Sunday, December 1, 2013

AMPIGA FIMBO YA KICHWA MAMA MKWE NA KUMSABABISHIA MAUTI, KISA KACHOKA KUMLEA.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida, ACP. Geofrey Kamwela akitoa taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo kwenye picha) juu ya matukio ya kuuawa watu wawili mkoani Singida, likiwemo la Egila Petro kumpiga kwa fimbo mama mkwe wake mwenye umri wa miaka 80 na kusababisha kifo chake.

WATU wawili mkoani Singida wamefariki dunia kwenye matukio tofauti likiwemo la kikongwe mmoja mwenye umri wa miaka 80, kupigwa fimbo kichwani na mkwewe kwa kile kilichodaiwa kuwa mkwewe huyo, amechoka kumlea.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida SACP,Geofrey Kamwela, amesema Egila Petro (42) mkazi wa kijiji cha Mpora kata ya Iseke tarafa ya Nkoko wilayani Manyoni amempiga fimbo kichwani mama mkwe wake Doris Chiwiche na kumsababishia kifo chake siku tisa baadaye.

Amesema kikongwe huyo Doris alipigwa fimbo kichwani na Egila Novemba 18 mwaka huu saa nane mchana na alifariki Novemba 27 mwaka huu saa 12 asubuhi.

Kamwela amesema chanzo cha mauaji hayo ni mgogoro wa chini kwa chini kati ya Egila na mama mkwe wake Doris huku ikidaiwa kuwa Egila amekuwa akimshinikiza mumewe Benard Mdemu amwondoe mama yake huyo na kumpeleka kwa ndugu zake wengine kwa vile yeye amechoka kumlea.

Katika tukio jingine Kamanda Kamwela amesema John Liongo (37) mkazi wa Misuna Singida mjini amefariki dunia baada ya kupigwa risasi kichwani na tumboni na watu wasiojulikana.

Amesema tukio hilo limetokea Novemba 27 mwaka huu saa 6.10 mchana huko katika kijiji cha Mnang’ana kata na tarafa ya Sepuka wilayani Ikungi.

“Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa marehemu akiwa na watu wasiojulikana siku ya tukio aliondoka Singida mjini kwa gari ambalo bado halijajulikana namba zake za usajili Walipofika katika kijiji cha Mnang’ana waliingia porini na huko ndiko walipomuulia John”,alifafanua Kamwela.

Kamanda huyo amesema katika eneo hilo la mauaji waliokota
maganda watatu ya SAR na SMG ambayo risasi zake zilitumika kumuulia John.

“Niseme tu kwamba uchunguzi zaidi bado unaendelea kwa lengo la kuwabaini wauaji hao waweze kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria”,amesema.

No comments:

Post a Comment