Tuesday, November 25, 2014

23 washikiliwa na Polisi kwa mauaji ya watu 4.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida, ACP, Thobias Sedoyeka.

JESHI la polisi mkoa wa Singida, linawashikilia watu 23 wakazi  wa kijiji cha Nkyala kata ya shelui wilaya Iramba mkoa wa Singida, kwa tuhuma ya kudaiwa kuuawa kwa makusudi wezi wanne wa madume ya Ng’ombe.

Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Singida, ACP, Thobias Sedoyeka, alisema watu hao kati yao 21 wanatuhumiwa kwa mauaji na wawili wanatuhumiwa kuiba ng’ombe watatu.

Aliwataja watu hao waliouawa kwa tuhuma ya wizi wa madume matatu ya ng’ombe ni Magupa Ngelela (32), Hemedi Masasi (29), wote wawili ni wakazi wa kijiji cha Nkyala.Wengine ni Saidi Hamisi (32) mkazi wa kijiji cha Kinkungu na Didas Mwigulu (36) mkazi wa kijiji cha Mgongo.

Akifafanua,alisema novemba 19 mwaka huu saa saba usiku,watu hao wanne kwa pamoja inadaiwa
walivunja zizi la Omari Iddi mkazi wa kijiji cha Nselembwe na kuiba madume matatu ya ng’ombe.

Alisema asubuhi yake,watu hao walifumwa wakiwa tayari wameisha wachinja Ng’ombe hao na bila kuwachuna,waliwakata kata na kujaza nyama kwenye mifuko ya sadarusi.

“Walivamiwa na kuanza kupigwa kwa silaha za jadi na walipofariki dunia,walichomwa moto”,alisema.

Alisema uchunguzi ukikamilika,watu watakaobainika kuhusu na mauaji hayo ya kikatili,watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma inayowakabili ya mauaji na wizi wa Ng’ombe.


“Kwa sasa hatuwezi kutangaza hadharani majina ya watuhumiwa tunaoendelea kuwashikilia, kwa vile kitendo hicho kinaweza kuharibu kazi ya upelelezi ambao bado unaendelea”, alisema kamanda Sedoyeka.

No comments:

Post a Comment