Tuesday, May 12, 2015

Wanafunzi 365 na walimu wanane wachangia choo kimoja chenye matundu manane.

Baadhi ya wazazi wa shule ya msingi Kilimani waliohudhuria kwenye mkutano wa wazazi wa shule hiyo uliofanyika kwenye viwanja vilivyotengwa kwa ajili ya mikutano shuleni hapo.


WANAFUNZI 365 pamoja na walimu wanane wa shule ya msingi Kilimani, kata ya Ibaga, tarafa ya Kirumi, wilayani Mkalama wanachangia matundu manane ya choo yaliyopo kati ya matundu 17 yanayohitajika katika shule hiyo.

Hayo yalibainishwa na mwalimu mkuu wa shule hiyo, Hamisi Masimba kwenye mkutano wa wazazi wa shule hiyo uliofanyika kwenye viwanja vilivyotengwa kwa ajili ya kufanyia mikutano mbali mbali ya shule hiyo.

Aidha mwalimu huyo alifafanua kuwa kutokana na upungufu huo wa matundu ya choo yaliyotenganishwa sehemu ya wanafunzi wa kiume na wa kike na ukuta,kumechangia kwa kiasi kikubwa wanafunzi wa kiume na wa kike wanapojisaidia huanza kuchunguliana kwenye matundu yaliyopo ili kuangalia anachofanya mwenzake.

Hata hivyo kibaya zaidi katika matumizi ya huduma hiyo shuleni hapo ni kwamba inapofikia wakati mwalimu yeyote yule anapotaka kwenda kujisaidia kwenye vyoo hivyo hulazimika kuweka ulinzi wa mwalimu mwenzake nje kuwazuia wanafunzi kwenda kujisaidia kwa wakati huo, kitendo ambacho kinaweza kuchangia wanafunzi kujisaidia kwenye eneo la msitu uliopandwa karibu na shule hiyo na hivyo hatarisha mazingira ya shule.

“Kwa kweli hali ya matundu ya vyoo katika shule yetu hii ni ya kutisha kwani kutokana na wanafunzi wote kutumia jengo moja lenye matundu ya vyoo manane lililotenganishwa na ukuta tu na hivyo wanapokwenda kujisaidia huanza kuchunguliana kila mmoja aweze kumuona mwenzake anavyojisaidia”alisisitiza mwalimu huyo.

Kwa mujibu wa Masimba katika mkutano huo uliolenga kuwahamasisha wazazi kuchangia chakula cha mchana kwa watoto wao baada ya WFP kuanza kukaribia kumaliza kipindi chake cha kutoa msaada,alisema ili kuondokana na adha hiyo wamelazimika kuwaita wazazi ili kuwaomba wachangie ujenzi wa matundu hayo kupunguza na kama siyo kumaliza tatizo hilo.

Hata hivyo wakati mkutano huo wa wazazi ukiendelea mwandishi wa habari hizi alishuhudia wanafunzi wa kiume na wale wa kike wakifukuzana kuwahi kwenda kujisaidia kabla ya mwingine,na hivyo kutokana na uhaba huo wa matundu walilazimika kulundikana kwenye milango wakisubiriana kuingia.

Baada ya kamati ya shule kujenga hoja kwa wazazi kuhusu tatizo hilo ndipo wazazi walikubaliana kuchangia shilingi mia tano kila kaya kwa ajili ya kumlipa fundi atakayefukua shimo la choo lenye matundu mawili na kukamilisha ujenzi wake kabla ya mwisho wa mwezi huu matundu hayo yawe yamekamilika.

Changamoto zingine zinazoikabili shule hiyo inayoongoza kwa kufaulisha wanafunzi wote wa darasa la saba kuanzia mwaka 2012 hadi 204 ni pamoja na upungufu wa vyumba vya madarasa matatu kati ya vyumba tisa vinavyohitajika,nyumba za walimu kumi zinazohitajika,ofisi mbili za walimu kati ya tatu na stoo moja kati stoo mbili zinazohitajika.  

Shule ya msingi Kilimani iliyofunguliwa aprili,08,2008 ikiwa na darasa la kwanza hadi la tatu,huku ikiwa na walimu wawili na madarasa mawili,hivi sasa shule hiyo ina jumla ya walimu wanane ina wanafunzi 365 wanaofundisha darasa la kwanza hadi la saba.

No comments:

Post a Comment