Wednesday, November 18, 2015

Mkoa wa Singida mwenyeji maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani, Desemba Mosi mwaka huu.

Mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko Vicent Kone,jana akitoa taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) juu ya kufanyika kwa maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani kitaifa mkoani Singida.
Baadhi ya waandishi wa habari mkoani Singida,wakiwa kwenye harakati za kupata picha bora ya mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko Vicent Kone (hayupo kwenye picha) jana.Mkuu huyo wa mkoa,alikuwa akitoa taarifa ya kufanyika kwa maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani itakayofanyika kitaifa mkoani Singida.

Rais mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani, ambayo kitaifa inatarajiwa kufanyika mkoani hapa  Desemba mosi mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisni kwake jana,mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko Kone,alisema maadhimisho hayo yanatarajiwa kuanza novemba 24 mwaka huu kwenye viwanja vya peoples mjini hapa, na yatazinduliwa rasmi  novemba 25.

Alisema katika wiki ya maadhimisho hayo,wadau mbalimbali watapata fursa ya
kuonyesha shughuli  wanazofanya kuhusiana na mapambano dhidi ya UKIMWI,na wananchi pia watapata fursa ya elimu dhidi ya UKIMWI na upimaji wa VVU.

“Ikumbukwe kuwa katika juma la maadhimisho hadi siku ya kilele,tunategemea kuwa na wageni mbalimbali wa kitaifa na kimataifa watakaojumuika nasi katika maadhimisho hayo.Lengo lokiwa ni   kuona shughuli na huduma mbalimbali zinazohusu masuala ya UKIMWI”,alisema.

Mkuu huyo wa mkoa,alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wakazi wa mkoa huu na wadau wote wa maendeleo,kujitokeza kwa wingi na kushiriki kwa dhati katika kufanikisha maadhimisho na kilele cha siku ya UKIMWI duniani,ambayo kitaifa yataadhimishwa viwanja vya peoples mjini Singida.

Aidha,aliwaomba  waandishi wa habari,kuusaidia mkoa kwa kusambaza ujumbe huu zaidi,ili uwafikie wananchi wengi zaidi.Vile vile amesisitiza pia wananchi wa  mkoa wa Singida,kujitokeza  kwa wingi katika maadhimisho hayo.


Dk.Kone,alisema; “Singida bila maambukizi mapya ya UKIMWI,Bila vifo vitokanavyo na UKIMWI na bila Unyanyapaa na Ubaguzi,Inawezekana” kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake”.

No comments:

Post a Comment