Monday, June 22, 2015

Waswidi watoa bilioni 1.4 kugharamia mradi wa Mwanzo mwema.

Balozi wa Sweden nchini,  Mh. Lennarth Hjelmaker, akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa mradi wa ‘Mwanzo Mwema’ (A Good Start) unaofadhiliwa na nchi yake kwa zaidi ya shilingi bilioni 1.4.Pamoja na mambo mengine, balozi huyo ameahidi nchi yake itaendelea kushirikana na Tanzania katika kuboresha sekta mbalimbali ikiwemo ya afya.
Mwakilishi wa shirika la WaterAid Tanzania, Ibrahimu Kabole, akitoa ufafanuzi juu ya mradi wa ‘Mwanzo Mwema’ (A Good Start) ambao pamoja na mambo mengine,utashughulikia afya ya uzazi kwa akina mama wajawazito.Mradi huo unafadhiliwa na serikali ya Sweden. Kulia ni Balozi wa Sweden nchini, Mh. Lennarth Hjelmaker.
Baadhi ya wadau wa afya mkoani Singida, waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa mradi wa ‘Mwanzo Mwema’ (A Good Start) unaofadhiliwa na nchi ya Sweden kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 1.4.


Mku wa mkoa wa Singida, Dk.Parseko Kone (kushoto) akiwa na mgeni wake Balozi wa Sweden nchini, Mh. Lennarth Hjelmaker wakati wakikagua kituo cha afya cha Sokoine manispaa ya Singida. Kulia ni Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Singida, Aziza Mumba na nyuma ya balozi, ni mke wake. Balozi Hjemaker alikuwa mkoani humo kuzindua mradi wa ‘Mwanzo Mwema’ unaofadhiliwa na nchi yake kwa gharama ya zaidi ya shilingi biloni 1.4.
Balozi wa Sweden nchini, Mh. Lennarth Hjemaker, akiwa amevutiwa na mtoto aliyefikishwa kituo cha afya cha Sokoine mjini hapa kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

SERIKALI ya Sweden kupitia shirika lake la Riksförbundet för sexuell upplysning (RFSU), imetoa msaada wa zaidi ya shilingi 1.4 bilion, kugharamia mradi wa ‘Mwanzo Mwema’ (A Good Start), utakaojishughulisha na upatikanaji wa maji ya kutosha kwenye vituo vya kutolea huduma za afya katika halmashauri ya Iramba na manispaa ya Singida mkoani hapa, kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Shughuli zingine zitakazotekelezwa na mradi huo kwa ushirikano wa mashirika ya WaterAid Tanzania, Amref, RFSU na SEMA, ni kuboresha usafi wa mazingira katika vituo vya kutolewa huduma ya afya, afya ya uzazi kwa akina mama wajawazito, afya ya watoto wachanga na vijana.

Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi rasmi wa mradi huo iliyofanyika mjini hapa, Balozi wa Sweden nchini, Lennarth Hjelmaker, alisema kwamba lengo la mradi huo ni pamoja na kuimarisha haki za afya ya uzazi kwa wasichana, na pia  kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wanawake, wasichana na watoto 60,000 wa wilaya ya Iramba na manispaa ya Singida.

Alisema hilo litafanyika na kufanikiwa kwa uelewa mpana kwa watoa huduma na hitaji halisi la kumaliza mapungufu yaliyopo kwenye vituo vya afya  ifikapo mwaka 2017.Ametaja baadhi ya mapungufu hayo ni uhaba wa maji, vitendea kazi na usafi wa mazingira.

“Baadhi yenu mliopo hapa, nimekutana nanyi kwa nyakati tofauti huko kwenye asasi zenu mbalimbali. Kwa hali hiyo,nafarijika kuwaona leo mpo hapa na  pamoja na mambo mengine, matarajio yetu sote yawe ni kufanya kazi kwa pamoja, ili lengo la mradi liweze liwe  kufikiwa kwa  ufanisi mkubwa”,alisema.

Akisisitiza, Hjelmaker alisema kuwa, anaamini mradi huo utaokoa maisha kwa watoto wanaozaliwa, mama wanaokwenda kujifungua, wauguzi na waganga, kutokana na usafi kuimarika.

Katika hatua nyingine, Balozi Hjeimaker ameahidi kwamba nchi yao itaendeleza  ushirikiano na Tanzania, ili kuwasaidia wananchi, na hasa wanawake na watoto wachanga, katika kukabiliana na changamoto mbalimbali, ikiwemo huduma duni za afya, zinazoikabili jamii, hapa nchini.

Awali, Mwakilishi wa shirika la WaterAid Tanzania Dk.Ibrahimu Kabole alisema mwaka jana walifanya utafiti kwenye baadhi ya vituo vya kutolea huduma ya afya katika manispaa ya Singida na wilaya ya Iramba na kubaini mapungufu mengi makubwa ikiwemo uhaba wa maji, vitendea kazi na kiwango duni cha usafi wa mazingira.

Akifafanua, Dk.Kabole alisema mapungufu hayo na mengine kwa kiasi kikubwa yanachangia vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga kwa kuambukizwa maradhi kupitia bakteria wa aina mbalimbali.

“Kwa ushirikiano wetu katika kutekeleza mradi huu, wenzetu wa AMREF, wao watajikita zaidi katika utoaji wa elimu juu ya haki za msingi na  hasa ya kila mwananchi anastahili kupata elimu. Hapa kwa wasichana ambao hawamalizi darasa la saba, watajengewa uwezo ili waweze kupata haki yao ya elimu kadri uwezo wao utakavyowaruhusu”,alifafanua.


Mwakailishi huyo ametumia fursa hiyo kuziomba halmashauri ya wilaya ya Iramba na manispaa ya Singida, kutoa ushirikiano wa dhati ili utekelezaji wa mradi huo uweze kuzaa matunda mazuri na hivyo kuwa mfano mzuri wa kuigwa na vituo vingine nchini katika utoaji wa huduma bora za afya ikiwemo huduma ya afya ya afya ya uzazi.

No comments:

Post a Comment