Friday, January 2, 2015

11,380 Singida, wachaguliwa kujiunga kidato cha kwanza

Katibu tawala mkoa wa Singida, Liana Hassan, akizungumza kwenye kikao cha mkoa cha kupangia shule wanafunzi waliofaulu mtihani wa taifa wa kumaliza elimu ya msingi mwaka huu,ili kuanza kidato cha kwanza mwakani.Wa kwanza kulia ni katibu tawala msaidizi kwa upande wa sekta ya elimu sekretarieti ya Mkoa,Fatuma Kilimia na kushoto ni mkuu wa wilaya ya Singida,Queen Mlozi.
Mbunge wa viti maalum mkoa wa Singida, Christowaja Mtinda, akizungumza kwenye kikao cha mkoa cha kupangia shule wanafunzi waliofaulu mtihani wa taifa wa kumaliza elimu ya msingi mwaka huu, ili kuanza kidato cha kwanza mwakani.

Baadhi ya wajumbe wa kikao cha mkoa cha kupangia shule wanafunzi waliofaulu mtihani wa taifa wa kumaliza elimu ya msingi mwaka huu,ili kuanza kidato cha kwanza mwakani.Kikao hicho kilifanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa kanisa katoliki mjini Singida.

JUMLA ya wanafunzi 11,380 mkoani Singida, wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani, kati ya 23,734 waliofanya mtihani wa kitaifa wa kumaliza elimu ya msingi mwaka huu.

Kati ya wanafunzi hao 11,380 waliofaulu mtihani huo,wasichana ni 5,954 na wavulana ni 5,426.Kwa upande wa waliofanya mtihani huo 23,734  wa kitaifa,wavulana ni 10,694 na wasichana ni 13,040.

Aidha, wanafunzi waliopata nafasi za shule za bweni ni,99,wavulana ni 64 na wasichana ni 35,wakati waliopata nafasi katika shule za kata (za kutwa) ni 11,217,wavulana 5,362 na wasichana ni 5,919.

Hayo yamesemwa  na Katibu tawala msaidizi elimu sekretarieti ya mkoa wa Singida, Fatuma Kilimia, wakati akitoa taarifa ya uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza mwakani.


Alisema ufaulu wa mwaka huu ni sawa na aslimia 48 ambao umepanda kwa asilimia 7 ukilinganisha na aslimia 41 kwa mwaka jana (2013).

Kilimia alisema manispaa ya Singida imeendelea kuongoza kwa ufaulu mzuri ambapo kwa mwaka huu,aslimia ya ufaulu ni 65.3,ikifuatiwa kwa karibu na halmashauri ya Singida vijijini yenye aslimia 62.8.

“Halmashauri ya Ikungi ni ya tatu yenye aslimia 53.5,Manyoni ya nne kwa aslimia 50,Iramba aslimia 42.3 na ya mwisho ni halmashauri ya wilaya ya Mkalama yenye ufaulu wa aslimia 25 tu”,alisema afisa huyo.


Alisema halmashauri tano ufaulu wake umepanda,isipokuwa tatizo bado lipo katika halmashauri ya Mkalama tu ambayo ufaulu wake ni aslimia 25 wakati mkoa umejiwekea lengo la ufaulu ni asilimia 85.

 Kilimia alitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta ya elimu kuwa ni shule nyingi kutokukaguliwa kwa muda mrefu na baadhi ya wanafunzi kutokujua kusoma,kuandika na kuhesabu.

Alitaja changamoto zingine kuwa ni utoro mkubwa wa wanafunzi,utoro wa reja reja wa walimu na baadhi ya walimu wapya kutokumudu ufundishaji wa masomo hasa Hisabati na Kiingereza.


Pia Kilimia alitaja baadhi ya mikakati ya kuinua taaluma kuwa ni pamoja na kuendesha mafunzo ngazi ya klasta na kata kwa masomo yenye utata,kubaini walimu wa wakuu wasiowajibika ipasavyo na kuwavua madaraka na kusikiliza na kutatua kero za walimu.

No comments:

Post a Comment