Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Singida, SACP Geofrey Kamwela.
WATU Wanne mkoani Singida wamefariki dunia katika matukio tofauti,likiwemo la wanandoa wawili kuuawa na kisha nyumba yao kuchomwa moto na wao kuteketea pamoja na mali zao.
Wanandoa hao ni Ramadhani Lyanga (80) na mke wake Aziza Ally (60) wakazi wa kitongoji cha Kizega kijiji cha New Kiomboi tarafa ya Kisiriri wilaya ya Iramba.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Singida, SACP Geofrey Kamwela amesema tukio hilo la kusikitisha,limetokea Juni 10 mwaka huu saa 7.15 usiku huko katika kitongoji cha Kizega.
Amesema mtu huyo alivunja mlango wa nyumba ya vikongwe hao kwa kutumia kitu kizito kinachodhaniwa kuwa ni jiwe aina ya Fatuma na alipoingia ndani moja kwa moja alienda chumba walichokuwa wamelala wajukuu wao watatu wa vikongwe hao na kuwatisha.
“Baada ya kuwatisha wajukuu hao mtu huyo alihamia chumba walikolala wanandoa hao na kuanza kuwacharaza fimbo hadi walipofariki dunia.Baada ya kufariki dunia,alimwaga petrol chumba kizima cha wazee hao na kisha kuwasha moto kwa kutumia njiti ya kiberiti”,amesema Kamwela.
Kamanda huyo,amesema wajukuu wa wazee huyo
waliweza kujinasua na kutoka nje huku wakipiga kelele za kuomba msaada na ndipo ndugu na majirani walipofika na kukuta tayari moto unateketeza nyumba hiyo wakiwemo wazee hao.Watu hao hawakuweza kunusuru kitu cho chote.
Amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa tukio hilo linahusiana na imani ya kishirikina na kwamba nyumba hiyo ilinusurika kuchomwa moto machi mwaka huu.
Katika tukio jingine,Kamwela amesema kuwa Charles Pandaa (54) na Njiku Mboni (43)wote wakazi wa kijiji cha Mabondeni kata ya Aghondi tarafa ya Manyoni wilaya ya Manyoni,wamefariki dunia juni 11 mwaka huu saa 1.20 jioni baada ya kugongwa na gari aina ya toyota L/crusier T.463 AYD.
Amesema watu hao waligongwa wakiwa wamepakizana kwenye baiskeli wakitokea kijiji cha Itagata wakirudi Manyoni mjini.Inadaiwa wapanda baiskeli hao waliingia barabarani (kichwa kichwa) bila kuchukua tahadhari yo yote.
Kamanda huyo amesema wanamshikilia dereva huyo kwa ajili ya mahojiano na pamoja na uchunguzi.
No comments:
Post a Comment