Naibu Waziri wa Maji, Mh. Amos Makala, akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa kijiji cha Makale na Itagata jimbo la Manyoni magharibi.Makala alikuwa jimbo la Manyoni magharabi kwenye ziara ya kikazi ya siku moja.Kushoto ni mbunge wa jimbo la Manyoni magharibi, John Paulo Lwanji.
Mhandisi wa maji halmashauri ya wilaya ya Manyoni, Eng.Desidedit Magoma.(wa kwanza kushoto) akitoa maelezo kwa naibu waziri wa maji Amos Makala (mwenye kaunda suti) juu ya maendeleo ya ujenzi wa bwawa la kijiji cha Itagata.Anayeangalia kamera ni mbunge wa jimbo la Manyoni magharibi,John Paulo Lwanji.
Baadhi ya wakazi wa kata ya Itigi, wakimsikiliza Naibu Waziri wa Maji,Amos Makala wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara.Makala aliwaambia wakazi hao kuwa serikali itatenga zaidi ya shilingi 1.5 kwa ajili ya kazi ya usanifu na ujenzi wa miundo mbinu ya maji katika mjini huo mdogo wa Itigi unaotarajiwa kuwa makao makuu ya wilaya ya Itigi.
Naibu Waziri wa Maji, Amos Makala (Mb), amefanya ziara ya kikazi katika wilaya ya Manyoni mkoa wa Singida na kutangaza neema ya maji baada ya kusema kuwa serikali imetenga zaidi ya shilingi 1.8 bilioni kupunguza kero ya uhaba wa maji wilayani humo.
Makala ameyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mbwasa jimbo la Manyoni mashariki na kwenye vijiji vya Makale, Itagata na Itigi jimbo la Manyoni magharibi.
Amesema serikalia inatambua tatizo la maji lililopo wilaya ya Manyoni,kupitia wabunge wake ambao wametumia muda mwingi kuihimiza serikali kuondoa kero hiyo ya maji inayowakabili wapiga kura wao na wananchi kwa ujumla.
“Niwahakikishie tu wananchi wa kata ya Mitundu na jimbo la Manyoni magharibi, kwamba mbunge wenu Lwanji kwa muda mrefu ameibana serikali juu ya tatizo la maji linalowakabili. Kwa hiyo, niwatoe hofu, kwa sababu hivi sasa
serikali imetenga fedha kwa ajili ya kupunguza na ikiwezekana kuliondoa kabisa tatizo la maji”,amesema Makala.
Aidha,Naibu Waziri huyo amesema Wizara imepokea maombi mengine ya miradi ya maji katika vijiji vya Itagata na Lulanga ya zaidi ya shilingi 926 milioni.Wizara kwa sasa inaendelea kuyapitia maombi hayo na kuyapatia ufumbuzi wa kudumu.
“Wananchi wa jimbo la Manyoni magharibi ninachoweza kuwaambia,ni kwamba kuweni na uvumilivu wakati huu ambapo serikali ipo kwenye mchakato wa kutoa fedha hizo za maji,iliyotenga kwa ajili ya kuwaondolea kero ya maji safi na salama wananchi wa wilaya ya Manyoni wakiwemo wa jimbo la Manyoni magharibi”,amesema Makala.
Akisisitiza zaidi, amesema ilani ya uchaguzi ya CCM ya sasa,imetamka wazi kwamba upo umuhimu mkubwa wa kupunguza kero ya uhaba wa maji na yapatikane kwa umbali mfupi.
“Malengo ya ilani ya uchaguzi ya sasa, yatafikiwa kabla ya mwisho wa mwaka kesho.Malengo hayo ni pamoja na kuondoa tatizo la uhaba wa maji safi na salama lililopo hivi sasa.Kwa hiyo nawaomba muendelee kuiamini serikali yenu ndiyo yenye uwezo wa kutatua kero hiyo na si vinginevyo”,amesema.
No comments:
Post a Comment