Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Singida, SACP Geofrey Kamwela.
Wito huo umetolewa mwishoni mwa wiki na kiongozi wa dawati la jinsia na watoto mkoa wa Singida Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Eileen Mbwatila wakati akizungumza na waandishi wa habari wanaotathmini utekelezaji wa mradi wa ushiriki sawa wa wanaume katika masuala ya afya ya uzazi na jinsia (TMEP).
Mradi huo unatekelezwa kwa pamoja na mashirika ya HAPA na YMC ya mjini hapa.
Alisema uzoefu unaonyesha wazi kwamba wanawake wengi mkoani hapa, wanaendelea kukandamizwa kwa kuachiwa kazi zote za nyumbani na wanaume,wananyanyaswa na wanapigwa vibaya kutokana na kutokujua haki zao.
Mbwatila alisema vitendo vingi viovu wanavyofanyiwa wanawake hasa na wanaume wakiwemo waume wao,vimekuwa vikifikishwa kwa ndugu ambao kazi yao ni kutoa
suluhu tu,badala ya vyombo vya sheria ambavyo kwa kiasi kikubwa vinakomesha vitendo hivyo.
“Wanandugu hawa kazi yao ni kusuluhisha tu na hawatafuti ufumbuzi wa kumaliza tatizo. Utakuta mwanamke amefanyiwa kitendo cha jinai lakini ndugu watang’ang’ania kutoa suluhu jambo ambalo halitoi ufumbuzi wa kudumu mbali linaendeleza unyanysaji na vitendo viovu kuwa sugu,” alisema mrakibu huyo msaidizi wa polisi.
Akiijengea nguvu hoja yake hiyo, Mbwatila alisema kati ya Januari na Machi mwaka huu, jumla ya wanawake 88 wameshambuliwa na wanaume wakiwemo waume zao.
“Matukio hayo 88 (yaliyoripotiwa tu) kwa kipindi kifupi ncha miezi mitatu, ni kielelezo tosha kwamba wanawake wanaendelea kuathirika na unyanyasaji kutokana na kutokujua haki zao.
Kwa upande wa wanaume, mrakibu msaidizi huyo wa polisi alisema wanaume ni nadra sana kutoa taarifa ya kunyanyaswa na wake au wanawake, kwa hofu ya kudharaulika mbele ya jamii inayowazunguka.
Kwa hali hiyo, Mbwatila alisisitiza kwamba elimu ya ushiriki sawa wa wanaume katika afya ya uzazi na ujinsia, ikaendelea kutolewa kwa madai ndiyo itakayoondoa kabisa vitendo vya unyanyasaji kwa upande wa wanawake.
Mradi wa TMEP unaotarajiwa kumalizika desemba mwaka huu,umetarajiwa kutumia zaidi ya shilingi 1.6 biloni.
No comments:
Post a Comment