Wednesday, March 12, 2014

Halmashauri ya Singida kutumia zaidi ya shilingi 350 milioni kujenga machinjio.

Mkurugenzi wa manispaa ya Singida, Joseph Mchina akitoa taarifa yake ya utekelezaji mbele ya kikao maalum cha baraza la madiwani. Wa pili kulia ni Mustahiki meya wa manispaa ya Singida na Sheikh wa mkoa wa Singida,Salum Mahami.Wa kwanza kushoto ni mwenyekiti wa CCM manispaa ya Singida, Hamisi Nguli na anayefuatia ni makamu meya manispaa ya Singida, Hassan Shabani Mkata.

HALMASHAURI ya Manispaa ya Singida inatarajia kutumia zaidi ya shilingi 350 milioni, kwa kujenga machinjio ya kisasa katika eneo la Ng’aida kijiji cha Kisaki.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo,Joseph Mchina wakati akitoa taarifa yake ya ujenzi huo mbele ya kikao cha baraza la madiwani.

Amesema eneo hilo lililoridhiwa kwa ujenzi huo na serikali ya kijiji cha Kisaki,lina ukubwa wa ekari 6.72,na jumla ya zaidi ya shilingi 11.2 milioni, zimetengwa kwa ajili ya kulipa fidia kwa wakazi watakaohamishwa kupisha ujenzi huo.

Akifafanua,Mchina amesema manispaa imeibua maradi huo ikiwa ni kutekeleza mkakati wa kuboresha mazao yatokanayo na mifugo hususani nyama na ngozi.

Aidha,, Mkurugenzi huyo amesema kuwa machinjio ya awali ambayo yalianza kujengwa eneo la Manguanjuki na ujenzi huo ukagharimu shilingi
52,650,000,umesitishwa kwa madai kwamba eneo hilo linafaa zaidi kwa ujenzi wa hoteli ya kitalii.

“Uthamini uliofanyika mwaka 2010/2011,ulionyesha kuwa thamani ya jengo hilo na eneo lilipojengwa,ni shilingi 195 milioni.Menejimenti imependekeza kuwa atafutwe mwekezaji wa kununua jengo hilo ili fedha itakayopatikana,ichangie kwenye ujenzi wa machinjio ya kisasa itakayojengwa katika eneo la Ng’aida”,amesema Mchina.


Mchina amesema mwekezaji atafutwe kwa njia ya kutoa matanagazo kwenye magazeti,radio,televisheni na mbao za matangazo.

No comments:

Post a Comment