Thursday, November 20, 2014

Katibu tawala Singida ataka mikakati kuwekwa kuongeza wakulima wanaotumia mbegu bora.

Katibu Tawala mkoa wa Singida, Liana Hassan, akizungumza kwenye ufunguzi wa semina juu ya kuongeza upatikanaji wa mbegu bora na mbolea kwa wakulima wadogo wadogo kwa kuimarisha masoko ya pembejeo katika mikoa ya Singida na Dodoma.
Baadhi ya wakulima wadogo wadogo mkoa wa Singida na Dodoma,wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa kwenye semina ya siku mbili iliyohusu kuongeza upatikanaji wa mbegu bora na mbolea.


KATIBU tawala mkoa wa Singida, Liana Hassan, amewahimiza wadau mbalimbali wanaojishughulisha na sekta ya kilimo,kuweka mikakati ya kuhakikisha zaidi ya aslimia 85 ya wakulima wawe wanatumia mbegu bora,ili kuleta mapinduzi ya kweli ya kilimo na kuwa cha kibiashara zaidi, katika mikoa ya Singida na Dodoma.

Hassan alisema mapinduzi hayo ya kilimo cha kibiashara, yaweze kuwatoa wakulima kwenye kilimo cha kujikimu ambapo kwa sasa matumizi ya pembejeo bora ni chini ya aslimia 40 tu.

Katibu tawala huyo aliyasema hayo wakati akifungua warsha ya siku mbili iliyohusu kuongeza upatikanaji wa mbegu bora na mbolea, kwa wakulima wadogo wadogo kwa kuimarisha masoko ya pembejeo mikoa ya Singida na Dodoma.

Akiijengea nguvu hoja yake hiyo, alisema ili kupandisha kiwango hicho cha kutoka asilimia 40 hadi zaidi ya aslimia 85 watakao tumia pembejeo bora,kunahitajika kuwajengea uwezo zaidi mawakala na kuzidi kuongeza idadi ya majaribio.

Katika hatua nyingine Katibu tawala huyo, alitumia fursa hiyo kulipongeza shirika la FIPs Africa (farm input promotion) kwa mfumo wao wao kuwafikia wakulima kwa kuwahamasisha kutumia njia mbalimbali za matumizi bora ya pembejeo.


“Kwa kipindi hiki chote nimeambiwa kuwa FIPs kwakushirikiana na halmashauri zetu,wamejenga mtandao wa wakulima ambao wamejiajiri wenyewe kupitia kuuza mbegu na kuchanja kuku”,alisema katibu huyo.

Akifafanua zaidi,Hassan alisema kuwa FIPs hawakuishia hapo,bali pia wamewasaidia wakulima wa mkoa wa Dodoma na Singida kuboresha udongo,kuboresha mazingira na hatimaye kuwezesha mkoa hii kujitosheleza kwa chakula.


“Pia nimeambiwa kuwa kupitia warsha hii, mtafanya mapitio ya shughuli ambazo zimefanyika tangu mradi huu uliopoanza.Ni imani yangu kwamba mapitio hayo yatawasaidia kutengeneza mpango kazi na mapendekezo yatakayosaidia kuendeleza kufanya shughuli zilizoanzishwa baada ya mradi huu kumaliza muda wake”,alisema Hassan.

No comments:

Post a Comment