Thursday, January 30, 2014

SIDO Singida yawataka wajasiriamali kutumia mikopo kuimarisha ndoa zao.

Meneja wa SIDO mkoa wa Singida, Shoma Kibende akitoa nasaha zake muda mfupi kabla hajatoa mikopo yenye thamani ya shilingi 18.9 kwa wajasiriamali wa kikundi cha Urafiki cha mjini Singida.Kulia (aliyekaa) ni katibu wa kikundi cha urafiki,Remiji Alex.
 Meneja wa SIDO mkoa wa Singida,Shoma Kibenda,akimkabidhi Remji Alex mkopo wa shilingi 500,000.
Meneja mikopo wa SIDO mkoa wa Singida, Ruben Mwanja akitoa mafunzo kwa wajasiriamali muda mfupi kabla ya kukabidhi mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi 18.9 milioni kwa kikundi cha urafiki cha mjini Singida.
Meneja mikopo wa SIDO mkoa wa Singida, Ruben Mwanja (wa kwanza kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na wanakikundi cha wajasiriamali cha Urafiki cha mjini Singida.Kikundi hicho kilikopeshwa zaidi ya shilingi 18.9 milioni na watarudisha na fidia ya shilingi 1.8 kwa mwezi.

MENEJA mikopo wa shirika la kuhudumia viwanda vidogo (SIDO) mkoa wa Singida,Ruben Mwanja,amewataka wajasiriamali kutumia mikopo yao vizuri na kwa malengo yaliyokusudiwa,na pia mikopo hiyo isaidie kuimarisha ndoa zao.

Mwanja aliyasema hayo wakati akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi mikopo mbalimbali yenye thamani ya shilingi 18,9 milioni kwa wanachama 39 wa kikundi cha Urafiki cha Singida mjini.

Amesema uzoefu unaonyesha wazi kwamba baadhi ya wanawake wanaobahatika kupata mikopo,hukorofishanana au kutengana kabisa wanaume wao.

“Pia wapo baadhi ya wanaume wakishapata mkopo wa kuendeleza biashara yao,hukimbilia kuoa mke mwingine”,amesema Mwanja na kuongeza;

“Nawasihi sana,mikopo ya SIDO isitumike kuongeza wake wengine au kuvunja ndoa za watu,itumike tu kuendeleza biashara ya mkopaji ili kupanua/kuongeza kipato cha mhusika”.

Kwa upande wake meneja wa SIDO mkoa wa Singida,Shoma Kibenda,alikipongeza kikundi cha Urafiki kwa madai kwamba kina utamaduni mzuri wa kurudisha mikopo kwa wakati na bila matatizo.

Kibenda aliwataka wapige hatua zaidi kwa kuangalia uwezekano wa kuanzisha viwanda vidogo kama njia moja wapo ya kujiongezea kipato zaidi.


Mikopo iliyotolewa juzi,kima cha chini kilikuwa shilingi
300,000 na cha juu,kilikuwa ni shilingi 500,000 kwa mwanachama mmoja mmoja.Riba ya mikopo hiyo ni asilimia 1.8 kwa mwezi.

No comments:

Post a Comment