Pichani ni majengo ya kituo cha afya cha tarafa ya Ndago, wilayani Iramba yanayokabiliwa na uhaba mkubwa wa dawa kwa wanachama wake wa Mfuko wa afya ya jamii (CHF)katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Oktoba hadi disemba,mwaka jana
LICHA ya Wilaya ya Iramba,Mkoani Singida kutajwa kuongoza nchini kwa kuwa na wanachama wengi wa Mfuko wa Afya ya Jamii Nchini (CHF) baada ya zaidi ya asilimia 60 ya kaya zake kujiunga,lakini bado kuna malalamiko ya huduma duni za afya katika baadhi ya vituo vyake.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi,baadhi ya wanachama wa Mfuko huo wamedai kuwa pamoja na kutoa fedha kwa ajili ya kujiunga na CHF ili kuwa na uhakika wa matibabu pindi watakapougua,lakini katika Kituo cha Afya cha Tarafa ya Ndago,wilayani humo bado huduma ni mbovu.
Walidai kuwa kwa zaidi ya miezi minne sasa,kila wanapokwenda kufuata huduma za matibabu katika kituo hicho cha afya wamekuwa hawapatiwa dawa za magonjwa mbalimbali yanayowasumbua.
Walisema kuwa kutokana na kukosekana kwa dawa katika kituo hicho,wanachama hao wa CHF wamekuwa
wakiandikiwa aina za dawa inayotakiwa kutibu maradhi yao na kushauriwa kwenda kununua kwenye maduka ya dawa muhimu ya watu binafsi,hali ambayo inayowasababishia gharama zisizo za lazima.
Walifafanua kuwa licha ya viongozi wa ngazi mbali mbali kwenye maeneo yao kuwahamasisha wajiunge na mfuko huo ili kuchangia kuboresha upatikanaji wa dawa,vifaa tiba pamoja na miundombinu lakini hali imekuwa tofauti katika kituo chao cha afya na kuanza kuwakatisha tamaa.
Walidai kuwa wamekuwa hawafahamu fedha za michango yao wanayochangia kwenye mfuko huo wa CHF zinapelekwa wapi au zinatumika kununulia kitu gani badala ya dawa kwa ajili kuwasaidia kuwatibu maradhi mbalimbali pindi wanafamilia wa kaya wanachama wanapougua.
Sofia Bakari na Jenifer Pendaeli wote wakazi wa Ndago ni miongoni mwa wanachama wa CHF waliosema kuwa hakuna faida yeyote ile ya kujiunga na mfuko kwani hawapati sitahiki yao ya matibabu badala yake wanalazimika kuingia gharama nyingine ya kujinunulia dawa madukani.
Akizungumzia malalamiko hayo ya wananchi wa tarafa ya Ndago,wilayani Iramba na maeneo jirani, Kaimu Mganga wa Kituo cha afya Ndago,Restituta Nkuu alikiri kwamba kituo hicho hakijapokea dawa za kutosha kwa miezi mitatu katika kipindi cha kuanzia Oktoba hadi Disemba,mwaka jana.
Nkuu alisema kuwa licha ya kituo hicho kuwasilisha wilayani zaidi ya shilingi laki sita kila mwezi,lakini dawa zinazotolewa kituoni hazitoshelezi mahitaji ya zaidi wa wakazi 19,000 waliopo.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba,Halima Mpita amesema kuwa katika kipindi cha miezi mitatu ya mwaka jana kulikuwa na uhaba wa upatikanaji wa dawa.
Mpita ambaye kitaaluma ni afisa mipango alielezea sababu za kuwepo kwa tatizo hilo kuwa ni kubadilika kwa mfumo wa ununuzi wa dawa kutoka kwa wazabuni wengine na kuanza kununua kwenye bohari ya madawa (MSD) na ndipo katika kipindi hicho serikali haikuwa imepeleka fedha za dawa za wilaya hiyo hivyo walipopeleka fedha,zilikatwa na kuingizwa kwenye deni walilokuwa wakidaiwa.
No comments:
Post a Comment