Tuesday, October 7, 2014

SEMA yatumia shilingi milioni 380 kusambaza Maji Iramba.

Mtendaji mkuu wa shirika la MEDICOR la nchini Uingereza, Fortunat Walther (wa kwanza kushoto) akitoa maelezo juu ya ujenzi wa visima vya maji kwa meneja wa SEMA, Ivo Manyaku, wakati Walther alipotembelea miradi hiyo inayofadhiliwa na shirika lake.
Meneja wa shirika la SEMA, Ivo Manyaku (wa pili kulia mbele), akitoa maelezo juu ya ujenzi wa visima vya maji wilaya ya Iramba, kwa mtendaji mkuu wa shirika la MEDICOR la nchini Uingereza, Fortunat Walther (wa kwanza kushoto).Shirika la MEDICOR linafadhili miradi ya maji na usafi wa mazingira inayotekelezwa na SEMA.

Mtendaji mkuu wa shirika la MEDICOR la Uingereza, Fortunat Walther, akipiga picha ya jengo la kisima kilichojengwa wilayani Iramba.

SHIRIKA lisilokuwa la kiserikali Linaloboresha na Kusimamia Mazingira ili kuleta Maendeleo Endelevu (SEMA) la mjini Singida limetumia zaidi ya sh milioni 380 kwa ajili ya utekelezaji  mradi wa maji wilayani Iramba, mkoani Singida kati ya Julai 2013 na Machi mwaka huu.

Meneja wa Shirika la SEMA (Sustainable Environment Management Action), Ivo Manyaku, alisema kuwa mradi huo uliofadhiliwa na Shirika la WaterAid la jijini Dar es Salaam, umetekelezwa katika vijiji viwili vya Mgongo na Kisunga-Shelui pamoja na kitongoji cha Kibululu wilayani humo.

Manyaku alisema kuwa mradi huo umelenga kufaidisha jumla ya wakazi 7,800 wa maeneo hayo kutokana na shida kubwa ya maji iliyokuwa ikiwakabili kabla ya mradi huo kuanza.

Kutokana na kukamilika mradi huo, Manyaku alisema kuwa asilimia 85 ya wakazi wa maeneo hayo sasa watapata maji safi na salama.

Mara baada ya kuzindua mradi huo, Mtendaji Mkuu wa Shirika la MEDICOR la nchini Uingereza, Fortunat Walther, aliutaka uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba kuutunza, kuulinda na kuufanyia matengenenezo ya mara kwa mara mradi huo ili uweze kuwa endelevu.

Baadhi ya wakazi wa maeneo hayo walisema kuwa ujio wa mradi huo umekuwa ni ukombozi mkubwa kwao, hasa kwa akina mama waliokuwa wakitumia muda mwingi kufuata maji mtoni, ambayo hata hivyo hayakuwa safi wala salama.

“Kabla ya mradi huu, tulikuwa tunaamka alfajiri kwenda mtoni kufuata maji au wakati mwingine tulikuwa tunaletewa na tela na kuuziwa na wafanyabiashara hao kwa bei ya sh 300 kwa ndoo moja lakini sasa tunapata kwa sh 50 tu” alisema Amina Juma ambaye aliungwa mkono na Amina Mkoma.

Naye Juma Japhet alisema kuwa kabla ya  hapo akina mama walikuwa wanahangaika kufuata maji mbali hivyo kupoteza muda mwingi kusaka maji badala ya kutumia muda huo kufanya shughuli za maendeleo.

No comments:

Post a Comment