambaru,kata ya Mang’onyi,wilaya ya Ikungi,Mkoani Singida wamo hatarini kupatwa na magonjwa ya mlipuko kutokana na kujisaidia vichakani kwa kutokuwa na vyoo vya kudumu kutokana na idadi kubwa ya wahamiaji wanaoishi kwenye vitongoji saba vilivyopo katika Kijiji hicho.
Ofisa mtendaji wa Kijiji cha Sambaru,Bwana Baraka Njiku amesema wakazi hao wapo kwenye hatari ya kukumbwa na magonjwa ya kuharisha,kuhara damu pamoja na kipindupindu kutokana na kula uchafu wa kinyesi wanachojisaidia kwenye vichaka vilivyopo karibu na nyumba zao za makazi.
Aidha ofisa mtendaji huyo amefafanua kwamba wakazi hao wapatao 5,870 wanaoishi katika kaya 899 wanahitaji matundu 899,lakini matundu ya vyoo vya muda yaliyopo ni 320 kati ya mahitaji wa wakazi wote wa Kijiji hicho.
Kwa mujibu wa Bwana Njiku katika Kitongoji cha Taru namba saba chenye kaya 99 kinahitaji jumla ya matundu ya vyoo 498 yaliyopo kwa sasa ni matundu ya muda
sitini hali inayochangia idadi kubwa ya wakazi wake kuendelea kwenda kujisaidia kwenye vichaka vilivyopo karibu na makazi wanayoishi.
Bwana Njiku ameyasema hayo kwenye mahojiano maalumu na gazeti hili lililotaka kufahamu hali halisi ya matundu ya vyoo vya kudumu yanayohitajika na yaliyopo kwa sasa kwa lengo la kukabiliana na magonjwa mbalimbali ya milipuko.
Aidha amefafanua kwamba idadi kubwa ya wakazi wa Kijiji hicho wamelazimika kuendelea kujisaidia vichakani kunatokana na wengi wao kuwa wahamiaji kutoka katika mikoa mbalimbali wanaohamia huko kwa lengo la kufuata malisho ya mifugo pamoja na mashamba.
Kuhusu hatua zilizochukuliwa na zinazotarajiwa kuchukuliwa
na ofisi yake,ofisa mtendaji huyo wa Kijiji ameweka bayana kwamba wametoa muda wa wiki mbili kwa kila mkazi asiyekuwa na choo kuhakikisha amechimba choo cha kudumu na kuanza kukitumia na kuonya kwamba kwa yeyote ambaye hatatekeleza agizo hilo atatozwa adhabu ya faini ya shilingi elfu kumi.
Hata hivyo alipotakiwa kufafanua sababu za wananchi wa kata hiyo kutokuwa na vyoo vya kudumu,Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi,Bwana Mohamedi Nkya alisema tatizo hilo linachangiwa na upungufu mkubwa wa wataalamu wa idara ya afya uliopo katika Halmashauri hiyo.
Kwa mujibu wa Bwana Nkya licha ya kuomba na kupatiwa kibali cha ajira za wataalamu wa afya,lakini hakuna waombaji waliojitokeza kuomba nafasi hizo ili kuziba pengo la upungufu mkubwa wa wataalamu uliopo katika Halmashauri hiyo watakaokuwa na majukumu ya kusimamia usafi wa mazingira katika kata zao.
No comments:
Post a Comment