Saturday, April 25, 2015

Pato la mkulima wa Tumbaku nchini limeongezeka na kufikia milioni 4.9 kwa mwaka.

Mkuu wa wilaya ya Manyoni mkoani Singida,Fatma Toufiq, akifungua mkutano wa wadau wa zao la Tumbaku nchini unaoendelea kwenye ukumbi wa mikutano wa chuo cha VETA mjini Singida.Dc huyo alifungua mkutano huo kwa niaba ya mkuu wa mkoa.
Baadhi ya viongozi na wadau wa zao la Tumbaku nchini wanaohudhuria mkutano wa kujadili maendeleo ya zao hilo hapa nchini.

MAPATO ya mkulima mmoja mmoja wa tumbaku nchini, yameongezeka kutoka wastani wa zaidi ya shilingi 2.2 milioni kwa kipindi cha mwaka 2011/2012 hadi zaidi ya wastani wa shilingi 4.9 milioni kwa mwaka 2013/2014 sawa na aslimia 121.

Hayo yamesemwa na mkuu wa mkoa wa Singida,Dk.Parseko Kone,wakati akifungua semina na mkutano wa (appreciation) wa mwaka wa 2015 unaoendelea kwenye ukumbi wa mkutano wa chuo cha VETA mjini hapa.

Kwa upande wa ushuru wa halmashauri za wilaya, alisema ushuru huo umeongezeka hadi kufikia shilingi bilioni 10 mwaka 2013/2014 sawa na aslimia 74 ya mapato ya ushuru wa shilingi bilioni 10.8 mwaka 2011/2012.

“Mapato ya fedha za kigeni yameongezeka kutoka dola za kimerekani 302.8 milioni mwaka 2011 hadi dola 359,9 milioni  mwaka jana,sawa na ongezeko la aslimia 19,na serikali kuu nayo imenufaika kwa kulipwa kodi ya shilingi 126.4 milioni mwaka 2011″,alisema Dk.Kone kwenye hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na mkuu wa wilaya ya Manyoni, Fatma Toufiq.

Katika hatua nyingine,mkuu huyo wa mkoa,aliziagiwa halmashauri za wilaya kupitia kamati zake za mazingira za vijiji zichukue hatua za kuhakikisha kuwa hatua thabiti zinachukuliwa katika kusimamia uvunaji miti na utunzaji miti,ili kulinda rutuba ya udongo.

“Nimeambiwa kuwa sheria ya sekta ndogo ya tumbaku inamktaka kila mkulima wa tumbaku apande miti.Pia nimearifiwa kuwa katika mpango mpya wa uhifadhi wa mazingira,kila mkulima wa tumbaku anapaswa kupanda miti 550 katika shamba lake kila msimu na miti 25  katika mashamba ya jumuia”, alisema na kuongeza;

“Ninayo taarifa kuwa wanunuzi wa nje wa tumbaku yetu hawako tayari kununua tumbaku Tanzania kama hatujapanda miti,zaidi ya hilo,nimeambiwa kuwa kiasi cha tumbaku itakayopandwa msimu ujao (2015/2016),itategemea kiasi cha miti iliyopo,hii ikiwa na maanda kuwa kama miti iliyopo ni michache,tumbaku itakayopandwa,itakuwa kidogo”.

Dk.Kone alitoa rai kwa wakulima na wadau wote wa tumbaku kuzingatia sana suala la mazingira,ili tumbaku inayozalishwa nchini,iweze kukubalika katika soko la dunia.

Kwa mujibu wa Dk.Kone,msimu 2011/2012,mkoa wa Singida ulizalisha kilo 2,102,824 ambazo ni sawa na aslimia tatu ya uzalishaji ki-taifa ambapo kilo 74,239,990 zilizalishwa.Msimu 2012/2013 jumla ya kilo 923,281 zilizalishwamswa na aslimia 1.07 ya uzalishaji wa nchi nzima,katika msimu huo uzalishaji ki-taifa ulikuwa kilo 86,343,099.Msimu uliopita wa 2013/2014,mkoa wa Singida ulizalisha kilo 995,093 ambazo ni aslimia 0.9 ya uzalishaji wote kwa nchi nzima ambao ulikuwa ni kilo 105,889,812 za tumbaku.

Zaidi ya wajumbe wa mkutano huo unaoendelea kwenye ukumbi wa mikutano wa chuo cha VETA mjini Singida,wametoka mkoa wa Mbeya,Iringa,Ruvuma,Tabora, Kigoma, Shinyanga, Geita, Kagera, Morogoro, Katavi na Mara.

No comments:

Post a Comment