Tuesday, October 7, 2014

Mfuga nyuki wa tuzo ya ‘Rais’ akoromea wanavijiji.

Rais wa shirikisho la wafuga nyuki duniani Gilles Ratia (wa tatu kulia) akifafanua jambo kuhusu mizinga ya nyuki kwa Kaimu Mkurugenzi misitu Gladnees Mkamba.Wa kwanza kulia ni mtendaji mkuu misitu, Juma Mgoo na anayefuatia ni Meneja shirika la Future Development Initiatives Jonathan Njau.

MSHINDI wa tuzo ya Rais  juu ya ufugaji  bora wa nyuki  kwa mwaka jana  Jackson Sombi,  wa mkoani Singida, ameibua tuhuma nzito  dhidi ya wana-kijiji wenzake akidai kuwa  ndio wanaokwamisha juhudi zake za kutaka kujikomboa kiuchumi kupitia uzalishaji wa asali na nta.

Sombi ametoa tuhuma hizo mbele ya Rais wa Shirikisho la Kimataifa la wafugaji  wa nyuki (APIMONDIA), Gilles Ratia,  wakati alipotembelea eneo la  hifadhi ya mfugaji nyuki huyo iliyopo katika kijiji cha Msikii halmashauri ya Wilaya ya Singida.

Amedai kuwa hifadhi yake yenye ukubwa wa kilometa za mraba 1,364 ikiwa na jumla ya mizinga
238, imekuwa ikiingiliwa mara kwa mara na wanakijiji  wenzake  ambao wanakata miti ovyo, kuchoma mkaa, kuchungia  mifugo na wengine  kukata kuni.

Amesema hali hiyo imesababisha kati ya mizinga 238 iliyopo kwenye hifadhi yake, 130 kubaki na nyuki, baada ya makundi mengine kukimbia kutokana na bughudha za shughuli za kibinadamu.

Sombi  ambaye  ni mfugaji maarufu wa nyuki mkoani Singida,  amesema licha ya Rais Jakaya  Kikwete,  kutambua umuhimu wa   sekta ndogo ya nyuki na kuanza kutoa tuzo kwa wafugaji bora,  lakini  bado  kuna haja kwa Serikali kuweka sheria itakayowalinda wafugaji nyuki binafsi dhidi ya hujuma mbali mbali za pamoja na watu wakorofi na wenye husuda.


Shirikisho la Kimataifa la Wafugaji Nyuki (APIMONDIA) lenye makao yake makuu nchini Italy lilianzishwa miaka 120 iliyopita ambapo kwa sasa lina nchi wanachama 130  zenye  wafugaji nyuki milioni saba.

No comments:

Post a Comment