Monday, December 2, 2013

Dk. Kone afunga semina ya siku mbili ya soko la kukuza Ujasiriamali (EGM).

Mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko Vicent Kone, akifungua semina ya siku mbili iliyohusu soko la kukuza ujasiriamali (EGM) iliyoandaliwa na soko la hisa la Dar-es-salaam (DSE) na kufadhiliwa na Financial Sector Deepening trust (FSDT).Semina hiyo imefanyika kwenye ukumbi wa Aque Vitae hotel mjini Singida. Kushoto ni Afisa Mahusiano na mshauri wa masula ya Kisheria wa soko la Hisa  Dar-es-salaam, Bi.Mary Mniwasa na kulia ni mwenyekiti  wa TCCIA mkoa wa Singida,Francis Mashuda.
Baadhi ya wajasiriamali na wafanyabiashara mjini Singida,waliohudhuria semina ya siku mbili iliyohusu soko la kukuza Ujasiriamali (EGM) iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Aqua Vitae hoteli mjini Singida.
Mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko Vicent Kone (wa pili kushoto) akijadiliana jambo na Afisa Mahusiano na mshauri wa masuala ya Kisheria wa soko la Hisa la Dar-es-salaam,Bi. Mary Mniwasa,(wa pili kulia) muda mfupi baada ya kufungua semina ya siku mbili iliyohusu soko la kukuza Ujasiriamali (EGM).
Mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko Vicent Kone,(wa pili kulia walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wajasiriamali na wafanyabiashara wa mjini Singida waliohudhuria semina ya siku mbili ya soko la kukuza Ujasiriamali (EGM).Wa kwanza kulia (walioketi) ni afisa mahusiano na mshauri wa masuala la kisheria wa soko la hisa la Dar-es-salaam (DSE) Mary Mniwasa na kushoto ni mwenyekiti wa TCCIA mkoa wa Singida,Francis Mashuda.

WAJASIRIAMALI na wafanyabiashara mkoani Singida wametakiwa kuchangamkia fursa zilizopo Soko la Hisa la Dar es Salaam ili kuboresha na kuendeleza biashara zao.
Mwito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk Parseko Kone wakati akifungua semina ya siku mbili juu ya Soko la kukuza ujasiriamali iliyofanyika ukumbi wa Aqua Vitae mjini hapa.

Dk Kone alisema kuwa Soko la Hisa la Dar es Salaam kupitia kitengo chake kipya kijulikanacho kama “Soko la Kukuza Ujasiriamali”, ni suluhisho la upatikanaji wa mitaji kwa wajasiriamali kote nchini.
Alisema kuwa soko hilo litatoa suluhisho kwa changamoto zinazowakabili wajasiriamali katika upatikanaji wa uhakika wa mitaji ya muda mrefu kwa ajili ya kuendeleza biashara zao, jambo ambalo limekuwa likiwasumbua wajasiriamali na wafanyabiashara.

“Kwa hiyo basi, soko la kukuza ujasiriamali litasaidia kuleta msukumo wa utekelezaji sera mbalimbali za serikali zinazolenga kuondoa changamoto hizo na kuleta urahisi wa upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya kukuza biashara zao,” Dk Kone alisema.
Aidha, alieleza kuwa soko hilo linatarajiwa kulichangamsha soko kwa ujumla kupitia ongezeko la utoaji na uorodheshaji wa hisa, kupanua wigo na fursa za kuwekeza mitaji na kuongeza
ari ya wananchi kujiwekea akiba.

Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa huo, baadhi ya faida ziletwazo na soko hilo ni kupunguziwa kodi katika gawio, kusamehewa kodi kwenye ongezeko la thamani ya mtaji na ushuru wa stempu na punguzo kodi ya makampuni.

No comments:

Post a Comment