Friday, November 25, 2011

Waandishi Wa Habari Singida Wapata Uongozi Mpya

Mwakilishi wa umuoja wa klabu za waandishi wa habari nchini(UTPC), Bw.Victor Maleko kutoka Mwanza akitoa nasaha kwa uongozi mpya.

Waandishi wa habari mkoa Singida wakiwa mkutanoni, tayari kushiriki uchaguzi kupata viongozi wapya.

Mwenyekiti mpya wa SINGPRESS(aliyesimama), Seif Takaza, akiwa na timu mpya iliyochaguliwa kuongoza klabu hiyo kwa miaka mitatu ijayo, mwenye kofia ni katibu wa chama hicho Bw. Abby Nkunu.

Aliyekuwa katibu wa SINGPRESS, Bi. Doris Meghji, akisoma risala kwa mgeni rasmi, mkuu wa mkoa Singida(mbele), Dk.Parseko Kone,kabla ya uchaguzi kuanza.

Viongozi wapya wa Chama Cha Wanahabari mkoa Singida(SINGPRESS), wakiwa katika picha ya pamoja baada ya uchaguzi jana, kutoka kulia mbele ni Nathaniel Limu, Joseph Lujuo, Awila Sila, Jumbe Ismailly na Elisante John; nyuma kutoka kushoto ni Emmanuel Michael, Abby Nkungu, Seif Takaza na Mchungaji Immanuel Barnaba.


MKUTANO mkuu wa Chama Cha Waandishi wa habari mkoa wa Singida(SINGPRESS), umepata viongozi wapya, watakaodumu madarakani kwa kipindi cha miaka mitatu, kulingana na katiba yao.
Waliochaguliwa na mkutano huo uliofanyika ukumbi wa kanisa katoliki mjini Singida na nyadhifa zao kwenye mabano ni Seif Takaza(mwenyekiti), Abby Nkungu(katibu) na Awila Sila(mhazini).
Wengine ni Jumbe Ismailly(mwenyekiti msaidizi), Emmanuel Michael(katibu msaidizi), Nathaniel Lim(mhazini msaidizi), na wajumbe watatu wa kamati ya utendaji ambao ni Elisante John,mchungaji Immanuel Barnaba na Joseph Lujuo.
Mapema akifungua mkutano huo, mkuu wa mkoa Singida Dk.Parseko Kone alipongeza hatua iliyochukuliwa na SINGPRESS, katika kuandaa uchaguzi huo, akidai kuwa waandishi wa Singida wameonyesha mfano halisi wa Demokrasia.
Hata hivyo aliwataka kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ukweli na ufanisi, pasipo kumuonea mtu au mdau yeyote katika utoaji wa taarifa.
Alikemea tabia ya waandishi wachache wanaochafua taaluma ya habari kwa kuandika habari zenye mlengo wa kukosanisha jamii na viongozi wanaowangoza.
Katika uchaguzi huo, ulisimamiwa na mwakilishi kutoka Muugano wa klabu za waandishi wa habari Tanzania(UTPC) Victor Maleko, na katibu tawala msaidizi mkoa Singida anayeshughulikia masuala ya maendeleo ya jamii, Zuhura Karya.

Thursday, November 17, 2011

Ziara Ya Mo Dewji Kwenye Mradi Wa BADEA


Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji safi na taka Singida,SUWASA, Marin Churi akifafanua jambo kwa ugeni ulioambatana na Mbunge wa Singida Mjini ,Mohammed Dewj (kuhoto) pamoja na wengine walioambatana kwenye msafara huo wakiwemo viongozi wa siasa.

Mbunge wa Singida Mjini,Mohammed Dewji akisalimiana na watendaji wakuu wanaosimamia mradi huo wa BADEA, Mr. Ragpathy (Contracts Manager) pembeni yake,Ashork Patel (Site Incharge) wa kampuni ya SPENCON SERVICE LTD.

Tanki la maji likiwa kwenye hatua ya ujenzi likionekana kwa sasa ambapo ujenzi wake unatarajia kumalizika mwakani, ambapo mradi huo utakuwa na matumaini makubwa kwa wananchi wa Singida ukikamilika.

