Thursday, January 3, 2013

Wanne wa Familia moja wateketea kwa Moto kuelekea mkesha wa Mwaka Mpya mkoani Singida.

Kamanda wa polisi mkoa wa Singida Linus Sinzumwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) ya wanafamilia wanne kufariki dunia baada ya kuangukiwa na nyumba ya Tembe.

 Watu wanne wa familia moja wakazi wa kijiji cha Kilunda tarafa ya Nduguti wilaya ya Mkalama mkoani Singida wamefariki dunia papo hapo baada ya
kuangukiwa na nyumba yao ya tembe.
Mvua nyingi zinazoendelea kunyesha mkoani Singida hivi sasa, zimepelekea paa la nyumba hiyo ya tembe iliyokuwa imeezekwa kwa miti aina ya mapawa na kukandikwa kwa udongo mwingi, kuporomoka na kuwafunika wanafamilia hiyo.
Baada ya kufunikwa, miti iliyokuwa imetumiwa kuezekea tembe hilo ilishika moto uliokuwa umewashwa kwa ajili ya familia hiyo kukabiliana na baridi ya usiku na kuanza kuteketeza miili ya watu hao.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Singida Linus Sinzumwa aliwataja wanafamilia hao kuwa ni Enock Edson (22), Kefasi Edson (14), Kulwa Edson (12) mwanafunzi wa darasa la sita shule ya msingi Nduguti, Elisha Edson (9) mwanafunzi wa darasa la tatu   shule ya msingi Nduguti.
Amesema tukio hilo la kusikitisha limetokea mkesha wa kumakia mwaka mpya 2013 usiku wa manane wakati familia hiyo ikiwa imelala.
Sinzumwa amesema mbali na wanafamilia hiyo pia ndama wawili na mbuzi 1 ,walikufa kutokana na kuangukiwa na paa la tembe hilo.
Kamanda Sinzumwa ametumia fursa hiyo kuwataka watu wanaomiliki nyumba za tembe pamoja na kuezekwa kwa bati wajenge tabia ya kukagua nyumba zao mara kwa mara ili kuepusha majanga au watu kupoteza uhai na mali zao.

1 comment: