Wednesday, June 3, 2015

Halmashauri ya Manispaa Singida yapewa msaada wa zaidi ya Mil 250 kwa ajili ya malori ya taka ngumu.

Kijiko mali ya manispaa ya Singida kilichonunuliwa kwa shilingi 110 milioni,kikipakia taka ngumu kutoka kwenye dampo la soko la vitunguu mjini hapa jana.
Malori mawili mapya mali ya manispaa ya Singida yaliyotolewa na serikali kuu kwa ajili ya kuzoa taka ngumu. Thamani ya malori hayo ni zaidi ya shilingi milioni 140. Na chini picha ya kijiko hicho .
Serikali kuu imeipatia msaada  halmashauri ya manispaa ya Singida, kijiko na malori mawili makubwa vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi 250 milioni,kwa ajili ya uzoaji wa taka ngumu.

Hayo yamesemwa juzi  na mkurugenzi wa manispaa ya Singida, Joseph Mchina, wakati akizingumza na waandishi wa habari juu msaada huo ambao utasaidia kwa kiwango kikubwa kuboresha hali ya usafi katika mji wa Singida,na  pia zitapunguza gharama kubwa ya uzoaji taka ngumu.

Alisema malori hayo mawili ya tani 20 kila moja, thamani yake ni shilingi 70 milioni kila moja na kijiko ni shilingi 110 milioni.

 “Kwa mwezi tulikuwa tunatumia zaidi ya shilingi
30 milioni kugharamia uzoaji wa taka ngumu. Vitendea kazi hivi tunatarajia vitasaidia kuokoa  zaidi ya shilingi 20 milioni kwa mwezi…. kwa maana kwamba kwa sasa shughuli za uzoaji taka ngumu itatugharimu shilingi 10 milioni”,alisema.

Aidha, Mchina alisema kwa siku walikuwa wanauwezo wa kuzoa tani 40 za taka ngumu, lakini kuanzia sasa wanatarajia kuzoa tani 80 kwa siku.

 “Kwa ujumla, baada ya kupata kijiko na malori yetu wenyewe, tunatarajia mji wetu sasa utaongoza kwa usafi nchini,na si vinginevyo”,alisema mkurugenzi huyo na kuongeza kuwa;

 “Ninachoomba ni kwamba kila mkazi wa mji wa Singida, ashiriki kikamilifu kuhakikisha hakuna taka inayotupwa ovyo. Tunayo sheria ndogo ambayo inaelekeza kwamba mtu akikamatwa anachafua mazingira, atatozwa papo hapo faini yake ni shilingi 50,000/= ”.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo amewataka waandishi wa habari kutumia taaluma yao katika  kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kuuwezesha mji wa Singida kuwa msafi wakati wote,ili uwe  mfano wa kuingwa katika suala zima la usafi.

Kwa upande wake  mstahiki meya wa Manispaa ya Singida, Sheikh Salum Mahami, alitoa shukrani za pekee kwa Serikali kuu kwa msaada huo ambao utasaidia pia kupunguza idadi kubwa ya vibarua wanaofanya  usafi.

 “Kwa sasa tutapambana vizuri na shughuli hii ya kuzoa taka ngumu, kila mkazi wa mji na wageni wetu, tunapaswa kushiriki kikamilifu kuhakikisha mji wetu unakuwa msafi  wakati wote. Na sio hivyo tu, kila mmoja awajibike kukamata watu/mtu ye yote  anayechafua mji  na kuwafikisha kwenye mamlaka zinazohusika”,alisema Sheikh Mahami.

Pamoja na Manispaa ya Singida kuwa na sheria ndogo inayosema kuwa mtu akikamatwa anachafua mazingira alipishwe faini ya shilingi 50,000 papo hapo, pia imeweka ada ya usafi ambapo kila kaya inalipa ada kuanzia 2,000/=na kuendelea  kwa mwezi na viwanda 70,000/=.

1 comment:

  1. AnonymousJune 16, 2015

    Sasa hakuna sababu vifaa vipya hivyo mjii uwe safi acheni uchafu jamani aibu, Singida iwe safi tupate watalii na sifa nzuri.

    ReplyDelete