Mo Dewji akipata maelezo ya sehemu mbalimbali ndani ya eneo la Ujenzi la mradi wa Tanki kubwa na lala kisasa kutoka kwa mmoja wa wataalum wa kampuni ya Spencon Service Ltd alipotembelea huko eneo la Mandewa.

Mkurugenzi wa SUWASA,Injinia Isaack Nyalonji Akitoa maelezo ya kisima kikubwa cha mradi wa BADEA katika eneo la Mwankoko, kushoto kwake Mbunge Mo Dewji alipotembelea kukagua mradi huo ambao unatarajia kumalizika mpaka Julai 12, mwakani. Wa pili kushoto, Mstahiki Meya, Shehe Salum Mahami, eneo la chanzo cha mradi huo wa maji.

Mo Dewji akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi mbalimbali mara baada ya kumaliza kukagua ujenzi wa mradi huo wa BADEA ambao unatarajia kumalizika Julai mwakani.

Wachimbaji W adogo Wapinga Kuondolewa Machimboni Singida


Katibu wa machimbo ya Taru Cavin Kamtwela, akilalamika kwa waandishi wa habari katika mkutano huo, jinsi wanavyotakiwa kumpisha mwekezaji.

Dhahabu ikiandaliwa

Wachimbaji wadogo wakikusanyika kwenye eneo la machimbo ya dhahabu, katika kijiji cha Taru, wilayani Singida.

Hii ni Guest house ya eneo hilo la machimbo

Wachimbaji wa dhahabu wakionyesha mawe yenye dhahabu, ambayo yametokana na kulipuliwa na baruti chini ya ardhi.

Mmoja wa wachimbaji wadogo akilalamika juu ya vitendo wanavyofanyiwa na serikali kwa kushirikiana na Shanta Mining, ili waondoke eneo hilo.

Wachimbaji hawa hupata mlo wao kwa kina mama kama hawa, waliopo katika maeneo hayo ya mgodi nao wakijitafutia riziki yao

WACHIMBAJI wadogo wa dhahabu katika vijiji vya Taru na Sambaru, wilayani Singida, wamepinga kuondolewa kwa nguvu kwenye eneo lao, ili kumpisha mwekezaji wa madini, kutoka nje ya nchi, kampuni ya Shanta Mining Ltd.
Walitoa msimamo huo juzi, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye machimbo hayo katika kijiji cha Taru, kujadili eneo lao wanalotaka kuporwa ili kuipisha kampuni hiyo,kufungua mgodi mkubwa wa dhahabu.
Walieleza kusikitishwa na hatua ya serikali kumkumbatia mwekezaji huyo, badala ya wachimbaji wadogo kumilikishwa wao eneo hilo, ili wapatiwe vibali halali, kwa ajili ya kuendesha kazi zao kisheria.
Wakizungumza katika mkutano huo, mwenyekiti wa kitongoji cha Taru Emmanuel Sawa,katibu wa wachimbaji hao Cavin Kamtwela na mchimbaji Said Hamad Sabodo,walidai kuvumbua eneo hilo, baada ya kutolewa kwa nguvu eneo linguine, ambalo pia walielezwa kumpisha Shanta.
Kutokana na mgogoro huo, wameomba msaada kutoka kwa mashirika, asasi za kiraia, watu na wanaharakati wanaojishughulisha na utetezi wa haki za binadamu, kwenda ili kujionea hali halisi na baadaye wasaidie katika mapambano hayo.
Kamishina msaidizi wa madini kanda ya kati ambayo ofisi zake zipo mkoani Singida, Manase Mbasha alisema kuwa, wachimbaji hao wakiondoka kwenye eneo hilo, watapatiwa lingine, baada ya kumpisha mwekezaji huyo.
Afisa madini huyo alifafanua kuwa, eneo linalotarajiwa kutumika kwa ajili ya kufungua mgodi, linajumuisha vijiji vya, Sambaru, Taru na Samumba, katika halmashauri ya wilaya ya Singida.
Kwa mujibu wa Mbasha, mwekezaji huyo ameomba leseni tatu kwa ajili ya kufungua mgodi, na tayari amemaliza shughuli za utafiti tangu oktoba mwaka huu, kazi aliyoianza mwaka 2003.

