Saturday, June 20, 2015

Halmashauri ya wilaya ya Singida yatoa chanjo ya Vitamin “A” kwa watoto 39,166

Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari za tarafa ya Mtinko wakiwa kwenye na mabango yenye ujumbe wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika iliyofanyika kiwilaya kata ya Ughandi, Singida vijijini.

Vikundi vya ngoma vilivyokuwa vikitumbuiza kwenye sherehe za siku ya mtoto wa Afrika.

Kikundi cha kwaya kilichokuwa kikitoa burudani ya nyimbo mbali mbali zilizokuwa na ujumbe unaoashiria kupiga vita mimba na ndoa za utotoni.
Wanafunzi wa shule mbali mbali za msingi na sekondari wakiandamana kupita kwa mgeni rasmi wakati wa sherehe za siku ya mtoto wa Afrika iliyofanyika kiwilaya kata ya Ughandi,Singida vijijini.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Singida, Bwana Kinyemi Sepeku (wa pili kutoka kushoto aliyevaa miwani), akiangalia burudani ya ngoma za asili zilizoonyeshwa na kikundi cha ngoma cha akina mama.
Akina mama waliokuja na watoto wao wachanga wakiangalia burudani mbali mbali katika uwanja wa shule ya msingi Ughandi.
Picha ya mtoto mdogo aliyembeba mwenzake kuonyesha upendo katika siku yao akiangalia burudani ya ngoma zilizokuwa zikitumbuizwa na vikundi vya akina mama vilivyohudhuria kwenye maadhimisho hayo.

HALMASHAURI ya wilaya ya Singida imetoa chanjo ya matone ya Vitamin A kwa watoto 39,166 wenye umri wa chini ya miaka mitano katika kipindi cha kuanzia januari hadi juni,mwaka huu.

Hayo yalibainishwa na Afisa Maendeleo ya jamii wa Halmashauri ya wilaya ya Singida,Peter Njau alipokuwa akisoma taarifa ya wilaya kwenye maadhimisho ya kilele cha siku ya mtoto wa Afrika kiwilaya iliyofanyika kata ya Ughandi,tarafa ya Mtinko,wilayani hapa.

Aidha Njau alifafanua kwamba watoto waliopatiwa chanjo hiyo ni wenye umri wa kuanzia miezi 6 -11 ambao jumla yao ni 1,533 sawa na asilimia 86.7 kati ya watoto 1,764 waliotarajiwa kupatiwa chanjo hiyo katika kipindi hicho.

“Halmashauri imeendelea na jitihada za kutoa huduma za afya kwa watoto kwa mwaka 2015,watoto wenye umri chini ya miaka mitano wamepatiwa matone ya Vitamin “A” katika vituo vya Afya na Zahanati zote za Halmashauri ya wilaya ya Singida”alifafanua afisa maendeleo huyo.

Alifafanua Njau kwamba watoto waliolengwa kupata Vitamin “A” ni kuanzia umri wa miezi 6 -11 na kwamba watoto wenye umri kati ya miezzi 12 -59 waliolengwa kupatiwa chanjo hiyo ni watoto 35,841 na waliopata chanjo hiyo ni watoto 37,633 sawa na asilimia 105.

Kwa mujibu wa Njau ili kuhakikisha kuwa haki za mtoto zinalindwa na kuheshimiwa,Halmashauri ya wilaya ya Singida imeendelea kudumisha mahusiano mazuri kati yake na wadau mbalimbali wanaotoa huduma na misaada kwa watoto hao.

Wadau hao ni pamoja na Shirika la World Vision, Action Aid,HAPA,SEMA,SICD na mengine mengi ambayo hayakutajwa kwenye taarifa na kuongeza kwamba ushirikiano kati ya Halmashauri na wadau ni nyenzo muhimu sana katika kutokomeza ukatili dhidi ya watoto na kudumisha haki za msingi za watoto.

 Akiwahutubia wananchi na wanafunzi waliohudhuria maadhimisho hayo,kaimu Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo,Kinyemi Sepeku alitumia fursa hiyo kuwahimiza wazazi,walezi na jamii kwa ujumla kuwa watoto wanastahili kusikilizwa,kuendelezwa na kuhudumiwa ipasavyo ili waweze kukua na kuishi katika mazingira mazuri na salama.

Hata hivyo Sepeku ambaye kitaalumu ni Afisa elimu wa Halmashauri hiyo,alisisitiza kuwa ukatili wa kwanza kwa watoto ni ule wa kunyimwa haki ya kuishi kwa kuwaua watoto wenye ulemavu kwa lengo la kupata ukatili kwa njia za ushirikina.

“Hii inatokana na kuwepo mwendelezo wa kuwaua watoto wenye ulemavu wa ngozi,yaani Albino,mauaji haya yamechangiwa sana na mila potofu”alisema kwa msisitizo huku akiwaangalia wazazi waliohudhuria maadhimisho haya.

Naye Afisa miradi (Action Aid) Kanda ya kati yenye mikoa ya Singida na Dodoma,Festo Kilonzo alifafanua kwamba wazazi wana mchango mkubwa sana wa kuhakikisha kuwa watoto wanakuwa kwenye maadili ambayo yanahitajika kwa jamii.


Akiwasilisha salamu za shirika la World Vision Tanzania, Meneja wa ADP Mtinko, aliyetambulika kwa jina moja tu Mwari alizitaja shughuli zinazofanywa na shirika hilo kuwa ni pamoja na kujenga zahanati,kuchimba visima vya maji,kuangalia zaidi haki kumi za mtoto na kujenga shule lakini haliajiri walimu kwani hiyo ni kazi ya serikali.

No comments:

Post a Comment