Tuesday, November 25, 2014

Auawa na kuchomwa moto kwa tuhuma za ujambazi.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida, ACP, Thobias Sedoyeka, akitoa taarifa ya wananchi kumuua kijana Hussein Jumanne Kisuke (31) anayedaiwa kuwa ni jambazi sugu. Baada ya kumshambuliwa kwa silaha za jadi na kufariki dunia na kisha kumchoma moto.

Mtuhumiwa wa Ujambazi mkazi wa Misuna Hussein Jumanne Kisuke (31) juzi  alipigwa na wananchi wa Misuna mjini Singida kwa kutumia silaha za jadi na kuuwawa na kisha kuchomwa moto.

Kamanda wa polisi mkoa wa Singida, ACP, Thobias Sedoyeka, alisema tukio hilo limetokea juzi saa 5.15 asubuhi huko katika maeneo ya Kipungua kata ya Misuna tarafa ya Mungumaji manispaa ya Singida.

Alisema Kisuke alikuwa akitafutwa muda mrefu kuhusiana na tuhuma mbalimbali za ujambazi na wizi wa pikipiki.

“Kwa ujumla Hussein Kisuke  alikuwa mzoefu wa matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha katika mji wa Singida. Siku ya tukio wananchi walimuona akipita katika maeneo ya Kipungua na hivyo
kumvamia na kuanza kumshambulia kwa kutumia silaha za jadi na kisha kumchoma moto”alisema Sedoyeka.

Kamanda huyo alisema hadi sasa hakuna mtu/watu waliokamatwa kuhusiana na mauaji hayo kwani wananchi waliojichukulia sheria mkononi,walitorokea kusikojulikana baada ya kufanya mauaji hayo.


Sedoyeka ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuacha mara moja tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake watoe taarifa polisi,ili mtuhumiwa/watuhumiwa wakamatwe na kufikishwa mahakamani.

No comments:

Post a Comment