Tuesday, November 8, 2011

Kituo Cha Mafuta Chauza Maji Badala Ya Petrol Singida

Mhusika wa gari hilo akihangaikia, baada ya kuwa limejazwa maji badala ya petrol, kwenye kituo cha Gapco mjini Singida, ambacho ni mali ya M/S Joel Traders wa Dar es Salaam

Rav 4 ikisaidiwa kupelekwa gereji

Magari mawili yakiwa katika eneo la kituo cha Gapco mjini Singida,baada ya kushindwa kufanya kazi kufuatia kujazwa maji,badala ya mafuta ya Petrol.

Fundi magari, akionekana kulifanyia matengenezo gari ilililojazwa maji badala ya petrol, matengenezo hayo yalihusu kubadilisha pampu na tenki la mafuta.

Meneja akinyanyua pampu, kwa madai kuwa iligongwa na gari, hivyo kusababisha maji kuingia, wakati huohuo akidai hitilafu ya umeme imesababisha maji kuingia,ajabu!.

KITUO cha mafuta cha GAPCO, mjini Singida kimewajazia maji wateja wake kwenye magari,badala ya petrol.
Tukio hilo limetokea jana jumatatu,ikiwa ni siku moja tabngu Mamlaka ya udhibiti wa Nishati na Maji(Ewura) kutangaza kupanda bei ya mafuta aina zote.
Hali hiyo imesababisha injini za magari hayo kuzima, kila mojawapo lilipojazwa maji badala ya mafuta, majira ya saa tatu asubuhi,kwenye kituo hicho, kilichopo eneo la Boma, jirani na ofisi za TRA,Singida.
Baadhi ya wateja walioathirika,Thomas Petro na Elisante Mkumbo, walishangazwa na kituo hicho,baada ya kubaini kiwango cha mafuta kwenye magari yao ni kidogo,kuliko mafuta.
Walidai, magari yao mawili, ni kati ya manne yaliyojazwa mafuta, kabla ya zoezi hilo kusitishwa na uongozi wa kituo hicho cha GAPCO, baada ya magari hayo kuzima,kila yalipokuwa yamejazwa mafuta.
Magari mengine, yaliyojazwa petrol kwenye kituo hicho yalibainika kuwa na maji hadi lita 20.
Hata hivyo wakati jeshi la polisi, kupitia kamanda wa mkoa,Celina Kaluba, likisema halifahamu chochote juu ya tukio hilo,meneja wa kituo cha Gapco, Kiwelu Amos, alisema maji hayo yametokana na mvua iliyonyesha.
Maelezo ya meneja huyo yalionekana kutofautiana kila alipoeleza, awali alidai athari hiyo ilitokana na maji ya mvua, na baadaye akasema imesababishwa na tatizo la umeme,lakini bila ya kufafanua zaidi.
Kituo hicho kinamilikiwa na M/S Joel Traders Ltd-Singida, anayeishi Dar es Salaam, na hii ni mara ya pili kufungiwa, awali kiliwahi kufungiwa baada ya kukiuka utaratibu wa kuweka rangi, kwenye mafuta yake.

Wednesday, November 2, 2011

DC Mabiti Aamuru Wachimbaji Dhahabu Waondoke

Mkuu wa wilaya Singida Paschal Mabiti akizungumza na wachimbaji wadogowadogo wa dhahabu kijiji cha Sambaru wilayani humo, ambapo aliwapa siku tatu hadi ijumaa wiki hii kuhakikisha wameondoka kwenye eneo hilo ili kumpisha mwekezaji kampuni ya Shanta

Mchimbaji George Stiven,kwa niaba ya wenzake akiomba waongezewe muda ili waondoke kwenye eneo hilo kama ilivyoamuliwa na serikali kwa ajili ya kumpisha mwekezaji anayetarajia kufungua mgodi,baada ya kukamilisha kazi ya kutafiti madini ya dhahabu.

