Kamanda Geofrey Kamwela
MKAZI wa Kijiji cha Chang’ombe kata, tarafa na wilaya ya Manyoni mkoani Singida Andrew Mlunda (40),amefariki dunia akiwa porini kutafuta na kuchimba dawa ya kienyeji.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida,SACP, Geofrey Kamwela amesema marehemu aliondoka nyumbani kwake juzi saa 10.00 jioni akiwa amebeba shoka na kuiaga familia yake kuwa anakwenda porini kutafuta dawa yake ya kifua kwani alikuwa anahisi maumivu.
Kamwela amesema kuwa tangu alipoondoka hakurudi nyumbani hadi giza lilipoingia na kusababisha hofu kwa familia yake.Hata alipopigiwa simu,simu yake ya kiganjani haikuweza kupatikana.
Kutokana na hali hiyo,amesema kuwa familia hiyo ilitoa taarifa kwa majirani na mara moja majirani walianza msako wa kumtafuta ndani ya pori la kijiji hicho.
“Wakiwa porini waliendelea kumpigia simu na kwa bahati walisikia mlio wa simu kutoka kichakani na waliposogea sehemu mlio wa simu ulikuwa unatoka,walimkuta Andrew akiwa tayari ameishafariki dunia”,amesema na kuongeza;
“Walimkuta akiwa ametoka damu nyingi huku shoka lake likiwa pembeni, baada ya hapo,walitoa taarifa katika kituo cha polisi Manyoni mjini na askari walifika mara moja na kuuchukua mwili kwa ajili ya uchunguzi”.
Kamwela amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa marehemu amefariki dunia baada ya
kupigwa na kitu kizito kwenye paji la uso na watu au mtu asiyejulikana.
Aidha, Kamanda huyo amesema chanzo cha tukio hilo bado hakijajulikana na polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi kujua chanzo.Hata hivyo hakuna mtu au watu waliokamatwa kuhusiana na mauaji hayo.
No comments:
Post a Comment