Wednesday, October 8, 2014

Meya ataka wasio na shughuli mijini kurejea vijijini.

Mstahiki Meya wa Nanispaa ya Singida, Sheikh Salum Mohammed Mahami ,akizungumza kwenya hafla ya uzinduzi wa shirika la TUSIFO. Hafla hiyo imefanykia katika shule ya msingi Kibaoni na Sheikh Mahami, alitumia fursa hiyo kuwasihi wakazi ambao hawana shughuli za kufanya mjini,warejee/waende vijijini kwa madai kuwa kwa sasa mazingira ya mjini, sio rafiki kwao tena. Kushoto ni mkurugenzi wa shirika la TUSIFO, Costantino Charles.
Mkurugenzi wa shirika lisilola kiserikali la Tunawakaribisha Singida Foundation (TUSIFO) la mjini Singida, Costantino Charles akizungumza muda mfupi kabla hajamkaribisha mgeni rasmi Mstahiki Meya wa manispa ya Singida, Sheikh Salum Mohammed Mahami, kuzindua rasmi shirika lisilo la kiserikali la Tunawakaribisha Singida Foundation (TUSIFO).T USIFO linajishughulisha na kutoa misaada ya madaftari, kalamu, sabuni na sare kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika katika masniapaa ya Singida.Kulia ni mstahiki meya wa manispaa ya Singida, Sheikh Salum Mohammed Mahami.
Mstahiki meya wa manispaa ya Singida, Sheikh Salum Mohammed Mahami, akikabidhi msaada wa daftari na kalamu kwa baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Kibaoni mjini Singida.


Baadhi ya wanafunzi walionufaika na msaada wa madaftari na kalamu uliotolewa na shirika la TUSIFO.

MSTAHIKI meya wa manispaa ya Singida, Sheikh Salum Mohammed Mahami, amewasihi wakazi wasio kuwa na shughuli maalum za kufanya mjini, warejee/waende vijijini kwa madai kwamba mazingira ya maeneo ya mjini, sio rafiki kwao.

Sheikh Mahami ambaye pia ni sheikh wa mkoa wa Singida, alisema kuwa mazingira ya mjini sio rafiki kwa watu wasio na kazi maalum za kufanya  kwa sababu gharama za kuishi mijini kwa sasa zimekuwa zikipanda kila kukicha na kupelekea maisha kuwa magumu mno kwa watu wasio kuwa na kipato.

Meya huyo ametoa wito huo wakati akizindua shirika lisilo la kiserikali la Tunawakaribisha Singida Foundation (TUSIFO) linalojishughulisha na kutoa misaada kwa wanfunzi wa shule za msingi na sekondari kwa manispaa ya Singida.

Alisema maisha ya mijini kwa sasa yanafaa zaidi kwa watu wanaofanya kazi  za kueleweka na wafanyabiashara, kwa vile wao wanao uwezo mzuri wa kumudu vema gharama hizo.


“Wafanyakazi na wafanyabiashara, hawa wana uhakika wa kupata chakula mara tatu kwa siku kama inavyotakiwa. Lakini ndugu zetu wasio na shughuli maalum za kufanya,wao hata kupata chakula mara moja kwa siku,kwao ni taabu kubwa”, alifafanua.

Akifafanua zaidi, Sheikh Mahami, alisema pia wasio na shughuli maalum za kufanya, wanalo tatizo la kuzaa watoto wengi bila utaratibu…….familia moja inaweza kuwa na watoto zaidi ya 10 wanaozaliwa mfululizo.

Aidha, alisema uzazi huo usio na tija ,hauzingatii kabisa uwezo wa kuwalea watoto vizuri na ule wa kugharamia masomo.

“Kule vijijini bado kuna maeneo ya ardhi ya kutosha ambapo mhusika anaweza kulima mazao ya kula na ya biashara ,akajipatia chakula cha kutosha na wakati huo huo, akaboresha hali yake ya kiuchumi kwa kuuza mazao ya biashara. Kwa hiyo nawasihi watu wasio na shughuli za kufanya hapa mjini,warudi kijiji mahali wanaweza kujiletea maendeleo na kusomesha watoto wao bila shida”, alisema Sheikh Mahami.

Awali Mkurugenzi wa TUSIFO, Costantino Charles alisema yeye pamoja na wananchama 15 waasasi hiyo, wameamua kuchangishana na kununua madaftari, kalamu, sabuni na sare ili kuwasaidia wanafunzi waweze kuendelea na masomo yao bila kuwa na matatizo.

“Baada ya kubaini baadhi ya wanafunzi kuacha shule kutokana na kukosa mahitaji hayo,tumemua tuchangishane sisi wenyewe na kuwaondolea kero hiyo wanafunzi kama njia moja wapo ya kuwajengea mazingira mazuri ya kujifunzia”, alisema Costantino.


Mkurugenzi huyo ametumia fursa hiyo,kuwaomba wadau wa sekta ya elimu kuiunga mkono asasi hiyo,ili iweze kufikia malengo yake.

No comments:

Post a Comment