Baadhi ya askari kikosi cha kutuliza ghasia waliofuatana na mkuu wa wilaya ya Singida Paschal Mabiti, wakiwa kwenye eneo la mkutano, tayari kudhibiti lolote linaloweza kuhatarisha uvunjifu wa amani


Singida
Novemba 01,2011
MKUU wa wilaya Singida Paschal mabiti ametoa siku kwa wachimbaji wadogo wanaofanya kazi zao kwenye kijiji cha Sambaru, kuondoka, haraka, bada ya hapo watakumbana na nguvu ya dola.
Mabiti amesema eneo hilo linalotoa madini ya dhahabu ni halali kwa mgodi wa kampuni ya Shanta, iliyotafiti na kupata kibali kwa kazi hiyo.
Alitoa karipio hilo juzi jumatatu, wakati akizungumza na wachimbaji hao katika viwanja vya kambi namba moja, kijijini Sambaru.
Alisema Shanta inayo leseni halali ya kutafiti na kuchimba dhahabu katika maeneo hayo, na amekamilisha maandalizi yote muhimu kwa ajili ya kuanza kazi ya mgodi.
“Tumezungumza sana na ninyi,tena mara nyingi sana na mazungumuzo hayo, nimekuwa nawaeleza kuwa, Shanta amewapa ruhusa kuchimba madini katika eneo hili kwa muda tu, Sasa muda huo umekwisha, mnatakiwa kuondoka kwa hiari yenu,”alisema.
Baadhi ya wachimbaji waliomba kuongezewa muda ili wahame eneohilo.
Huku wengine wakisema wazi hawapo tayari kuona wanaporwa maeneo yao, hivyo wameiomba serikali kuingilia kati malalamiko yao waliyodai sasa ni ya muda mrefu.
Walitoa tahadhari kupatikana suluhu, ili yaliyotokea mkoani Mara na Shinyanga yasijirudie mkoani Singida.

Madiwani Wa CCM Wamlalamik​ia Meya Wao

Diwani wa kata Mungumaji Hassan Mkata akiongea kwenye baraza la madiwani, Manispaa ya Singida, kuhusiana na maamuzi mbalimbali yanayoafikiwa na baraza hilo, lakini hayatekelezwi

Diwani wa kata ya Utemini Bartazar Kimario akiongea kwa hisia kali katika baraza hilo, kulalamikia maamuzi mbalimbali yanayotolewa na baraza hilo, lakini hayatekelewi hali aliyotishia kutoka kwenye kikao hicho.hata hivyo alibaki baada ya mawazo yake kukubaika

Madiwani wakifuatilia hoja kupitia katika makablasha yao

.:Meya wa manispaa Singida Shekhe Salum Mahami akifungua baraza hilo, kulia ni mkurugenzi wa mniapsaa Yona Maki

MADIWANI wa manispaa ya Singida wamemlalamikia Meya shekhe Salumu Mahami, wakidai hayatendea haki maamuzi ya baraza hilo na hiyo inaweza klutoa nafasi kwa wapinzani, siku za usoni.

Baadhi ya madiwani waliotoa shutuma hizo ni Hassan Mkata (Mungumaji), Shaaban Sattu(Unyambwa), Baltazar Kimario(Utemini) na Moses Ikaku(Unyamikumbi).
“Meya lazima sasa tusome nyakati, umekuwa kama kinyonga, unabadilika badilika rangi kutokana na eneo unalokuwa….mnaifichaficha nini, mkurugenzi naye tunaweza kumtoa nje ili tumjadili, tukiona amekosea tutaamua hapa hapa,”alisisitiza Mkata.
Baraza la madiwani, manispaa ya Singida lina jumla wajumbe 21, wote kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) pekee, wakiwemo wawakilishi kata 14, viti maalumu watano na wabunge wawili.