Tuesday, October 7, 2014

Shirika la FU-DI kutumia zaidi ya Mil 90 kwa miradi ya nyuki.

Meneja wa shirika lisilo la kiserikali la Future Development Initiatives (FU-DI) lenye makazi yake Ikungi mkoa wa Singida, Jonathan Njau akimkaribisha ofisini kwake rais wa shirikisho la wafuga nyuki duniani, Gilles Ratia.
Rais wa shirikisho la wafuga nyuki duniani Gilles Ratia (wa tatu kulia) akifafanua jambo kuhusu mizinga ya nyuki kwa Kaimu Mkurugenzi misitu Gladnees Mkamba.Wa kwanza kulia ni mtendaji mkuu misitu, Juma Mgoo na anayefuatia ni Meneja shirika la Future Development Initiatives Jonathan Njau.
Mizinga ya kienyeji iliopo kwenye shamba darasa la ufugaji nyuki kisasa katika kijiji cha Mahambe tarafa ya Ikungi mkoa wa Singida.

Rais wa shirikisho la wafuga nyuki duniani Gilles Ratia akichukua picha ya mizinga ya kisasa ya shamba darasa lililopo kwenye kijiji cha Mahambe tarafa ya Ikungi mkoa wa Singida.
Banda la mizinga kwenye shamba darasa la ufugaji Nyuki kisasa lililopo katika kijiji cha Mahambe tarafa ya Ikungi mkoa wa Singida.
Kaimu mkurugenzi wa misitu Gladnes Mkamba (kulia) akiteta  jambo na  meneja wa shirika la Future Development Initiatives Jonathan Njau (kushoto).Katikati ni rais wa shirikisho la wafuga nyuki duniani, Gilles Ratia.

WAKAZI wa jimbo la Singida mashariki,wamehimizwa kujiunga/kuanzisha vikundi na kuvisajili,ili kujijengea mazingira mazuri ya kunufaika na misaada mbalimbali inayotolewa na shirika lisilo la kiserikali la Future Development Initiatives (FU-DI) ikiwemo ya ufugaji nyuki.

Imedaiwa kujiunga au kuanzisha vikundi na kuvisajili, kunasaidia pia kujijengea mazingira mazuri ya kukopesheka na taasisi za kifedha.


Wito huo umetolewa na Meneja wa shirika la FU-DI, Jonathan Njau, wakati akitoa taarifa fupi juu ya majukumu ya shirika hilo kwa rais wa shirikisho la wafugaji nyuki duniani Gilles Ratia, aliyetembelea shamba darasa la ufugaji nyuki kisasa la FU-DI.

Alisema FU-DI linatarajia kutumia zaidi ya shilingi 97 milioni kugharamia miradi ya ufugaji nyuki kwa njia za kisasa,ili kumkomboa mkazi wa jimbo hilo la Singida mashariki.

Njau ambaye kitaalum ni mwanasheria,alisema ili mkazi aweze kunufaika na ufugaji huo,anawajibika kujiunga kwenye kikundi kilichosajiliwa cha watu wasiozidi 15.

“Pamoja na ufugaji bora wa nyuki,FU-DI pia inatoa misaada kwa vikundi vilivyosajiliwa vya kilimo,ufugaji mifugo,kuku wa kienyeji na ujenzi wa nyumba bora.Hii ni fursa nzuri kwa kila mkazi wa jimbo letu kuchangamkia misaada ya uhakika ambayo itamkomboa kiuchumi na hivyo kuishi maisha bora”,alisema.


Kwa upande wake rais Ratia,alilipongeza shirika la FU-DI, kwa madai  kuwa linamejizatiti vizuri kuwakomboa wananchi kiuchumi kupitia ufugaji bora wa nyuki.

No comments:

Post a Comment