Tuesday, December 3, 2013

Klabu ya Waandishi wa Habari waaswa kuacha makundi.

Katibu mtendaji  wa klabu ya waandishi wa habari (Singpress) mkoa wa Singida, Abby Nkungu akitoa taarifa yake juu ya baadhi ya wanachama na viongozi wa klabu hiyo waliosimamishwa Uanachama kutokana na tuhuma mbalimbali.
Mkurugenzi mtendaji wa Umoja wa vilabu vya waandishi wa habari (UTPC) Tanzania, Abubakari Karsan akitoa nasaha zake mbele ya mkutano mkuu maalum wa klabu ya waandishi wa habari (Singpress) mkoa wa Singida.Mkutano huo uliitishwa kwa ajili ya kuwajadili baadhi ya wananchama ambao hawajishughulishi kikamilifu na kazi ya uandishi wa habari.
Baadhi ya wananchama wa klabu ya waandishi wa habari (Singpress) mkoa wa Singida, wakifuatilia kwa makini taarifa zilizokuwa zikitolewa kwenye mkutano mkuu maalum wa klabu hiyo.
WANACHAMA wa Klabu ya Waandishi wa Habari (Singpress) Mkoa wa Singida wameaswa kuacha kuendeleza makundi kwa madai kwamba yatadumaza ustawi wa klabu hiyo.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari (UTPC) Tanzania, Abubakar Karsan wakati akizungumza kwenye Mkutano Mkuu maalum wa klabu hiyo ya Singpress.

Amesema makundi kwenye chama au kikundi chochote cha watu ni sumu ya maendeleo kwa umoja wa wahusika.

Karsan amesema kuwa maendeleo endelevu ya kikundi au chama cho chote yataletwa na ushirikiano wa dhati baina ya wahusika wa chama au kikundi.

“Mimi niwaombe tu muepuke kuwa na makundi imarisheni ushirikiano upendo na kuvumiliana kwa lengo la kuendeleza klabu yenu Pia viongozi watumikieni kikamilifu wanachama wenu kwa kuwapa fursa kwanza”,amesema.

Katika hatua nyingine, Karsan amesema UTPC imesikitishwa sana na kitendo cha baadhi askari polisi wa Mkoa wa Singida kuwanyanyasa na kuwazuia waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao.

“Hata hivyo niwaombeni mfahamu kwamba kitendo hicho hakijafanywa na Jeshi la Polisi isipokuwa kimefanywa na wahuni wachache walioko katika Jeshi la Polisi, Polisi kwa ushirikiano na UTPC itawachukulia hatu stahiki wahuni hao”,alifafanua Karsan.

Mkutano huo maalum, umemchagua Jenifrida Hongoa kuwa Mweka Hazina wa klabu hiyo baada ya kuzoa kura 11 za ndio kati za 15 zilizopigwa.

Hongoa ameziba nafasi hiyo baada ya aliyekuwa Mweka Hazina Awila Silla, kuvuliwa wadhifa huo kwa madai kuwa sio mwanachama halali na pia hana uwezo wa  kumudu nafasi hiyo.

Aidha, Mkutano huo umemchagua Damiano Mkumbo kuwa Makamu Mwenyekiti na Hudson Kazonta kuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji.

Wakati huo huo, Mkutano huo umewaagiza Doris Meghji na Daudi Nkuki kuwasilisha kwa kamati ya utendaji vielelezo vya
kutumikia vyombo vya habari na zionyeshe wazi kwamba wanatumika kikamilifu ili waweze kurudishiwa uanachama wao.

No comments:

Post a Comment