Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Singida, SACP Geofrey Kamwela.
WATU watatu mkoani Singida, wamefariki dunia katika matukio tofauti likiwemo la mkulima moja kupigwa vibaya na askari mgambo akituhumiwa kuvunja mlango wa ofisi ya afisa mtendaji wa kijiji.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Singida, SACP Geofrey Kamwela alisema katika tukio la kwanza,mkulima mkazi wa kijiji cha Milade tarafa ya Kinyangiri wilaya ya Mkalama,Salum Abrahamani (42) amefariki dunia Septemba mbili mwaka huu saa 6.10 usiku.
Alisema siku ya tukio. Abrahaman alivunja mlango wa ofisi ya mtendaji wa kijiji hicho alikokuwa amefungiwa kwa kosa la kumjeruhi Saidi Nyuha (25).
“Baada ya kuvunja mlango huo, marehemu alienda nyumbani kwake kulala. Baada ya kubaini kuvunjwa kwa mlango huo,askari mgambo Shaban Idd (28),Aman Ramadhan na Shaban Adamu,walimfuata marehemu nyumbani kwake na
kumkamata akiwa amelala”,alisema Kamwela.
Alisema baada ya wanamgambo hao kumkamata,walimpiga sehemu mbalimbali za mwili,na baada ya kuzirai,walimbeba na kumrudisha katika ofisi ya mtendaji wa kijiji na haikuchukua muda mrefu alifariki dunia ndani ya ofisi hiyo ya serikali ya kijiji.
“Kwa sasa tunamshikilia askari mgambo Shaban Idd,wakati msako mkali unaendelea kuwasaka askari mgambo Aman Ramadhani na Shaban Adamu waliofanikiwa kutoroka”alisema.
Katika tukio jingine, Kamwela alisema kuwa Rupia Shija (35) mkulima mkazi wa Kahama mkoa wa Shinyanga,amefariki dunia septemba mosi mwaka saa 5.30 usiku baada ya kupigwa na wananchi wenye hasira kali.
Alisema Shija ameuawa baada ya kukutwa juu ya dari ya nyumba ya kulala wageni ya Vunjo iliyopo mtaa wa Ipembe mjini Singida akiwa na lengo la kutoboa bati ili kuwaibia wateja/wapangaji waliokuwa wamepanga kwenye nyumba hiyo.
“Siku ya tukio,Shija alikuwa mpangaj wa nyumba ya kulala ya Vunjo chumba no.nane.Alipofanyiwa upekuzi wa maungoni,alipatikana na funguo bandia (master key) ambazo zina uwezo wa kufungua milango mingi.Pia alikutwa na funguo zingine ambazo alitoroka nazo kutoka nyumba nyingine ya kulala wageni”,alisema kamanda huyo.
Wakati huo huo, Kamwela amesema mwili wa mwanaume anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 30,umeokotwa juzi saa nane usiku kando kando ya barabara ya mtaa wa Dk.Salmin kata ya Misuna mjini Singida.
Alisema mwili wa marehemu huyo mwanaume,ulizungukwa na vipande vya matofali vinavyohisiwa vilitumika kuumuulia mwanaume huyo ambaye mwili wake umehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya mkoa mjini Singida.
No comments:
Post a Comment