Thursday, November 20, 2014

135 wafa katika ajali Singida.

Kamanda wa Jeshi la polisi mkoa wa Singida, ACP, Thobias Sedoyeka ,akitoa taarifa ya utendaji kazi mkoani Singida kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Septemba mwaka huu.

Baadhi ya waandishi wa habari na askari polisi waliohudhuria hafla ya kamanda wa polisi mkoa wa Singida kwa ajili ya kutoa taarifa ya utendaji kazi kwa kipindi cha miezi tisa.


JUMLA ya ajali 89 za barabarani, zimetokea mkoani hapa na kusababisha vifo vya watu 135 katika kipindi cha kuanzia Januari  hadi Septemba mwaka huu.

Hayo yamesemwa na kamanda wa polisi mkoa wa Singida, ACP,Thobias Sedoyeka, wakati akitoa taarifa yake ya utendaji kazi kwa kipindi cha miezi tisa iliyopita kwa waandishi wa habari.

Alisema hata hivyo idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na ajali hizo, imeongezeka kwa watu 39 ikilinganishwa na watu 96 waliopoteza maisha kwenye ajali 85 zilizotokea mwaka jana.

Sedoyeka alisema pia ajali za barabarani zipatazo 63 zilizotokea katika kipindi hicho,zimesababisha watu 346 kupata majeraha mbalimbali.

“Katika kipindi cha Januari hadi Septemba mwaka jana, ajali 91 zilitokea na kupelekea watu 267 kujeruhiwa.Hivyo kulikuwa na upungufu wa ajali za majeruhi 28 pamoja na ongezeko la watu 79 waliojeruhiwa ikilinganishwa na ajali za mwaka huu”,alisema kamanda huyo

Katika hatua nyingine,Sedoyeka alisema kuwa katika kipindi hicho cha Januari hadi Septemba mwaka huu,jumla ya madereva 59 wa vyombo vya moto,wamefikishwa mahakamani ikilinganishwa na 98 waliofikishwa mahakamani katika kipindi hicho kwa mwaka jana.

Wakati huo huo, kamanda Sedoyeka alisema kuwa kitengo cha usalama barabarani kimekusanya zaidi ya shilingi 631.6 milioni zilizotokana na faini mbalimbali zilizotozwa kwa makosa 20,900 ya usalama barabarani.

No comments:

Post a Comment