Tuesday, January 13, 2015

Askofu mstaafu Singida ataka jamii kuepuka vishawishi.

 Kanisa la Pentekoste (FPCT) la mjini Singida.
ASKOFU mstaafu wa kanisa la Pentekoste (FPCT) Singida, mchungaji Paulo Samweli akitekeleza majukumu yake.

ASKOFU mstaafu wa kanisa la Pentekoste (FPCT) Singida, mchungaji Paulo Samweli,amewasihi waumini na wananchi kwa ujumla wajenge utamaduni wa kukataa kushawishiwa kirahisi,kwa njia hiyo wanaweza   kujiepusha na mambo ambayo yanaweza kumsababishia washindwe  kuishi kwa amani na utulivu.

Askofu Samwel ametoa wito huo wakati akihubiri kwenye ibada ya kawaida ya waumini wa kanisa la FPCT la mjini Singida.

Askofu huyo mstaafu, alisema mambo yote maovu likiwemo la uchotaji wa fedha za akaunti ya escrow Tegeta,huanza na
ushawishi wa kutosha.Watu waovu/wenye dhambi ni mabingwa katika suala la ushawishi ambao mara nyingi, huwaingiza watu wema na waadilifu katika matatizo mazito.


“Hawa viongozi wasomi wazuri wanao daiwa kuchota fedha za akaunti ya ESCROW, kabla ya kuchota, kwanza walishawishiwa wakashawishika. Waliambiwa ‘bosi’/kiongozi hizi fedha hazina matatizo kabisa ,tukikupatia zitakuendeleza wewe na familia yako na hutapata tatizo lo lote kuhusiana na fedha hii”,alifafanua.

Akifafanua zaidi, alisema viongozi hao wasomi wazuri kwa sasa wanashangaa,wanashindwa kuamini wanayoyasikia kuhusu fedha za ESCROW.Wimbo sasa kila mahali nchini, ni kwamba wajiuzulu nyadhifa zao zinazowapatia heshima kubwa na kisha wafikishwe mahakamani mara moja.

“Waumini wenzangu na wananchi kwa ujumla,mwaka huu wa 2015 na kuendelea tukatae au  tusikubali kabisa kushawishiwa.Mambo ya kushawishiwa yatatuangamiza na yatatupeleka mahali pabaya mno”,alisema.

Aidha,askofu mstaafu Samwel,amewataka waache kuishi maisha ya ujanja ujanja,bali waishi maisha yanayompendeza Mungu,yanayotii sheria zilizowekwa na vipato vyao  vitokane na shughuli/kazi halali na si vinginevyo.


“‘Pia kuanzia mwaka huu wa 2015 na kuendela,tuachane na maisha yanayotawaliwa na papara nyingi,umbea,kujipendekeza,kujikweza  na kujisifu binafsi.Tutulize akili zetu na tusome biblia kila siku sambamba na vitabu vingine vitakavyotusaidia kupata elimu ya kupambana na maisha ya kimwili”alisisitiza askofu mstaafu, Samweli.

No comments:

Post a Comment